// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HATA SEKTA YA MICHEZO INAYO MAJIPU YANAYOHITAJI KUTUMBULIWA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HATA SEKTA YA MICHEZO INAYO MAJIPU YANAYOHITAJI KUTUMBULIWA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, December 07, 2015

    HATA SEKTA YA MICHEZO INAYO MAJIPU YANAYOHITAJI KUTUMBULIWA

    Na Salum Vuai, ZANZIBAR
    IMEKUWA kama kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezinduka kutoka katika usingizi mzito ambao watendaji wasiojali maslahi mapana ya umma bali nafsi zao tu waliutumia kuchota mali walizokuwa wamepewa dhamana kuzisimamia.
    Kasi aliyoanza nayo Rais wa awamu ya tano Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, ambayo kwa kweli imewavutia wengi, ni parapanda linalotoa ishara kwa mafisadi na watendaji wengine waliokosa maadili kukaa chonjo. 
    Ni dhahiri kwamba, Mhe. Rais ameonesha aina ya viongozi tunu katika bara la Afrika ambalo limeshuhudiwa kuugua saratani ya kuanguka kiuchumi sio kwa kuwa halina rasilimali, bali kwa matumizi mabaya yanayoangalia zaidi ustawi wa wachache na sio wananchi wao.
    Kwa hili, napenda nimpongeze Dk. Magufuli na kumuombea kila la kheri katika safari yake ya kujenga Tanzania mpya isiyo na chembe hata moja ya ufisadi na dhuluma dhidi ya umma.
    Kikosi cha Malindi mwaka 1995 ambacho kilifika Nusu Fainali ya Kombe la CAF

    Aidha nichukue fursa hii kumvulia kofia Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuonesha kwamba anaweza kwenda sambamba na kasi hiyo.
    Kwa hivyo, ni matumaini yangu na ninaamini ya Watanzania wote kwamba wananchi wenzetu watakaobahatika kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri litakaoundwa baadae, watawasaidia viongozi wa juu kwa kutenda yale ambayo Watanzania wanayatarajia katika kuwaletea maendeleo.
    Haitakuwa vyema, Mhe. Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu, waachiwe peke yao kufanya kazi ya kusafisha nyumba yetu ili kuwatoa mchwa wanaotafuna boriti na mbao zilizotumika kuijenga, il-hali sote tunaishi na kulala humo.
    Sasa, wakati Mhe. Rais akiendelea kutumbua majipu katika mashirika ya umma na taasisi za serikali, natumai mbele ya safari na baada ya kupata Baraza la Mawaziri, hata taasisi zilizopewa dhamana ya kuendesha na kusimamia michezo nazo zitapitiwa na fagio hilo.
    Imenibidi kusema hivyo kwa sababu sekta ya michezo nayo imejaa majipu yanayopasa kutumbuliwa kama kweli Tanzania inataka kujijengea hadhi kimichezo na kutambulika kimataifa.
    Kama inavyoeleweka, Tanzania ndiyo inayotambulika kimataifa katika michezo mbalimbali, ikiibeba pia Zanzibar kupitia mashirikisho yake ya michezo tofauti.
    Mathalan TFF katika mpira wa miguu, CHANETA (netiboli), RT (riadha), TAVA (mpira wa wavu), TAHA (mpira wa mikono), SOT (Olimpiki Maalum) na mingine mingi.
    Lakini ni jambo la kusikitisha kwamba kwa miaka mingi, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka vyama vya michezo Zanzibar juu ya kutotendewa haki na mashirikisho hayo.
    Vyama hivyo vimekuwa na kilio cha kutokupewa kasma ya vifaa mbalimbali vya michezo vinavyotolewa na mashirikisho ya dunia, safari za kushiriki mikutano ya kimataifa, nafasi za mafunzo, na hata migao ya fedha za  kuendeshea ofisi za vyama hivyo.
    Mara kadhaa, vimewahi kufanyika vikao vya mabaraza ya michezo Tanzania (BMT) na Zanzibar (BTMZ) kwa agizo la mawaziri waliokuwa na dhamana ya michezo, baada ya kuibuka migogoro kati ya ama mabaraza hayo, au vyama vya michezo vya pande zote mbili.
    Soka na netiboli ndiyo michezo iliyokuwa imetawaliwa na mivutano ya siku nyingi hata ikabidi mikono ya wizara iingie kunusuru mpasuko.
    Lakini miezi kadhaa iliyopita, kumeshuhudiwa pia Chama cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA) na Shirikisho la mchezo huo Bara (TBF), nao wakiingia kwenye mgogoro unaofanana na ile ya soka na netiboli.           
    Ukimya huu unaoshuhudiwa sasa hauna maana kwamba mambo yako sawa, la! Ukweli ni kwamba mivutano kati ya vyama vya michezo ni sawa na uji wa uwele ambao kwa kuutazama juujuu ukiwa bakulini mtu hudhani umepoa lakini akiuvamia kuunywa lazima utambabua midomo.
    Mbali na hayo, baadhi ya mashirikisho na vyama vya michezo yamekuwa yakiendeshwa kama mali za watu maalum ambao kila kunapofanyika uchaguzi kunakuwa na mizengwe mingi kuzuia wengine, ama wasigombee au wakigombea wasipite.
    Vyama vingi vya michezo vimekuwa havifuati katiba zao katika kujiendesha na hata viongozi wa vyama hivyo kujenga makundi yanayozorotesha shughuli za michezo nchini.
    Viko pia vyama vilivyodiriki kuweka vifungu kwenye katiba zao vinavyolenga kujijengea uzio na kuwazuia wengine wasiweze kugombea nafasi za uongozi kama kwamba vyama hivyo ni milki yao.
    Aidha, wapo watu wengine wanaong’ang’ania kubaki kwenye madaraka ya vyama vya michezo kama njia ya kuendesha miradi yao, ikiwemo haramu, ya usafirishaji mihadarati kama ilivyowahi kutokea kwa Shirikisho la Ngumi Tanzania.
    Halikadhalika, vipo baadhi ya vyama vya michezo ambavyo muda wa viongozi wao kuwepo madarakani umeshamalizika kwa miezi au hata miaka mingi lakini hakuna dalili ya vyama hivyo kuitisha chaguzi za kutafuta viongozi wapya.
    La kushangaza, vyama hivyo viko kwa sheria ya urajis wa vyama na klabu za michezo, ambayo ina mamlaka ya kuchukua hatua, ama kuvielekeza kuheshimu katiba kwa kuitisha chaguzi, au kuwaondoa viongozi na kuunda kamati za muda kabla ya kufanya chaguzi hizo.
    Viongozi wa michezo kama hawa ni sawa na majipu yanayopaswa kupitiwa na makamuzi ya Mhe. Rais ili kujenga vyama vyenye maadili ya uongozi na vitakavyonufaisha pande zote mbili za Muungano.
    Sote ni mashuhuda wa hali mbaya ya sekta ya michezo nchini.
    Tunayaona majipu haya kwani tunaishi nayo maungoni mwetu. Umefika wakati sasa yatumbuliwe hata kama kutumbuliwa huko kutagharimu maslahi ya wengine, kwani tunachotafuta ni manufaa ya wengi na sio ya wachache.
    (Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa nambari +255 777 865050 na +255 714 425556)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATA SEKTA YA MICHEZO INAYO MAJIPU YANAYOHITAJI KUTUMBULIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top