// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); SIMBA WAINYAMAZISHA YANGA NA KUBEBA NGAO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE SIMBA WAINYAMAZISHA YANGA NA KUBEBA NGAO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, August 23, 2017

    SIMBA WAINYAMAZISHA YANGA NA KUBEBA NGAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imebeba Ngao ya Jamii baada ya ushindi wa penalti 5-4 kufuatia sare ya bila kufungana na mahasimu wa jadi, Yanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula aliokoa penalti ya kwanza ya Yanga iliyopigwa na beki Kevin Yondan, wakati kiungo Mahadhi akapiga juu kabisa penalti yake. Lakini penalti za Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi, Wazimbabwe Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na mzawa Ibrahim Hajib zilimpita Manula kama amesimama.
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akimkabidhi Ngao ya Jamii Nahodha wa Simba, Method Mwanjali
    Winga wa Yanga, Emmanuel Martin akiutelezea mpira miguuni mwa kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima
    Kipa wa Yanga, Youthe Rostand akidaka mpira dhidi ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, huku beki wake, Gardiel Michael akiwa tayari kusaidia  
    Papy Kabamba Tshishimbi wa Yanga akimuacha chini Shiza Kichuya wa Simba
    Kipa wa Simba, Aishi Manula akiokoa dhidi ya mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma

    Kipa Mcameroon wa Yanga, Youthe Rostand aliokoa penalti ya beki wa kushoto na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini akashindwa kuokoa za beki Mzimbabwe, Method Mwanjali, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi, kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, na wazawa Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim ‘Mo’.
    Kwa Simba hiyo inakuwa mara ya tatu kutwaa Ngao ya Jamii tangu ilipoanzishwa mwaka 2001, baada ya kuibeba pia katika miaka ya 2011 ikiifunga Yanga pia 2-0 na 2012 ikiifunga Azam FC 3-2.
    Katika mchezo wa leo, uliochezeshwa na marefa wa Dar es Salaam Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Ferdinand Chacha wa Mwanza, timu zilishambuliana kwa zamu ndani ya dakika 90 za kawaida.
    Lakini sifa ziende kwa safu za ulinzi za timu zote, Yanga ikiongozwa na Yondan na Simba ikiongozwa na Mwanjali pamoja na makipa wao, Manula na Rostand.
    Safu ya ulinzi ya Yanga leo ilikuwa ina uhai zaidi kutokana na uhodari na ufundi wa kiungo mpya wa ulinzi, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi aliyesajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.
    Kiungo aliyetoka Yanga kwenda Simba, Haruna Niyonzima alicheza vizuri na kutengeneza nafasi ambazo hata hivyo hazikutumiwa vizuri. Hajib pia aliyetoka Simba kuhamia Yanga, naye alicheza vizuri lakini akapoteza nafasin nzuri za kufunga.  
    Donald Ngoma aliisumbusa ngome ya Simba, lakini akapoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kama ilivyokuwa kwa Okwi, naye alipoteza nafasi moja nzuri. Winga Emmanuel Martin alikaribia kuifungia Yanga kipindi cha pili baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kuingia na mpira kwenye boksi, kabla ya kupigiwa filimbi ya kuotea na refa Sasii. Beki mpya wa Yanga, Gardiel Michael leo alimdhibiti vizuri Okwi na Juma Abdul akamficha Kichuya.
    Baada ya mchezo huo, Simba walikabidhiwa Ngao na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku Medali wakivishwa na Makamu wa Rais, Michael Wambura. 
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk89, Salim Mbonde, Method Mwanjale, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk80, Laudit Mavugo/Juma Luizio dk73, Emanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
    Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy dk88, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk75, Thabani Kamusoko, Ibrahim Hajib, Donald Ngoma na Emmanuel Martin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAINYAMAZISHA YANGA NA KUBEBA NGAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top