MSHAMBULIAJI Mbrazil, Neymar Junior leo ametambulishwa rasmi katika klabu yake mpya, Paris Saint-Germain kufuatia kukamilisha uhamisho wa rekodi ya dunia wa Pauni Milioni 198 na kusema haoni baya alilowafanyia Barcelona.
Baada ya kukamilisha uhamisho huo uliogharimu Pauni Milioni 100 zaidi tofauti na ilivyotarajiwa, Neymar aliyesaini mkataba wa miaka mitano PSG kwa mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki, akasema ameondoka Barcelona kwenda kwa vigogo wa Ufaransa kufuata changamoto mpya.
Neymar amesema hana uhakika wa muda mrefu wa mustakabali wake, lakini ameshawishiwa na wachezaji wenzake wa Kibrazil waliopo PSG. Pia amesema hajahamia Paris ili awe nyota mkubwa wa klabu, ingawa hajatoa sababu haswa ya kumfanya aondoke Barcelona.
Neymar akiwa ameshika jezi namba 10 wakati wa kutambulishwa Paris Saint-Germain PICHA ZAIDI GONGA HAPA
Katika mkutano na Waandishi wa Habari leo, Neymar amesema: “Klabu ina malengo sawia na ya kwangu, nataka changamoto kubwa. Moyo wangu umefanya maamuzi haya, na ndiyo maana nipo mbele yenu leo kuisaidia timu hii,”.
Neymar akasema ameumizwa na kashfa alizotupiwa na baadhi ya mashabiki wa Barca baada ya kuamua kuondoka, wakati anaiheshimu klabu hiyo ya Katalunya na alikuwa ana haki ya kufuata changamoto mpya.
“Siku mbili zilizopita nilimuarifu kocha, alikuwa wa kwanza kujua, ninaiheshimu klabu na kocha,” amesema. “Nina furaha na uamuzi wangu, ninavutiwa,”. “Sijafanya kitu kibaya, sijawakosea heshima mashabiki, nafikiri kila mchezaji angeruhusiwa kubaki au kuondoka klabuni. Wakati mchezaji anafikiri ni sahihi kuondoka, awe tayari kuondoka,”.
Kuondoka kwa Neymar ni pigo Barcelona, kwani safu yao kali ya ushambuliaji iliyokuwa inaundwa na mapacha watatu, pamoja na Lionel Messi na Luis Suarez ikijulikana kama MSN imebomoka.
Na sasa Barca inahusishwa mno na mpango wa kumchukua mshambuliaji mwingine Mbrazil, Philippe Coutinho kutoka Liverpool huo ukiwa mpango wa kocha mpya, Ernesto Valverde kuziba pengo hilo Nou Camp.
0 comments:
Post a Comment