// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HAKUNA KUNDI LAINI KWA TAIFA STARS HII MBOVU MBOVU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HAKUNA KUNDI LAINI KWA TAIFA STARS HII MBOVU MBOVU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, January 22, 2017

    HAKUNA KUNDI LAINI KWA TAIFA STARS HII MBOVU MBOVU

    MWEZI huu CAF, Shirikisho la Soka Afrika limetoa ratiba ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon na Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
    Droo hiyo iliyopangwa mjini Libvreville, Gabon siku mbili kabla ya kuwanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya (AFCON) mwaka huu nchini humo inamaanisha safari hii Taifa Stars haitaanzia kwenye mchujo.
    Furaha ya kwanza kwa Watanzania ni kwenda moja kwa moja kwenye kundi kuzichanga hesabu za kuvuna pointi nyumbani na ugenini ili kufuzu AFCON 2019.
    Lakini sherehe ya pili inayoibuka ni imani kwamba wamepangwa katika kundi rahisi, yaani wanawachukulia poa wapinzani wao Uganda, Cape Verde na Lesotho, wakiamini wapo ndani ya uwezo wao.
    Majirani Kenya pia wataanzia hatua ya makundi, wamepangwa Kundi F pamoja na Ghana, Ethiopia na Serra Leone, wakati Rwanda ipo Kundi H pamoja na Ivory Coast, Guinea na Afrika ya Kati (CAR).
    Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora. 
    Michuano hiyo itaanzia kwa hatua ya mchujo, Raundi ya Awali itakayohusisha timu za Comoros, Djibouti, Madagascar, Mauritius, Sao Tome E Principe na Sudan Kusini.
    Timu zitakazofuzu hapo zitaingia moja kwa moja kwenye makundi A, B na C kukamilisha idadi ya timu nne nne. Kundi Ab lina timu za Senegal, Equatorial Guinea na Sudan, B kuna wenyeji Cameroon, Morocco na Malawi na C kuna Mali, Gabon n Burundi.
    Makundi mengine ni; D: Algeria, Togo, Benin na Gambia, E: Nigeria, Afrika Kusini, Libya na Shelisheli, G: DRC, Kongo, Zimbabwe na Liberia, I: Burkina Faso, Angola, Botswana na Mauritania, J: Tunisia, Misri, Niger na Swaziland, K: Zambia, Msumbiji, Guinea-Bissau na Namibia.
    Cameroon ikiongoza Kundi, mshindi wa pili atafuzu moja kwa moja na kama itashika nafasi ya tatu au ya nne, mshindi wa kwanza atafuzu moja kwa moja na mshindi wa pili atawania nafasi tatu za ziada za kufuzu kama mmoja wa washindi wa pili bora. 
    Hatua ya mchujo itachezwa kati ya Machi 20 na 28 wakati mechi za kwanza za makundi zitaanza Juni 5 na 13, za pili Machi 19 na 27 2018, za tatu Septemba 3 na 11, 2018 za nne Oktoba 8 na 16, 2018 na za tano Novemba 5 na 13, 2018.
    Tangu baada ya kutolewa kwa ratiba hii, kumekuwa na maoni na mitazamo tofauti, wengine wakisema ni rahisi, wengine si rahisi kufuzu AFCON kutoka Kundi L.
    Na wengi wenye kutoa maoni na mitazamo yao wamekuwa wakifafanua pia kwa nini ni rahisi, si rahisi kwenda Cameroon 2019 dhidi ya na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
    Ukipitia maoni hayo na kufanya mjumuisho utagundua ni kweli Tanzania imepangwa katika kundi nafuu kidogo, tofauti na kama ingepangwa na timu za Kaskazini au Magharibi mwa Afrika, ambazo nyingi sipo mbali kisoka.
    Pamoja na imani hiyo kwamba ipo kundi nafuu, Stars inaweza kujikuta inapunguza idadi ya mabao kutoka 7-0 walizopigwa na Algeria mwaka jana hadi angalau 3-0.
    Mara ya mwisho kukutana na Uganda Julai 4, mwaka 2015 Stars walitoa sare ya 1-1 Kampala, Uganda wakitoka kufungwa 3-0 na The Cranes Juni 20, mwaka 2015 katika mchezo wa kufuzu CHAN kisiwani Zanzibar.
    Lesotho mara ya mwisho waliifunga Taifa Stars 1-0 Mei 22 katika mchezo wa kirafiki, wakati Cape Verde ni timu pekee kufungwa, 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mara ya mwisho walipokutana Oktoba 11, mwaka 2008 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2010 Afrika Kusini.
    Huo ulikuwa mchezo wa marudiano baada ya wao kutufunga mchezo wa kwanza Juni 7, mwaka 2008 kwa visiwa vya Cape Verde.
    Lakini katika Kundi L Cape Verde inajitokeza timu ngumu zaidi na inayopewa nafasi kubwa ya kufuzu, kwani kutoka 2008 walipokutana nayo mara ya mwisho imekwishashiriki AFCON mbili, 2013 Afrika Kusini na 2015 Equatorial Guinea.
    Mwaka 2013 ilishika nafasi ya pili Kundi A nyuma ya wenyeji Afrika Kusini, ikizipiku Morocco na Angola kufuzu Robo Fainali, ambako ilikwenda kutolewa na Ghana. 
    Ilifungwa 2-0 na Ghana Februari 2, 2013 mabao ya Abubakar Wakaso dakika ya 54 kwa penalti na 90 na ushei.
    Na mwaka 2015 ilishika nafasi ya tatu Kundi B, ikizidiwa kete na Tunisia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika kundi lililokuwa na Zambia pia iliyoshika mkia.
    Hii inatosha kutujuza Cape Verde iliyopangwa kundi moja na Stars ni timu ya aina gani. Stars ilishinda 3-1 katika mwaka ambao soka ya Tanzania ilikuwa juu mno baada ya jitihada za kocha Mbrazil, Marcio Maximo. 
    Stars haiwawezi Ugnda kwa sasa, Lesotho labda wawataifungia kwao tu Dar es Salam na Cape Verde ya sasa ni maji marefu – hizo ndizo timu tulizonazo kundi moja.
    Ni Taifa Stars gani inayokwenda kukutana na timu hizo kuwania tiketi ya Cameroon 2019 kama si hii iliyocheza mechi nne buila kushinda, ikifungwa tatu mfululizo, moja nyumbani2-0 na Misri.
    Kwa Taifa Stars hii iliyocheza ovyo kabisa wakati inafungwa 3-0 na Zimbabwe katika mchezo wake wa mwisho wa kujipima Novemba 13, mwaka 2016 ndiyo tunapata jeuri ya kusema; “Tumepangwa kundi mchekea”?.
    Tuache kujidanganya. Tutacheza mechi ya kwanza ya kundi kati ya Juni 5 na 13 maana yake tuna kipindi kirefu kutokea hapa.
    Lazima tuwe na maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kwa mechi za mchujo, kuhakikisha kwamba mechi zote za nyumbani tunashinda. Na maandalizi si Kamati za ujanja ujanja watu kujitafunia fedha, bali ni Maandalizi ya kuandaa timu tu, si kitu kingine.
    Wakati huo huo hatuelewi kuhusu mustakabali wa benchi la Ufundi baada ya kuondolewa kwa Charles Boniface Mkwasa, je kocha wa muda Salum Mayanga atakuwa wa kudumu, au?
    TFF, Shirikishio laSoka Tanzania wana majhibu juu ya hilo, kwani huwezi kuzungumzia maandalizi bila benchi la Ufundi. Leo nilikuwa nataka tuondoe dhana kwamba eti tupo kundi mchekea.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAKUNA KUNDI LAINI KWA TAIFA STARS HII MBOVU MBOVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top