KLABU ya Borussia Dortmund imemfukuza kocha wake, Thomas Tuchel.
Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 43, aliyerithi mikoba ya Jurgen Klopp Uwanja wa Signal Iduna Park, anafukuzwa akitoka kuiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lakini taarifa za kutofautiana kwake na bodi ya klabu ndiyo inamfikisha kwenye kufukuzwa.
Taarifa ya Dortmund imesema: Mabingwa mara nane wa Ujerumani, Borussia Dortmund awametengana na kocha Thomas Tuchel. Haya ni matokeo ya mazungumzo baina ya Hans-Joachim Watzke (Mtendaji Mkuu), Michael Zorc (Mkurugenzi wa Michezo), Thomas Tuchel na Mshauri wake, Olaf Meinking yaliyofanyika Jumanne,".
Thomas Tuchel amefukuzwa ukocha wa Borussia Dortmund baada ya kutofautiana na uongozi PICHA ZAIDI GONGA HAPA
Dortmund imemshukuru Thomas Tuchel na wasaidizi wake kwa mafanikio waliyoleta BVB na kuwatakia kila heri baada ya kuondoka.
Gazeti la Bild limeandika kwamba sakata la Tuchel kuondolewa linaweza kuigharimu Dortmund kiasi cha Pauni Milioni 2.5.
Baada ya kuchukua nafasi ya kazi katika klabu hiyo ya Ligi Kuu Ujerumani Julai mwaka 2015, Tuchel akafanikiwa kuwa mmoja wa makocha bora katika historia ya Dortmund akipata wastani wa pointi zaidi ya mbili kwa kila mechi ya Bundesliga.
Ameshinda mechi 69 kati ya 107 akiwa kazini, akimaliza nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich katika msimu wake wa kwanza na ya tatu msimu huu.
Jumamosi aliiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt, ingawa tayari kulikuwa kuna matatizo ya ndani kwa ndani baina yake na uongozi.
Hakufurahia kuuzwa kwa wachezaji kama Henrikh Mkhitaryan, Ilkay Gundogan na Mats Hummels msimu uliopita na tangu hapo uhusiano wake na Hans-Joachim Watzke ukaharibika kabisa.
Tuchel inadaiwa alikorofishana pia na Msaka vipaji mkuu, Sven Mislintat na kufanya uwezekano wake wa kubaki uzidi kuwa mdogo.
Dortmund sasa inaingia sokoni kutafuta kocha mwingine atakayemrithi Tuchel, huku Lucien Favre akipwea nafasi kubwa ya kuchukua kazi hiyo.
0 comments:
Post a Comment