// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); PLUIJM: WACHEZAJI WA TANZANIA WANATAKIWA KUBADILIKA WACHEZE ULAYA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE PLUIJM: WACHEZAJI WA TANZANIA WANATAKIWA KUBADILIKA WACHEZE ULAYA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Friday, December 09, 2016

    PLUIJM: WACHEZAJI WA TANZANIA WANATAKIWA KUBADILIKA WACHEZE ULAYA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAADA ya kuiongoza Yanga SC kwa mafanikio tangu mwaka 2014, kocha Mholanzi Johannes ‘Hans’ Franciscus van der Pluijm mwezi uliopita alipandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, nafasi yake akimuachia Mzambia, George Lwandamina.
    Kwa misimu miwili na nusu ya kuwa Yanga, Pluijm anakuwa kocha wa kwanza Yanga baada ya muda mrefu kazi yake kuonekana ndani ya timu na ni kwa sababu hiyo, Bin Zubeiry Sports – Online ikamtafuta kwa mahojiano mafupi. Endelea.

    Hans van der Pluijm mwezi uliopita alipandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi Yanga

    Bin Zubeiry Sports – Online; Baada ya misimu miwili na nusu, umejifunza nini katika soka ya Tanzania
    Pluijm; Kiufundi na maarifa, bado kuna mambo mengi ya kurekebisha. Wachezaji wanatakiwa kubadilika na kuichukulia soka kama kazi ndani na nje ya Uwanja ili wafikie mafanikio makubwa pamoja na kucheza Ulaya. Wanatakiwa kuangalia mbele zaidi, lakini wengi wao wanabadilika hatua kwa hatua. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Zipi changamoto kubwa ulipokuwa kazini? 
    Pluijm; Ubora wa vifaa, vitendea kazi, viwanja vya mazoezi na kuchezea mechi vinahitaji kuboreshwa. Hii inakwamisha kupandisha kiwango cha soka. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Wakati wote imeonekana wachezaji wa kigeni wamekubeba kushinda mataji
    Pluijm; Ndiyo, hiyo inachangiwa na kukosa mfumo mzuri wa soka ya vijana na misingi mizuri, akademi za soka na makocha wazuri. Maana yake wanakosekana wachezaji waliotayarishwa vizuri japokuwa kuna vipaji vingi hapa
    Bin Zubeiry Sports – Online; Umegundua kwa nini hakuna uwekezaji kwenye soka ya vijana hapa?
    Pluijm; Nafikiri ni masuala ya kifedha, ukosefu wa wadhamini na kadhalika. Ila naona kwa sasa Shirikisho la Soka (TFF) inalifanyia kazi hilo, na hii itaisaidia soka ya Tanzania baadaye.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Changamoto zipi unatarajia katika nafasi mpya kama Mkurugenzi wa Ufundi Yanga? 
    Pluijm; Changamoto zipo katika nafasi yoyote kwenye taasisi. Kumtengenezea mazingira mazuri ya kufanya kazi Kocha wetu Mkuu na kushirikiana naye kuiboresha timu pale inapohitajika.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kwa upande wako kama Mkurugenzi wa Ufundi, kuhusu majukumu yako?
    Pluijm; Kuunda mfumo mzuri zaidi wa kisasa na kitaalamu katika taasisi nzima kadiri itakavyowezekana. Kujenga mfumo wetu wenyewe wa soka ya vijana na kuiimarisha timu yetu ya vijana iliyopo, ili tupate wachezaji wa kupandisha kwenda kikosi cha kwanza.    
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ulikuja hapa ukitokea Ghana ambako ulifanya kazi kwa muda mrefu ukitokea kwenu Uholanzi. Je, Ligi Kuu ya Ghana na Tanzania zina tofauti gani?    
    Pluijm; Ligi ya Ghana nayo ina matatizo yake.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kwa mfano
    Pluijm; Sifikirii ni sahihi kuzungumzia matatizo ya Ligi ya Ghana. Lakini kukosekana kwa wadhamini mwaka jana kulisababisha matatizo kwa klabu nyingi.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Nini kikubwa cha kujivunia baada ya miaka takriban miaka miwili na nusu ya kuwa Kocha Mkuu wa Yanga?
    Pluijm; Kushinda mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la FA pamoja na kupewa tuzo ya Kocha Bora wa Ligi ya Tanzania, hayo ni ya kujivunia kwangu. Lakini kikubwa zaidi kwangu ni heshima niliyopewa na mashabiki kwa miaka miwili wameonyesha upendo na heshima kubwa kwangu kwa yale tuliyoyachuma kwenye timu. Najihisi ni mmoja wao. Huu ni uhusiano mzuri na mashabiki wetu babu kubwa, ambao unanifanya nijivunie.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Unazungumziaje mahusiano yako na wachezaji?
    Pluijm; Kwa ujumla sina tatizo na wachezaji, lakini kama ujuavyo, ukiwa kocha wa Yanga, uongozi na mashabiki unakutazama wewe kwa uchezaji wa timu. Haiwezekani kushinda kila wakati, lakini kila mmoja anataka na anatarajia ushindi. Ushindi baada ya ushindi. Hii inamaanisha wachezaji wanapaswa kuzingatia na kujituma katika kazi yao. Nimejaribu kutengeneza mazingira ya kufanya kazi kwa weledi na wakati huo huo unatakiwa kudhibiti nidhamu za wachezaji ndani na nje ya Uwanja. Nimekuwa kocha wa nidhamu na baba kwao. Lakini kama unavyojua, mchezaji asipopata nafasi ya kucheza hafurahii. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Amewahi kutokea mchezaji wa kukulalamikia humpangi? 
    Pluijm; Hapana, nasikia wanalalamika pembeni, lakini mchezaji anapaswa kujiuliza mwenyewe kwanza, kwa nini hachezi. Ni mazoezi ndiyo yanayoamua mchezaji acheze au hapana. Hakuna kocha asiyepanga timu yake bora uwanjani. Naweza kusema kwamba sina tatizo na mchezaji binafsi, lakini ni kiwango cha mchezaji ndicho kinachotazamwa. Nimefafanua hilo mara kadhaa. Lakini nyuma yangu wakati wote kila mtu yupo tayari  kusikiliza malalamiko ya wachezaji ambao hawachezi.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ukweli ukoje?
    Pluijm; Kucheza timu kama Yanga ni kitu tofauti na kucheza timu nyingine. Wachezaji wanapokuja Yanga wanabadilika kwa sababu wanakuwa maarufu, jambo ambalo inabidi lishughulikiwe na kocha na hiki ndicho kitu wasichopenda sana (wachezaji). Ukweli unauma wakati mwingine, lakini kupiga hatua kisoka na kibinadamu ni vizuri kujifunza na kukubali.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Wapo wachezaji wanaokuelewa na kurudi kwenye mstari baada ya kuyumba?
    Pluijm; Ndiyo, wapo nimefanya kazi Afrika tangu mwaka 1996 na ninazungumza ninachokifahamu. “Unaweza kuupata utamu wa chungwa pale unapolikamua sana na kwa maneno mengine, huwezi kupendwa na kila mtu.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ukipata ofa ya kazi sehemu nyingine hapa Tanzania, utakubali?
    Pluijm; Kwa heshima, naomba nisijibu swali hilo. Mungu tu ndiye anayejua nini kinachofuata kwangu.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Unawazungumziaje wachezaji wa Ghana waliomiminika Tanzania siku za karibuni wakijiunga na Azam, Simba na klabu nyingine? 
    Pluijm; Wachezaji kutoka Ghana wanaokuja Tanzania ni wazuri, baadhi yao ninawajua, kama hao wanaotoka Medeama, nimefanya nao kazi. Klabu zilizowasajili zitafurahia huduma zao. Na wachezaji nao watafurahia maisha hapa. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Unaijua vyema Afrika kwa sasa, itachukua muda gani klabu au timu ya taifa hapa Afrika kuchukua Kombe la Dunia?
    Pluijm; Hili swali gumu kujibu, lakini nafikiri bado itachukua miaka mingi. Bado tuko nyuma sana ya Ulaya na Amerika Kusini. Mipango thabiti ya maendeleo, miundombinu madhubuti, vifaa na mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu vinahitajika. Na muhimu zaidi ni, watu sahihi wenye ujuzi na utaalamu wa kuongoza wahusishwe. Ambao wapo kwa manufaa ya soka na si maslahi yao binafasi.  

    Pluijm katika siku ya mwisho ya kufanya kazi kama Kocha Mkuu Yanga 

    WASIFU WA PLUIM
    JINA KAMILI: Johannes Franciscus van der Pluijm
    KUZALIWA: Januari 3, 1949 (Miaka 67)
    ALIPOZALIWA: Nieuwkuijk, Uholanzi
    NAFASI ALIYOCHEZA: Kipa
    KLABU ALIZOCHEZEA:
    Mwaka Timu
    1967–1986 FC Den Bosch (Alidaka mechi 338)
    TIMU ALIZOFUNDISHA:
    1990–1995 FC Den Bosch (Uholanzi)
    1995–1996 Excelsior (Uholanzi)
    2000–2002 Obuasi Goldfields (Ghana)
    2002–2003 Heart of Lions (Ghana)
    2004–2005 Ashanti Gold (Ghana)
    2014: Yanga SC (Tanzania)
    2015: Al Shoalah FC (Saudi ya Arabia)
    Tangu; 2015; Yanga SC (Tanzania)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM: WACHEZAJI WA TANZANIA WANATAKIWA KUBADILIKA WACHEZE ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top