Joachim Low amekubali kuongeza mkataba ambao utamfanya aendelee kuwa kocha wa Ujerumani hadi mwaka 2022 PICHA ZAIDI GONGA HAPA
KOCHA Joachim Low ameongeza muda wa kuendelea kuifundisha timu ya taifa ya Ujerumani na amemjumuisha kikosini kipa majeruhi Manuel Neuer katika kikosi cha awali kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.
Shirikisho la Soka Ujerumani (DFB) leo limetangaza kwamba Low, msaidizi wa zamani wa Jurgen Klinsmann aliyemrithi mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham baada ya Ujerumani kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo mwaka 2006 nyumbani, ameongeza mkataba wa miaka minne hadi mwaka 2022.
Mkataba wake wa sasa ulikuwa unatarajiwa kumalizika kwenye michuano ijayo ya Kombe la Mataifa Ulaya mwaka 2020.
Ujerumani ambayo ilitwaa taji la nne la Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014 kwa bao la dakika za nyongeza la Mario Gotze dhidi ya Argentina Uwanja wa Maracana, imetaja wachezaji 27 wa kikosi cha awali cha kwenda kutetea taji lao Urusi mwezi ujao.
Neuer amerejea kwenye anga za kimataifa licha ya kukosekana kwenye kikosi cha klabu yake, Bayern Munich kwa sasa kwa sababu ya maumivu ya mguu, ingawa beki wa Arsenal, Shkodran Mustafi na kiungo wa Liverpool, Emre Can ni miongoni mwa wanaokosekana pamoja na Gotze.
Mshambuliaji wa Freiburg, Nils Petersen ameitwa kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kufunga mabao mengi msimu huu kwenye Bundesliga, lakini Sandro Wagner wa Bayern hayumo.
Mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Marco Reus amejumuishwa baada ya kukosekana kwenye Kombe la Dunia 2014 na Euro 2016 sababu ya kuwa majeruhi.
Baada ya mechi za kujipima nguvu na Austria na Saudi Arabia, Die Mannschaft wataanza kutetea taji lao kwa kumenyana na Mexico mjini Moscow Juni 17, kabla ya kumenyana na Sweden mjini Sochi siku sita baadaye na kukamilisha mechi zao za Kundi F dhidi ya Korea Kusini mjini Kazan.
0 comments:
Post a Comment