MRENO Cristiano Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya mara tatu, baada ya leo pia kushinda tuzo hiyo msimu wa 2016-2017.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, amempiku hasimu wake mkubwa, nyota wa Barcelona, Lionel Messi na kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon kutwaa tuzo hiyo baada ya kuiwezesha Real Madrid kutwaa mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Katika kura za makocha 80 wa timu zilizocheza michuano ya Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Ulaya msimu uliopita pamoja na Waandishi wa Habari 55 wa Ulaya wakiwakilisha vyama na mashirikisho ya soka wanachama wa UEFA, Ronaldo amepata pointi 482, akifuatiwa na Messi pointi 141 na Buffon pointi 109.
"Nina furaha mno kuwa hapa na heshima kushinda taji hili tena," amesem Ronaldo. "Shukrani kwa wachezaji wenzangu na pongezi kwao pia. Nimebarikiwa mno – shukrani pia kwa mashabiki wa Real Madrid, na kila mmoja aliyenisaidia kushinda hii,".
Ronaldo alimaliza msimu na mabao 42 katika mechi 46, ambao ulikuwa msimu mbaya zaidi kwake tangu ahamie Bernabeu akitokea Manchester United mwaka 2009.
Pamoja na hayo, mabao 12 — yakiwemo mawili aliyofunga katika fainali — na pasi nne za mabao katika mechi 13 za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilikihakikishia kikosi cha Mfaransa, Zinedine Zidane kuwa timu ya kwanza kutetea taji hilo katika mfumo wa sasa.
Haikuwa ajabu Ronaldo pia aliposhinda tuzo ya Mshambuliaji Bora wa Mwaka wa UEFA licha ya ukweli kwamba Messi, aliyefunga mabao 54 katika mechi 52 alimbwaga mpinzani wake huyo mkubwa katika vita ya Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya.
Haikuwa ajabu Ronaldo pia aliposhinda tuzo ya Mshambuliaji Bora wa Mwaka wa UEFA licha ya ukweli kwamba Messi, aliyefunga mabao 54 katika mechi 52 alimbwaga mpinzani wake huyo mkubwa katika vita ya Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya.
Wachezaji wenzake wa Real Madrid, Sergio Ramos na Luka Modric waliungana naye jukwaani kuchukua tuzo za Beki Bora na Kiungo Bora wa Mwaka wa Ulaya.
Buffon akatwaa tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka wakati kiungo Mholanzi wa Barcelona, Lieke Martens ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike wa UEFA baada ya mafanikio yake ya hivi karibuni katika Euro 2017.
Martens aliyewasaidia wenyeji Uholanzi kung'ara katika mashindano hayo, amempiku mshambuliaji wa Denmark, Pernille Harder na kiungo wa Ujerumani, Dzsenifer Marozsan kutwaa tuzo hiyo.
0 comments:
Post a Comment