Rahim 'Zamunda' Kangezi |
BAADA ya timu yake kufanikiwa kurejea katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao, uongozi wa timu ya African Lyon umesema hautasajili wachezaji watakaoachwa na klabu kongwe za Simba na Yanga.
African Lyon na Ruvu Shooting ndiyo timu ambazo zimeshakata tiketi ya kucheza Ligi Kuu huku timu ya tatu kutoka Kundi C bado haijajulikana kufuatia kashfa ya upangaji matokeo iliyojitokeza kwenye kundi hilo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Mmiliki wa klabu hiyo, Rahim Kangezi maarufu kama Zamunda alisema kwamba timu yake itaelekeza nguvu kusajili wachezaji chipukizi ambao kila mmoja analenga kupata mafanikio.
Kangezi alisema kuwa tayari benchi la ufundi la timu hiyo limeshawapandisha baadhi ya nyota waliofanya vizuri na kuisaidia kupanda daraja huku pia wale waliong'ara kwenye vikosi vya timu nyingine za vijana.
"Hatuaangalia wachezaji kutoka Simba wala Yanga, ni wasumbufu na kasi yao katika kusaidia timu si ya kuitegemea, wasihangaike kutufuata watakapoachwa," alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa kabla ya msimu kuanza, timu hiyo itaenda kuweka kambi ya mwezi mmoja nje ya nchi na kucheza mechi za kirafiki za kimataifa ili kujiimarisha na kuwapa uzoefu wachezaji wake.
0 comments:
Post a Comment