// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); SHAABAN IDDI CHILUNDA; MTAMBO MPYA WA MABAO AFRIKA MASHARIKI NA KATI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE SHAABAN IDDI CHILUNDA; MTAMBO MPYA WA MABAO AFRIKA MASHARIKI NA KATI - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Tuesday, July 10, 2018

    SHAABAN IDDI CHILUNDA; MTAMBO MPYA WA MABAO AFRIKA MASHARIKI NA KATI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MABAO manne katika mechi moja ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kufungwa na mchezaji mmoja? Ndiyo.
    Mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda hapana shaka jana ameweka rekodi mpya katika soka ya Afrika Mashariki na Kati baada ya kufunga mabao yote ya timu yake, Azam FC ikiibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Chilunda aliyefunga mabao hayo katika dakika za 19, 33, 39 na 64 kwa sasa anacheza kwa mara ya mwisho Azam FC kabla ya kwenda Hispania kuanza kuutumikia mkataba wa mkopo wa miaka miwili Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania.
    Shaaban Iddi Chilunda ni mtambo mpya wa mabao Afrika Mashariki na Kati

    Kumbukumbu zinaonyesha hakuna mchezaji aliyewahi kufunga mabao manne katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tangu inaanzishwa mwaka 1974 – maana yake chipukizi wa Tanzania ameweka rekodi mpya.
    Na heshima zaidi kwake amefunga dhidi ya timu ngumu yenye safu imara ya ulinzi, Rayon Sport ambao pia wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa Kundi moja na vigogo wa Tanzania, Yanga SC.
    Tayari Chilunda amekwishafunga mabao saba katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu, pamoja na mawili dhidi ya Kator FC ya Sudan Kusini na moja dhidi ya Vipers FC katika hatua ya makundi.
    Na zaidi ya hayo, anasifiwa kufunga bao zuri zaidi kwenye mashindano haya hadi sasa, ambalo ni dhidi ya Vipers FC ya Uganda akimpiga kanzu kipa kabla ya kutumbukiza mpira nyavuni.
    Shaaban Iddi akikabidhiwa mpira jana baada ya kufunga mabao yote manne 

    Mabao saba ndiyo kiwango cha juu hadi sasa cha wafungaji bora wa michuano ya Kagame, idadi ambayo mara ya mwisho ilifikiwa na mshambuliaji wa Yanga, Said Rashid Bahanuzi katika michuano ya mwaka 2012 mjini Dar es Salaam, akimfuatia Chiukepo Msowoya wa APR mwaka 2010 nchini Rwanda.
    Kagame iliyopita, mwaka 2015 mjini Dar es Salaam pia mfungaji bora alikuwa mshambuliaji Michael Olunga wa Gor Mahia aliyefunga mabao matano, wakati mwaka 2014 mabao matatu yalitosha kumpa John Bocco wa Azam FC ufungaji bora wa michuano iliyofanyika nchini Rwanda.
    Na kwenye idadi kubwa ya mabao katika mchezo mmoja, mara ya mwisho mchezaji mmoja kufunga mabao mengi ilikuwa mwaka 2013 na huyo ni Mrundi, Amissi Tambwe akiwa na Vital'O ya kwao aliifunga mabao matatu dhidi ya AS Ports ya Djibouti katika ushindi wa 6-0, mchezo wa Robo Fainali.
    Na kabla ya hapo, hat trick nyingine ya Kagame ilifungwa na John Raphael Bocco mwaka 2012 akiwa na Azam FC akiiadhibu timu yake ya sasa, Simba SC kwenye Robo Fainali pia.
    Chilunda atakayefikisha umri wa miaka 20 Julai 20 mwaka huu tangu azaliwe mwaka 1998, sasa ataiongoza Azam FC katika mechi nyingine mbili, Nusu Fainali dhidi ya Gor Mahia Jumatano na Fainali, au kuwania nafasi ya tatu, akitarajiwa kuongeza mabao na kuzidi kuvunja rekodi. 
    Hongera Shaaban Iddi Chilunda; Huu ni mtambo mpya wa mabao Afrika Mashariki na Kati.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHAABAN IDDI CHILUNDA; MTAMBO MPYA WA MABAO AFRIKA MASHARIKI NA KATI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top