Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amewapiku Lionel Messi na Neymar kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa FIFA PICHA ZAIDI GONGA HAPA
MRENO Cristiano Ronaldo amefanikiwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa FIFA baada ya kumshinda hasimu wake mkubwa, Lionel Messi na Neymar katika sherehe zilizofanyika usiku wa jana mjini London.
Nyota huyo wa Real Madrid amenyakua tuzo hiyo mbele ya wapinzani wake wakuu wa Barcelona na Paris Saint-Germain baada ya ushindi wake wa mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
Ronaldo amefunga mabao 44 katika klabu yake hadi sasa mwaka 2017 na alifunga mawili katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwezi Juni, Real ikitetea taji hilo na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo la Ulaya kwa mara ya 12.
"Nawashukuru sana watu mlionipigia kura mimi,"alisema Ronaldo baada ya kukabidhiwa tuzo yake. "(Ningependa) kutambua uwepo wa Leo (Messi) na Neymar hapa. Mashabiki wa Real Madrid, wachezaji wenzangu, kocha, rais, wote walionisapoti kwa mwaka wotw huu, hivyo ninachoweza kusema ni ninawashukuru wao.
"Tupo England kwa mara ya kwanza na ninashinda tuzo hii mfululizo, hivyo nina furaha kweli, ni wakati mzuri kwangu. FIFA imewapa fursa mashabiki, Nafahamu nina mashabiki dunia nzima (hivyo) asante kwa sapoti, ninakubali hii... nina furaha sana,".
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alikabidhiwa tuzo hiyo na Diego Maradona katika sherehe zilizofanyika kwenye ukumbi wa Palladium Jijini London.
Hizi ni tuzo za pili tangu tuzo hii ya FIFA itenganishwe na Ballon d'Or.
Messi amefunga mabao 50 kwa Barca na Argentina wakati Neymar, ambaye ni mchezaji ghali duniani kwa sasa baada ya kuondoka Barcelona kuingia PSG kwa Pauni Milioni 198 msimu huu, amefunga mabao 25 kwa klabu na nchi yake.
Kwa mafanikio yake ya msimu uliopita, Ronaldo alipewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo.
Aliwasili London Jumatatu pamoja na nyota wengine wa soka wakiwemo beki wa kulia wa PSG, Dani Alves, magwiji Maradona, na Patrick Kluivert.
Mapema katika usiku huo, Olivier Giroud alitwaa tuzo ya Puskas inayotokana na bao bora alilofunga kwa staili ya Nge katika mechi baina ya Arsenal na Crystal Palace, wakati Zinedine Zidane ameshinda tuzo ya Kocha Bora wa Kiume wa Mwaka.
Ronaldo, Neymar na Messi pia waliingizwa kwenye kikosi cha wachezanji 11 Bora, maarufu kama FIFPro World XI sambamba na kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon, Alves na Sergio Ramos.
Toni Kroos na Luka Modric walikuwa ni kati ya wachezaji watano wa Madrid kwenye kikosi hicho, wengine wawili kutoka Barcelona na bahati mbaya hakuna mchezaji hata mmoja kutoka Ligi Kuu ya England.
Buffon pia alishinda tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka baada ya kuiwezesha Juventus kutwaa taji la sita mfululizo la Serie A na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa, wakati Lieke Martens wa Uholanzi ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike wa Mwaka wa FIFA.
Tuzo nyingine zimekwenda kwa Francis Kone (Mchezo wa Kiungwana), Celtic (mashabiki) na Sarina Wiegman (Kocha wa Kike).
0 comments:
Post a Comment