RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez ameibuka na kuanza kumtetea Cristiano Ronaldo juu ya kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili, mara tu baada ya kutoka kwa habari za mchezaji huyo kutakiwa na timu yake ya zamani, Manchester United.
Ronaldo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka Bernabeu - huku uwezekano ukiwa ni kurejea kwa Mashetani Wekundu - baada ya kupoteza furaha kutokana na kutopewa sapoti na Madrid juu ya kesi yake kukwepa kodi.
Nahodha huyo wa Ureno anatuhumiwa kuuza haki za picha zake kwa kampuni moja Uingereza na kukwepa kulipa kodi ya Pauni Milioni 13 Hispania. Perez amesema anamfahamu Ronaldo ni mstaarabu, ambaye hawezi kufanya hivyo.
Amesema wamejiridhisha kwamba wakati wote Cristiano amekuwa akifanya mambo mema, kwa sababu namna alivyo.
"Wote tunatakiwa kutimiza wajibu wetu wa kulipa kodi zetu,' amesema Perez na kuongeza kwamba Ronaldo amekuwa akitumia kampuni ile ile aliyokuwa akiitumia England na hakuwa na tatizo huko. Amesema pia mchezaji huyo hakujaribu kuficha chochote.
Alipoulizwa kama zilikuwa mbinu za Ronaldo kutaka alipiwe faini na klabu ambayo inaweza kufika Euro Milioni 40, Perez akasema: "Swali halina maana kwa sababu hayuko hivyo, kama hayuko sawa, si kwa sababu hiyo. Sijazungumza naye tangu Cardif (Real ilipoifunga Juventus 4-1 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya). Amekuwa na mawasiliano nasi, hivyo ni mchezaji wa Madrid,".
Pamoja na hayo, Perez amesema hajazungumza na klabu yoyote juu ya uhamisho wa mchezaji yeyote hadi sasa, si Cristiano Ronaldo, ama Alvaro Morata, au James Rodriguez.
0 comments:
Post a Comment