BAO la kipindi cha kwanza la kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim limetosha kuipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda, Rayon Sport jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Mbele ya Mawaziri wawili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Januari Makamba – Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mo Ibrahim alimtungua kwa shuti kali kipa wa Rayon, Mutuyimana Evariste dakika ya 16 baada ya pasi nzuri ya mshambuliaji Mganda Emmanuel Arnold Okwi.
Rayon walicheza vizuri kuanzia kwenye eneo lao hadi katikati ya uwanja tu, lakini mbele hawakuwa na makali ya kuisumbua ngome ya Simba, iliyoongozwea na Nahodha wake, Mzimbabwe Method Mwanjali.
Mohammed 'Mo' Ibrahim akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao pekee leo Uwanja wa Taifa
Wachezaji wapya, Aishi Manula, Erasto Nyoni, John Bocco waliosajiliwa kutoka Azam FC wote, Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC na Salim Mbonde kutoka Mtibwa Sugar wote walianza na kucheza vizuri kwenye timu mpya, Simba.
Kiungo mpya mtaalamu wa kuchezea mpira, Haruna Hakizimana Fadhili Niyonzima aliingia kipindi cha pili na kwenda kuwapa burudani wapenzi wa Simba kwa soka maridadi, lakini bahati mbaya washambuliaji wa timu hiyo walishindwa kutumia nafasi za kufunga alizowatengenzea kuiongezea mabao timu hiyo.
Mshambuliaji mpya, kutoka Ghana, Nicholas Agyei naye aliingia kipindi cha pili na kwenda kucheza vizuri, lakini akashindwa kufunga akiwa mmoja wa waliopoteza nafasi nzuri zilizotengezwa na Niyonzima baada ya kushindwa kumaliza krosi dakika ya 76 kutoka upande wa kushoto.
Pamoja na ushindi huo, kocha Omog bado ana kazi ya kwenda kuwaunganisha wachezaji wake, wacheze kitimu, tofauti na ilivyoonekana leo kucheza ‘kibinafsi’ zaidi kwa wachezaji nyota hususan wapya kutaka kuonyesha uwezo wao zaidi.
Mchezo huo ulitanguliwa na zoezi la kutambulisha wachezaji wa kikosi cha msimu huu cha Simba mmoja baada ya mwingine pamoja na benchi lake Ufundi, lilio chini ya Mcameroon, Joseph Marius Omog, anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja.
Mapema mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye inaaminika ametoa fedha nyingi kusajili wachezaji wapya nyota, akiwemo kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Aishi Salum Manula alizindua Apps ya klabu hiyo maalum kwa habari za timu.
Baada ya mchezo huo, Simba inarejea kambini kwa maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Yanga Agosti 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa pia – kuashiria kupenuliwa kwa pazia la msimu huu wa Ligi Kuu.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Jamal Mwambeleko/Ally Shomary dk46, Method Mwanjali, Salim Mbonde/Bukaba Paulo dk84, James Kotei/Jonas Mkude dk46, Shiza Kichuya/Mwinyi Kazimoto dk71, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk71, John Bocco/Laudit Mavugo dk84, Emmanuel Okwi/Haruna Niyonzima dk46 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Nicholas Gyan dk46.
Rayon Sport; Mutuyimana Evariste, Jean D’Amour Nzayisenga, Gabriel Mugabo, Ally Niyonzima, Idrissa Nzengiyumba/Manishimwe Djapoel dk34, Nova Bayama, Pierre Kwizera, Alhassane Tamboura/Usengimana dk55, Tidiane Kone na Gilbert Mugisha/Habimana dk24.
0 comments:
Post a Comment