Petr Cech akishangilia jana baada ya kufikisha mechi 170 za Ligi Kuu ya England bila kufungwa PICHA ZAIDI GONGA HAPA
KIPA wa Arsenal, Peter Cech ameweka rekodi mpya katika Ligi Kuu ya England, baada ya kufikisha jumla ya mechi 170 za kudaka bila kuruhusu nyavu zake kuguswa.
Kipa huyo aliyetua Emirates msimu huu akitokea Chelsea, alifikisha rekodi hiyo jana Arsenal ikishinda 2-0 dhidi ya Bournemouth.
Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 33 hatimaye amevunja rekodi ya kipa wa zamani namba moja wa England, David James - ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya kudaka mechi nyingi bila kufungwa kabla ya kustaafu akiwa na Portsmouth mwaka 2010.
Cech anavunja rekodi hiyo ndani ya jumla ya mechi 352 za Ligi Kuu ya England alizodaka katika klabu za Chelsea na Arsenal.
James, aliyedaka jumla ya mechi 562, aliweza kuzuia nyavu zake kuguswa katika 169 na kushikilia rekodi ya kipa aliyedaka mechi nyingi za Ligi Kuu ya England bila kufungwa kwa muda mrefu.
"Ni mafanikio makubwa binafsi na nimejisikia faraja sana mwishoni mwa mchezo ukitazama katika orodha ya makipa waliodaka mechi nyingi bila kufungwa na unaona orodha ya makipa waliokuwa wanacheza na ambao bado wanacheza katika ligi hii, kisha wazi ni mafanikio makubwa kuongoza katika orodha," amesema.
Kipa huyo wa kimataifa wa Czech, alitua Arsenal baada ya miaka 11 ya kupiga kazi Stamford Bridge.
0 comments:
Post a Comment