WABRAZIL Neymar na Philippe Coutinho pamoja na Mfaransa N'Golo Kante ni miongoni mwa nyota 10 wa mwanzo katika orodha ya wachezaji 30 waliongizwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, Ballon d'Or mwaka 2017.
Waandaaji wa Ballon d'Or nchini Ufaransa wametoa majina 10 ya mwanzo ya orodha hiyo, wakiwemo Neymar anayecheza Ligue 1 na nyota wa Ligi Kuu ya England Kante na Coutinho.
Neymar aliyehamia Paris Saint-Germain kutoka Barcelona kwa dau la Pauni Milioni 198 msimu huu anatarajiwa kufanya vizuri safari hii baada ya mwaka jana kushika nafasi ya tano.
Neymar ametajwa kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu PICHA ZAIDI GONGA HAPA
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameanza vizuri maisha Parc des Princes akifunga mabao nane katika mechi nane za mwanzo za mashindano yote.
Kante alikuwa nyota wa Ligi Kuu ya England kutajwa kufuatia mafanikio yake ya msimu wa 2016-17 akitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa, PFA baada ya kuiwezaesha Chelsea kushinda taji.
Ameungana na kiungo Kibrazil, Coutinho, ambaye kazi yake nzuri msimu uliopita akiwa na Liverpool iliwavutia hadi Barcelona wakataka kutoa Pauni Milioni 138 kumnunua msimu huu.
Sergio Ramos, Luka Modric na Marcelo wameorodheshwa pia baada ya kuisaidia Real Madrid kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa na La Liga msimu wa 2016-17.
Mshambuliaji wa Barcelona, Luis Suarez, aliyekuwa wa nne katika tuzo zilizopita mwaka 2016, pia yumo wakati kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak ametajwa katika orodha ya wachezaji 30 kwa mara ya kwanza.
Na kwenye Serie A, Paulo Dybala na Dries Mertens pia wameingia. Dybala alikuwa na msimu mzuri uliopita akiisaidia Juventus kutwaa taji la Serie A, wakati Mertens amefunga mabao 34 akiwa na jezi namba 9 ya Napoli.
Cristiano Ronaldo anabaki kuwa mchezaji anayepewa nafasi kubwa ya kushinda tena tuzo hiyo baada ya mafanikio yake ya mwaka.
Alishinda tuzo hiyo mwaka jana akiwaangusha Muargentina Lionel Messi na Mfaransa, Antoine Griezmann na anatarajiwa kuwamo katika orodha ya pili ya majina yatakayotolewa leo.
Ikiwa Ronaldo atashinda Ballon d'Or na mwaka huu atafikia rekodi ya Messi kutwaa tuzo hiyo mara tano.
Wapinzani hao wakubwa wawili, wamepokezana tuzo hiyo peke yao kwa miaka tisa iliyopita tangu Ronaldo aitwae kwa mara ya kwanza mwaka 2008 kama mchezaji wa Manchester United.
0 comments:
Post a Comment