Kocha wa Geota Gold, Suleiman Matola |
KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itakutana tena kesho (Jumamosi) kuanzia Saa 3:00 asubuhi katika ofisi za TFF zilizopo Karume kujadili matokeo ya utata ya mechi za mwisho Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Na baada ya kikao cha kesho, Kamati hiyo inatarajiwa kutoa maamuzi yake Saa 7:00 mchana.
Katika kikao cha kesho, Kamati inakutana kwa ajili ya kumalizia shauri la upangaji wa matokeo Ligi hiyo StarTimes kwa mechi za Kundi C linalozihusisha timu za Geita Gold ya kocha Suleiman Matola, JKT Kanembwa, JKT Oljoro na Polisi Tabora.
Viongozi watakaohojiwa na Kamati ya Nidhamu ni, Yussuf Kitumbo (Mwenyekiti wa Chama Soka Tabora), Fateh Remtullah (Katibu wa Chama cha Soka Tabaora), viongozi wa benchi la ufundi Polisi Tabora, Mrisho Selemani, Boniface Komba na Bernard Rabiamu.
Kamati pia itawahoji Mwenyekiti wa Chama cha Soka Geita, Salum Kurunge na Mwenyekiti wa Klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita.
Ikumbukwe JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold SC katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Baada ya hapo, TFF ilitangaza kusitisha matokeo hayo na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) iliyokutana Februari 16, mwaka huu kupitia taarifa za mechi hizo mbili ikalipeleka suala hilo Kamati ya Nidhamu kufuatia kutilia mashaka upangaji wa matokeo.
0 comments:
Post a Comment