HATIMAYE baada ya danadana za muda mrefu, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo amewasili usiku wa Jumatano kujiunga na Simba SC.
Mavugo aliwasili Saa 4:30 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na kupokewa na Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyempeleka hotelini kupumzika.
Asubuhi ya Alhamisi, Mavugo atakuwa na mazungumzo na uongozi wa Simba SC kabla ya kwenda kambini Chuo cha Biblia mjini Morogoro kujiiunga na wenzake.
Laudit Mavugo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam usiku wa Jumatano
Na mshambuliaji huyo wa Vital’O ya kwao, anakuja Tanzania baada ya mpango wa kujiunga na klabu ya Tours ya Ligi Daraja la Pili, Ufaransa maarufu kama Ligue 2 kukwama.
Mavugo alikwenda Ufaransa wakati tayari Simba SC wamesema wamekwishaingia Mkataba na mchezaji huyo kuanza kuwatumikia kuanzia msimu ujao.
Mavugo (kulia) akiwa na Makamu wa Rais wa Simba, Kaburu baada ya kuwasili JNIA |
Hapa ni baada ya Mavugo kuwasili kabla ya kuvalishwa jezi ya Simba
Wakati huo huo: Simba SC imefungwa 1-0 na KMC ya Kinondoni jioni ya Jumatano katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Highlands, Bigwa mkoani Morogoro.
Huo unakuwa mchezo wa kwanza Simba SC kupoteza chini ya kocha mpya, Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya awali kushinda mechi zote tatu, 5-0 dhidi ya Burkina Fasso, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 6-0 dhidi ya Polisi Morogoro.
Katika hatua nyingine, timu ya Interclube ya Angola haitakuja kucheza na Simba katika sherehe za miaka 80 ya klabu hiyo, maarufu kama Simba Day badala yake itakuja AFC Leopards ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment