// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MAREFA WA LEO NA MAREFA WENGINE WA SIMBA NA YANGA, YETU MACHO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MAREFA WA LEO NA MAREFA WENGINE WA SIMBA NA YANGA, YETU MACHO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, April 29, 2018

    MAREFA WA LEO NA MAREFA WENGINE WA SIMBA NA YANGA, YETU MACHO!

    REFA Emmanuel Mwandembwa wa Arusha ndiye atachezesha mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya mahasimu wa jadi, Simba na Yanga Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Mwandembwa ambaye ni mwaka huu tu amepata beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), katika mchezo wa leo atasaidiwa na Frank Komba wa Dar es Salaam na Mohammed Mkono wa Tanga, wakati refa wa akiba atakuwa Heri Sasii.
    Mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu Oktoba 28, mwaka jana Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam ilichezeshwa na refa wa akiba leo, Heri Sasii timu hizo zikifunga bao 1-1.
    Kupitia kwa Mkuu wake wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Hajji Sunday Manara Simba SC ililalamikia uchezeshaji wa Sasii ikidai aliwapendelea mahasimu, Yanga.
    Manara aliwawekea Waandishi wa Habari video ya mchezo huo kuwaonyesha namna ambavyo refa Sasii hakutoa penalti licha ya mpira kuwagonga mikononi beki, Kevin Yondan na kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi Jumamosi.
    Huo ulikuwa mwendelezo wa malalamiko dhidi ya marefa wa Tanzania kwenye mechi za watani wa jadi, ambao kwa hakika kwa asilimia kubwa wamekuwa hawaitendei haki mechi hiyo kwa uchezeshaji wao.
    Rejea Oktoba 1, mwaka 2016, refa Martin Saanya aliyechezesha mechi ya watani hao wa jadi, alifungiwa miaka miwili kwa pamoja na Msaidizi wake, namba moja, Samuel Mpenzu kwa kuvurunda.
    Na pamoja na kuwafungia waamuzi huo kwa makosa ya kutoa maamuzi ya utata, pia Kamati ya Masaa 72 ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilifuta Kadi nyekundu ya mchezaji Jonas Mkude baada ya kubaini hakufanya kosa.
    Maamuzi ya utata ya Saanya yalisababisha vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi ya Oktoba 1, mwaka jana baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Awali, Mpenzu alikataa bao safi la Simba lililofungwa na Ibrahim Ajib mapema kipindi cha kwanza akidai aliotea.
    Mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baina ya miamba hiyo ulichezeshwa na refa Mathew Akrama kutoka Mwanza Februari 25, mwaka huu pale pale Taifa na winga Shiza Ramadhani Kichuya, kwa mara nyingine aliibuka shujaa wa Simba baada ya kutokea benchi na kuisaidia timu yake kushinda 2-1.
    Kichuya aliyempokea beki Novatus Lufunga dakika ya 55, kwanza alimsetia mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuifungia bao la kusawazisha Simba dakika ya 66 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la ushindi dakika ya 81.
    Kama Oktoba 1, na Februari 25 Yanga SC walitangulia kwa bao la mapema tu dakika ya tano la Simon Msuva kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo Mzambia, Obrey Chirwa kuangushwa kwenye boksi na Lufunga.
    Akrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki Mkongo wa Simba, Janvier Besala Bokungu dakika ya 55 baada ya kumuonyesha kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea rafu Chirwa.
    Akrama alikuwa mwiba kwa timu zote mbili siku hiyo kutokana na maamuzi yake ya kufuata sheria 17 za soka bila kusita pale tu lilipotokea kosa, hali ambayo ilisababisha wachezaji wenyewe waamue kuwa na nidhamu uwanjani.
    Na kazi nzuri ya Akrama Oktoba 1 ilikuwa sawa na kusahihisha makosa yake ya Oktoba 3, mwaka 2012 alipochezesha kwa mara ya kwanza mechi ya watani hao wa jadi, ikiwa ya Ligi Kuu pia timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa. 
    Katika mchezo huo ulioanza Saa 1:02 usiku, Akrama alimtoa kwa kadi nyekundu winga Simon Msuva wa Yanga dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu beki wa Simba, Juma Nyosso.
    Siku hiyo, Simba ndiyo walitangulia kwa bao la kiungo Amri Kiemba dakika ya pili, kabla ya mshambuliaji Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga dakika ya 63 kwa penalti baada ya beki Paul Ngalema kuunawa mpira kwenye boksi.
    Lakini Akrama alilaumiwa kwa kumuonyesha kadi ya njano badala ya nyekundu kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ licha ya kumchezea rafu mbaya beki wa Yanga, Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul.
    Na pia alilaumiwa kuwa kutomchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
    Haikuwa ajabu Oktoba 6 Akrama alipoondolewa kwenye orodha ya wamuzi wa kuchezeaha Ligi Kuu baada ya kuvurunda mechi hiyo namba 80, huku aliyekuwa mshika kibendera namba mbili, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam akipewa onyo.
    Lakini bado kazi nzuri ya Akrama Februari 25 haiwezi kunibadilisha msimamo wangu wa muda mrefu wa kutaka mechi za watani hawa wa jadi zichezeshwe na marefa wa nje – ila kwa kuwa wenye mamlaka, TFF na Bodi ya Ligi hawajaona umuhimu wa hilo chochote nitakachoandika kitakuwa sawa na kelele za chura, hazitamzuia ng’ombe kunywa maji. 
    Lakini ukweli unabaki pale pale, marefa wetu wamesababisha adha kubwa kwenye mechi za watani, achilia mbali za Oktoba 1, mwaka jana kuna matukio mengine makubwa ya kihistoria yamewahi kutokea na kuhatarisha hata maisha ya viongozi wetu wakubwa wa nchi.
    Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alinusurika katika tukio la hatari Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1.
    Siku hiyo refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuhatarisha amani uwanjani pia kwa madudu yake.
    Mechi hiyo ya fainali ambayo Alhaj Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa alikuwa mgeni rasi – chupuchupu  ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. 
    Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
    Ni marefa wachache sana wamewahi kuziongoza vizuri mechi za Simba na Yanga na zikamalizika bila manung’uniko, akiwemo mwanamama mwenye beji ya FIFA, Donisya Rukyaa wa Kagera anayefuata nyayo za marefa wakongwe kama Nassor Hamdoun wa Kigoma.
    Tathmini mbalimbali za kitaalamu za vyombo vya habari vya kimataifa zimekwishaipitisha mechi ya Simba na Yanga kama moja ya mechi kubwa mno za watani wa jadi Afrika.
    Tatizo kubwa ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
    Rejea hata mchezo wa Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka kufanya kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au kukwepa lawama, matokeo yake akafanya madudu.
    Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Mzambia Davies Robby Mwape kwenye eneo la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya njano.
    Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
    Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Mghana Yaw Berko kufuatia shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
    Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote, lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
    Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza? Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia aangalie kwenye TV kubwa iliyopo uwanjani marudio ya tukio lile na baada ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
    Tujiulize, kusingekuwa na ile TV, Simba wangedhulumiwa bao lao? Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.   
    Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa kuwapa Yanga penalti ya utata dakika ya 89 na ushei, ambayo Sekilojo Chambua aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
    Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona ukweli wa madai ya Kazi.
    Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amekwishawatoka mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
    Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
    Aprili 19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
    Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni hiyo ya mapenzi yao kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
    Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha fainali ya mwisho ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
    Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA, uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAREFA WA LEO NA MAREFA WENGINE WA SIMBA NA YANGA, YETU MACHO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top