// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KARIBU LIGI KUU YA 55, TUNATARAJIA UCHEZESHAJI WA HAKI ILI KUPATA BINGWA HALALI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KARIBU LIGI KUU YA 55, TUNATARAJIA UCHEZESHAJI WA HAKI ILI KUPATA BINGWA HALALI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, August 22, 2018

    KARIBU LIGI KUU YA 55, TUNATARAJIA UCHEZESHAJI WA HAKI ILI KUPATA BINGWA HALALI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAADA ya miaka 16 ya kampuni ya simu ya Vodacom kuibeba Ligi Kuu ya Tanzania, hatimaye wameitupa na msimu huu hakutakuwa tena na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kama ilivyozoeleka.
    Vodacom walioanza kudhamini Ligi Kuu mwaka 2002 wakiipokea Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yao ya Safari Lager, hawajaafikiana na TFF juu ya mkataba mpya na michuano inaanza leo.
    Ni Benki ya Biashara ya Kenya (KBC) wameweka fedha kudhamini Ligi Kuu ambao wametoa dau dogo mno, kiasi cha Shilingi Milioni 420 kwa mwaka, ambayo haifikii hata nusu ya fedha zilizokuwa na Vodacom kwa mwaka.
    Kwa udhamini wa KCB, kila timu itapata gawio la Sh. Milioni 15 kwa msimu mzima na ni kwamba Ligi Kuu itabebwa mno na fedha za haki za matangazo ya Televisheni kutoka kwa Azam TV ambao wanatoa gawio la Sh. Milioni 162 kwa kila timu kwa msimu.   
    Mshambuliaji na Nahodha wa Simba SC, John Bocco akiruka dhidi ya wachezaji wa Kagera Sugar

    Pamoja na yote, Ligi Kuu inarejea tena kwa mara ya 55 tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 kwa wigo finyu na hali dunia kabisa, ikishirikisha klabu za Dar es Salaam pekee.
    Timu 20 zinatarajiwa kujitupa dimbani kuwania pointi za mwanzoni, katika mbio za kusaka ubingwa wa ligi, unaoshikiliwa na Wana Jangwani, Yanga SC. 
    Katika mechi za ufunguzi, Simba SC wakitoka kubeba Ngao ya Jamii kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi iliyopita, leo wataikaribisha Tanzania Prisons kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Alliance FC na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Coastal Union na Lipuli FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, zote zikianza Saa 10:00.
    Ligi hiyo itaendelea kesho na mabingwa wa kihistoria, Yanga SC watamenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru kuanzia Saa 12:00 jioni, JKT Tanzania watamenyana na KMC kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Dar es Salaam, Stand United wataikaribisha African Lyon kuanzia Saa 10:00 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Azam FC watamenyana na Mbeya City kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
    Ikumbukwe msimu huu Ligi Kuu itakuwa na timu nne zaidi kutoka 16 za msimu uliopita, Bodi chini ya Mkurugenzi wake, Boniphace Wambura ikitambulisha mfumo mpya wa mashindano hayo.  
    Historia ya Ligi hiyo inaanzia mwaka 1929 ilipoanzishwa kifukara, tu kwa sababu ya mapenzi ya watu na soka wakaamua kuungana na kuanzisha michuano ya kutafuta bingwa, ingawa ni timu za Dar es Salaam pekee zilizokuwa zikishiriki wakati huo.

    Utawala wa Yanga umezimwa msimu uliopita baada ya kupokonywa taji na mahasimu wa, Simba SC

    Kufika mwaka 1965, ilianzishwa michuano ya Klabu Bingwa Tanzania, ambayo ilikuwa inaanzia ngazi ya Wilaya, ikichezwa kwa mtindo wa mtoano, ingawa pia katika miaka miwili ya mwanzoni, timu za Dar es Salaam pekee ndizo zilizoshiriki.
    Katika mfumo huo, bingwa wa kwanza ilikuwa ni klabu ya Sunderland ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ilifanikiwa kutetea ubingwa wake msimu uliofuata, kabla ya kuutema kwa Cosmopolitan ya Dar es Salaam pia mwaka 1967.
    Lakini wakati wote huo, bado Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hivyo Sunderland hawakuwahi kucheza michuano ya Afrika. Cosmo ingekuwa ya kwanza kucheza Klabu Bingwa Afrika mwaka 1968 kama isingejitoa, lakini kwa kujitoa kwao, Yanga ilifungua historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza mwaka 1968, kabla ya kuutetea mara nne mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970, 1971 na 1972. Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na kuitwa Simba kurejesha taji lake mwaka 1973.
    Simba ilishindwa kuutetea ubingwa wake msimu uliofuata mwaka 1974 baada ya kupokonywa na Yanga katika fainali ya kihistoria iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kwa kuchapwa mabao 2-1.  
    Mwaka 1975 Yanga iliutema ubingwa huo kwa Mseto SC ya Morogoro, iliyoweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa nchi.
    Lakini Mseto ilishindwa kuteteqa taji hilo, ikapokonywa na Simba msimu uliofuata- na Wekundu wa Msimbazi walifanikiwa kutetea ubingwa huo kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.
    Siri ya kutawala kwa Simba kwenye ligi hiyo kwa miaka yote hiyo ni kuyumba kwa Yanga baada ya kukumbwa na mgogoro mkubwa 1976, uliosababisha kukimbiwa na wachezaji wote nyota, hivyo kuanza upya kabisa kuunda timu. 
    Ni ndani ya kipindi hicho Simba iliweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 5-0 na Yanga mwaka 1968, wakati nayo ilipowatandika watani wao hao wa jadi 6-0 mwaka 1977.  
    Juni 1, mwaka 1968 Yanga iliigaragaza Simba 5-0, mabao yake yakitiwa kimiani na Maulid Dilunga (sasa marehemu) katika dakika za 18 kwa njia ya penalti na 43, wakati mengine yalitiwa kimiani na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 kabla ya Kitwana Manara kupachika la kuhitimisha karamu ya mabao dakika ya 86.
    Julai 19, mwaka 1977 Simba nayo ililipa kisasi kwa kuibugiza Yanga mabao 6-0, wafungaji wakiwa ni Abdallah 'King' Kibadeni aliyetikisa nyavu mara tatu katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73 na Selemani Sanga wa Yanga alijifunga dakika ya 20.
    Kufika mwaka 1981, tayari Yanga ilikuwa imara tena na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara ingawa msimu uliofuata iliutema kwa Pan African. 
    Kuanzia mwaka 1982, mfumo wa Ligi ya Tanzania ulibadilishwa na kukawa na ligi tatu, kwanza ni Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza visiwani Zanzibar na Ligi Kuu ya Muungano.
    Yaani baada ya kupatikana washindi wawili wa juu wa kila ligi, Bara na Visiwani, walikutana kwenye Ligi Kuu ya Muungano, kutafuta bingwa wa Tanzania na washindi wake.
    Wakati huo, bingwa wa Ligi ya Muungano alikwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili alicheza Kombe la Washindi.
    Baadaye timu ziliongezwa na kuwa tatu kila upande katika Ligi ya Muungano.
    Mwaka 1983, Yanga ilirejesha taji hilo kwenye himaya yake, ingawa msimu uliofuata ililitema tena kwa Simba.  Kwa ujumla muongo mzima wa 1980, taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara lilikuwa la kukoponyana, kwani Simba nayo mwaka 1985 ilipokonywa taji hilo na Yanga, ambayo nayo ililitema kwa timu mpya katika Ligi Kuu msimu wa 1986, Tukuyu Stars ya Mbeya.
    Tukuyu nayo iliwarejeshea Yanga taji lao mwaka 1987, wakati mwaka 1988 Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga ilijiingiza katika orodha ya timu zilizowahi kutwaa taji hilo. Mwaka 1989, Yanga ilifunga orodha ya mabingwa ya mabingwa wa muongo huo kwa kutwaa tena ubingwa wa Bara.
    Simba iliibuka mwaka 1990 na kutwaa ubingwa huo, ikitoka kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita. 
    Kupokonyana taji kuliendelea hata kwenye muongo wa 1990, kwani Simba iliutema ubingwa huo kwa Yanga mwaka 1991.
    Yanga iliutetea ubingwa huo mara mbili mfululizo katika miaka ya 1992 na 1993, kabla ya kupokonywa na Simba mwaka 1994. Simba ilifanikiwa kuutetea mara moja 1995.
    Mwaka 1996 ndipo Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilipozaliwa rasmi chini ya udhamini wa Bia ya Safari Lager, bia inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ikijulikana kama Safari Lager Premier League, Yanga ndiyo iliyokuwa bingwa wake wa kwanza. Yanga iliutetea ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo 1997 na 1998. Mwaka 1999, Yanga ikiwa tayari imetwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, alitengua matokeo hayo kwa kuiongezea Mtibwa Sugar pointi za mezani, hivyo kuipiku Yanga. Hatimaye Mtibwa ilipata ubingwa wa mezani.
    Mtibwa ilifanikiwa kutetea ubingwa mwaka 2000, kabla ya kupokonywa na Simba msimu uliofuata, 2001. Lakini Simba SC haikupata zawadi ya ubingwa kutokana na wadhamini TBL kujitoa baada ya kukasirishwa na idadi ya timu kuongezwa bila ya wao kushirikishwa.
    Bahati nzuri Vodacom wakaichukua Ligi Kuu kuanzia msimu uliofuata, lakini Simba haikuweza kutetea taji hilo baada ya kupokonywa na mahasimu wao wa jadi, Yanga walioibuka mabingwa wa mwaka 2002.
    Mwaka 2003 Simba iliyokuwa kali zaidi ilifanikiwa kuutwaa tena ubingwa huo na kuutetea mwaka 2004 kabla ya kupokonywa na Yanga 2005 ambao waliutetea 2006. Mwaka 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya mabadiliko ya kalenda yake, ikitaka Ligi yake iendane na ligi za Ulaya, hivyo ikaamua kuchezesha ligi ndogo ya mpito kumpata bingwa na mwakilishi wa Kombe la Shirikisho, kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Agosti.
    Simba iliibuka bingwa wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Yanga kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kufuatia sare ya 1-1.
    Lakini msimu uliofuata ikiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifanikiwa kuurejesha ubingwa wake msimu wa 2008 na kutetea msimu uliofuata ikiwa chini ya kocha huyo, ambaye hata hivyo msimu uliopita alitupiwa virago katia mzunguko wa kwanza tu wa ligi na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia mwenzake, Kostadin Bozidar Papic, ambaye alishindwa kubakisha taji Jangwani, baada ya Simba kuchukua kwa kishindo.
    Simba ilishinda mechi zote ikiwemo mbili dhidi ya watani wa jadi, Yanga na kutoa sare mbili tu dhidi ya Kagera Sugar Bukoba na African Lyon Dar es Salaam, hivyo kutwaa ubingwa kwa mbwembwe za aina yake na kufanikiwa kuutetea 2010.
    Mwaka 2011 Yanga SC walirejesha taji lao, kabla ya 2012 kulitema kwa Simba SC na huo ukawa mwaka wa mwisho kwa Wekundu wa Msimbazi kulitia mkononi taji la Ligi Kuu.
    Katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2013, Yanga imetwaa taji la Ligi Kuu mara nne hadi mwaka huu, ikilikosa mara moja tu, mwaka 2014 lilipochukuliwa na Azam FC.
    Lakini utawala wao ukazimwa msimu uliopita, baada ya Wekundu wa Msimbazi kubeba taji la kwanza la Ligi Kuu tangu mwaka 2012.
    Wakati Ligi Kuu ikizipoteza timu za Maji Maji na Njombe Mji FC zote za Nyanda za Juu Kusini mwa nchi zilizoshuka daraja msimu uliopita – msimu huu zimeibuka timu nyingine ambazo ni Coastal Union ya Tanga, Biashara United ya Mara, Alliance FC ya Mwanza, JKT Tanzania, African Lyon na KMC zote za Dar es Salaam.
    Coastal, Lyon, JKT, Biashara iliyokuwa ikijulikana kama Polisi Mara zote zimewahi kucheza Ligi Kuu, wakati Alliamce FC na KMC zimepanda kwa mara ya kwanza kabisa. 
    Pamoja na ongezeko la timu, TFF imerejesha mfumo wa timu mwenyeji kuchukua mapato yote ya mlanfoni huku pia timu zikiruhusiwa kusajili wachezaji 10 wa kigeni na kuwatumia wote kwa wakati mmoja.
    Karibu msimu wa 55 wa Ligi Kuu. Tunatarajia ushindani zaidi, mchezo wa kiungwana na uchezeshaji wa haki ili kupata bingwa halali. 
    Wachezaji wa Simba SC mwaka 1993 wakiingia uwanjani kwa ajili ya moja ya mechi zao za michuano ya Afrika

    MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
    1965 : Sunderland (Dar es Salaam) 
    1966 : Sunderland (Dar es Salaam) 
    1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam) 
    1968 : Yanga 
    1969 : Yanga 
    1970 : Yanga 
    1971 : Yanga 
    1972 : Yanga 
    1973 : Simba 
    1974 : Yanga 
    1975 : Mseto SC (Morogoro) 
    1976 : Simba 
    1977 : Simba 
    1978 : Simba 
    1979 : Simba 
    1980 : Simba 
    1981 : Yanga 
    1982 : Pan African 
    1983 : Yanga 
    1984 : Simba 
    1985 : Yanga 
    1986 : Tukuyu Stars (Mbeya) 
    1987 : Yanga 
    1988 : Coastal Union (Dar es Salaam) 
    1989 : Yanga 
    1990 : Simba  
    1991 : Yanga 
    1992 : Yanga 
    1993 : Yanga 
    1994 : Simba 
    1995 : Simba 
    1996 : Yanga 
    1997 : Yanga 
    1998 : Yanga 
    1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro) 
    2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)  
    2001 : Simba 
    2002 : Yanga 
    2003 : Simba 
    2004 : Simba 
    2005 : Yanga 
    2006 : Yanga 
    2007 : Simba (Ligi Ndogo) 
    2008 : Yanga 
    2009:  Yanga 
    2010: Simba SC
    2011: Yanga SC
    2012: Simba SC
    2013: Yanga SC
    2014: Azam FC
    2015; Yanga SC
    2016: Yanga SC
    2017: Yanga SC
    2018: Simba SC
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIBU LIGI KUU YA 55, TUNATARAJIA UCHEZESHAJI WA HAKI ILI KUPATA BINGWA HALALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top