Donald Ngoma ameondoka leo asubuhi kwenda Zimbabwe kuhudhuria msiba wa mdogo wake |
MSHAMBULIAJI wa Zimbabwe, Donald Dombo Ngoma hatakuwepo Jumamosi wakati Yanga SC inacheza na Cercle de Joachim ya Mauritius mechi ya marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika..
Ngoma amesafiri leo asubuhi kwenda kwao Zimbabwe kuhudhuria mazishi ya mdogo wake aliyefariki jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema uongozi umelipa uzito suala la mchezaji huyo na kumopa ruhusa.
"Tumeangalia nafasi yetu ya kusonga mbele katika mchezo wa Jumamosi na kuona ni kubwa baada ya ushindi wa awali wa 1-0 ugenini, hivyo tukaona bora tumruhusu Ngoma awahi msiba wa ndugu yake,"amesema Muro.
Yanga SC inahitaji sare yoyote kama si kushinda kujenga heshima ili kusonga mbele, baada ya ushindi wa ugenini wa 1-0 katikati ya mwezi huu.
Pamoja na hayo, Muro ametaja viingilio vya mchezo wa Jumamosi kuwa ni Sh. 30,000 kwa VIP A, Sh. 20,000 kwa VIP B, Sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya Chungwa na Sh. 5000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.
Amesema tiketi zitaanza kuuzwa kesho katika vituo vya Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume), Makao Makuu ya klabu, Jangwani, ukumbi wa Dar Live, Mbagala na Buguruni.
0 comments:
Post a Comment