Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Amissi Joselyn Tambwe leo ametokea benchi na kufunga mabao mawili, Yanga SC ikishinda 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Wakicheza kwa mara ya kwanza bila ya kodha wake Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyejiuzulu jana, wachezai wa Yanga walijituma na kuvuna ushindi huo mnono.
Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 24 baada ya kucheza mechi 11 na sasa inazidiwa pointi tano tu na mahasimu wao, Simba SC waliopo kileleni mwa ligi hiyo.
Mabao mengine ya Yanga jana yalifungwa na Mzambia Obrey Chirwa na mzalendo Simon Msuva moja kila mmoja.
Chirwa ndiye aliyekata utepe wa mabao ya Yanga dakika ya sita akimalizia pasi ya Msuva, bao ambalo lilidumju hadi mapumziko.
Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akishangilia baada ya kutokea benchi na kufunga mabao mawili, Yanga ikishinda 4-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
Wafungaji wa mabao mengine ya Yanga leo, Obrey Chirwa (kulia) na Simon Msuva (kushoto)
Chirwa kushoto akipiga mpira mbele ya kipa wa JKT
Mshabuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akimruka kipa wa JKT Ruvu
Winga wa Yanga, Simon Msuva akimtoka beki wa JKT Ruvu, Salim Aziz Gilla
Beki wa Yanga, Hassan Kessy akipiga mpira mbele ya mchezaji wa JKT Ruvu
Yanga ingeweza kupata mabao zaidi kama wachezaji wake wangetumia nafasi walizotengeneza. Mzimbabwe Donald Ngoma alimdakisha kipa wa JKT Ruvu, Said Kipa dakika ya 25 baada ya pasi nzuri kutoka ya beki Hassan Kessy kutoka kulia.
JKT Ruvu nao walipoteza nafasi nzuri dakika ya 17 baada ya kiungo wa zamani wa Yanga, Hassan Dilunga kupiga juu akiwa kwenye nafasi nzuri.
Kipindi cha pili, JKT Ruvu walirudi kwa kasi kama ya kutaka kusawazisha na dakika ya 48 mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Atupele Green akapiga nje.
Tambwe akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 64, baada ya kuwatoka mabeki wa Ruvu JKT na kuzamisha mpira nyavuni, bao zuri ambalo lilimuinua jukwaani kocha Pluijm kushangilia.
Msuva akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 83 kwa ustadi mkubwa baada ya kumtoka kwa kasi beki wa pembeni kushoto 2wa JKT Ruvu, Salim Aziz Gilla kufuatia pasi ya Tambwe na kuingia ndani kabla ya kumtungua kipa Kipao.
Tambwe akakamilisha shangwe za mabao za Yanga kwa kufunga bao la nne dakika ya 90, akitumia makosa ya kipa wa Ruvu, Kipa kuzembe a kuokoa mpira aliorudishiwa na beki wake, Michael Aidan hivyo Mrundi huyo akaupitia na kubutua hadi nyavuni.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munish ‘Dida’, Vicent Bossou, Hassan Kessy, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva/Juma Mahadhi dk89, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa, Donald Ngoma/Amissi Tambwe dk57 na Deus Kaseke/Goffrey Mwashiuya dk84.
JKT Ruvu; Said Kipao, Omary Kindamba/Michael Aidan dk60, Salim Gilla, Nurdin Mohammed, Rahim Juma, Ismail Amour/Hamisi Thabir dk89, Kassim Kisengo/Samuel Kamuntu dk46, Naftar Nashon, Atupele Green, Hassan Dilunga na Pera Mavuo.
0 comments:
Post a Comment