KLABU ya Barcelona imetangaza kukamilisha usajili wa mshambuliaji chipukizi, Ousmane Dembele kutoka Borussia Dortmund kwa dau la Pauni Milioni 96 ambalo linaweza kuongezeka.
Klabu hiyo ya Katalunya imethibitisha habari hizo katika ukurasa wake wa Twitter ikiweka na picha ya Dembele akiwa na jezi ya Barca na katika taarifa nyingine kwenye tovuti yao wamemuita 'mmoja wa wachezaji bora barani'.
Anawasili kuziba pengo lililoachwa na Neymar, aliyehamia PSG mapema mwezi huu kwa dau la rekodi ya dunia, Pauni Milioni 198 na Dembele atakuwa anavaa jezi namba 11 iliyoachwa wazi na Mbrazil huyo aliyeondoka.
Barcelona imetangaza kumsajili Ousmane Dembele kutoka Borussia Dortmund PICHA ZAIDI GONGA HAPA
Dau la Pauni Milioni 96 linamaanisha Dembele atakuwa mchezaji wa pili ghali kihistoria baada ya Neymar na klabu itakayotaka kumnunua mchezaji huyo italazimika kuipa Barca Pauni 368.
Barcelona imesema Dembele atawasili Hispania Jumapili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo Jumatatu kabla ya kutambulishwa mapema wiki ijayo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 aliibukia Rennes ya Ufaransa, kabla ya kujiunga na timu ya Bundesliga msimu uliopita.
Dembele amefunga mabao 10 katika mechi 49, na anashika nafasi ya tatu Ulaya kwa kutengeneza nafasi za kufunga, akiwa ameseti mabao 20 katika mashindano yote.
Haijulikani kama baada ya Barcelona kumpata Dembele itaendelea na mpango wa kumsajili kiungo Mbrazil wa Liverpool, Philippe Coutinho baada ya ofa zake nne kukataliwa Anfield au la.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa sasa anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na kuumwa kwake kumekuza tetesi za kuondoka ingawa ameitwa hivyo hivuo katika timu yake ya taifa, Brazil kwa ajili ya mechi zijazo.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema leo kuhusu Coutinho kwamba: "Kwa sasa yupo kwenye orodha yetu ya majeruhi, hivyo ndivyo ilivyo na haijabadilika. Sijui. Sijawasiliana na FA ya Brazil kwa sasa, lakini sheria ni kama wanataka kumuona na kumuangalia anapaswa kwenda huko,".
0 comments:
Post a Comment