Deo Julius atakosekana wiki mbili Mbeya City |
BEKI wa Mbeya City, Deogratius Julius atakuwa nje kwa wiki mbili kufuatia kuumia goti katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wa jiji la Mbeya, Prisons.
Daktari Mkuu wa Mbeya City FC, Dk Joshua Kaseko ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba Deo Julius aliyeumia katika mchezo wa Jumapili uliomalizika kwa sare ya 0-0 baada ya kufanyiwa vipimo imegundulika anahitaji mapumziko ya wiki mbili.
Maana yake mlinzi huyo tegemeo wa Mbeya City inayopambana kuepuka kushuka daraja, ataikosa michezo yote mitatu ndani ya wiki hizi mbili za ratiba ya Ligi Kuu na Kombe la FA kwa maumivu hayo.
"Mimi na timu yangu nzima ya kitengo cha madaktari wa Mbeya City, tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha beki huyo anapona ndani ya muda na kurejea kikosini,"amesema.
Deo ataanza kukosekana kuanzia leo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation dhidi ya Wenda FC, kabla ya kukosa pia mechi za Ligi Kuu dhidi ya Toto Africans mwishoni mwa wiki mjini Mbeya na dhidi ya African Sports mjini Tanga Alhamisi wiki ijayo.
Mbeya City wanashuka kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya leo kumenyana na Wenda FC ya Mbalizi, katika mchezo wa mwisho wa hatua ya 32 Bora Kombe la TFF na mshindi atamenyana na Prisons katika hatua ya 16 Bora.
0 comments:
Post a Comment