BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amesema kwamba kwa uwezo wake hivi sasa anajiona anaweza kucheza popote.
Akizungumza kwa simu jana kutoka Afrika Kusini baada ya kuiongoza timu yake, Baroka FC kutoa sare ya 1-1 na Kaizer Chiefs juzi katika mchezo wa Ligi Kuu, Banda amesema kwamba kwa uwezo wake wa sasa anaweza kucheza poote duniani.
“Uwezo wangu umepanda sana ndani ya wastani wa mwaka mmoja wa kucheza Afrika Kusini, naamini kabisa kwa sasa ninaweza kucheza sehemu yoyote duniani. Ni suala la kusubiri muda tu bahati itokee nipate timu yenye maslahi makubwa kuliko hapa,”amesema Banda.
Abdi Banda amesema kwa sasa anajiona anaweza kucheza popote duniani
Katika mchezo wa juzi Uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane, Petersburg, beki Daniel Cardoso alianza kujifunga dakika ya 36 kuwapatia Baroka FC la kuongoza, kabla ya mkongwe Siphiwe Tshabalala kuisawazishia Kaizer dakika ya 43.
Matokeo hayo yanaifanya Baroka FC ifikishe pointi nne baada ya mechi tatu za mwanzo za msimu, kwani mbali ya sare hiyo, pia imeshinda mechi moja na kufungwa moja.
Banda alijiunga na Baroka FC Julai mwaka jana akitokea Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo aliichezea kwa misimu mitatu baada ya kusajiliwa akitokea Coastal Union ya Tanga.
Mume huyo wa Zabibu Kiba, dada wa mwanamuziki nyota Tanzania, Ally Kiba kwenye soka anafuata nyayo za baba yake, Hassan Banda ambaye alicheza Simba SC.
0 comments:
Post a Comment