// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); BAMCHAWI, MANGARA WANGEKUWA ‘LEGELEGE’ KWA WAZUNGU… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE BAMCHAWI, MANGARA WANGEKUWA ‘LEGELEGE’ KWA WAZUNGU… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, December 09, 2015

    BAMCHAWI, MANGARA WANGEKUWA ‘LEGELEGE’ KWA WAZUNGU…

    MCHANA mmoja wa Februari mwaka 1999 kilitokea kituko katika iliyokuwa hoteli ya Embassy, Dar es Salaam.
    Mara baada ya kikosi cha Al Ahly ya Misri kuwasili Dar es Salaam, msafara ulipelekwa katika hoteli ya Embassy.
    Vigogo hao wa Misri walikuja kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Raundi ya Kwanza dhidi ya Mabingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Majimaji ya Songea.
    Baada ya kufika hoteli ya Embassy, iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, msafara wa Ahly uligoma kuingia vyumbani.
    Waandishi wa Habari wa Tanzania walipohoji, kocha wa timu hiyo wakati huo, Mjerumani Reiner Zobel akawajibu kwa sababu hoteli mbaya na akaongeza; “Tukikaa hapa pachafu, tukioga maji ya hapa tutakuwa kama huyu (akimuonyeshea mfano mwandishi wa kike, Grace Hoka akitokea gazeti la Mtanzania wakati huo)”.
    Kitendo kile kililaaniwa na Waandishi wengine wote, kwa sababu Zobel alionekana kutoa kauli ya kibaguzi.
    Angeweza kusema chochote katika kuikataa hoteli ya Embassy – lakini si kumaanisha weusi wetu tuliopewa na Mungu ni kwa sababu ya uchafu.
    Hakujali, Zobel aliiongoza Ahly kuifunga Majimaji 3-0 Dar es Salaam na mchezo wa marudiano wakashinda 2-0 hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-0.
    Wakati Zobel anawakashifu weusi wa Afrika, timu ya taifa ya Tanzania ilikuwa chini ya Mjerumani mwenzake, Burkhad Pape.
    Watanzania hawakumchukia Pape kwa sababu eti Mjerumani mwenzake ametukashifu – na Waandishi wa Habari tuliendelea kumpa ushirikiano mwalimu huyo.
    Hatukuwachukia Wajerumani, au Wazungu wengine wote tunaoishi nao hapa nchini, eti kwa sababu Zobel ametudharau.
    Ni kwa sababu tunawaheshimu watu weupe, na wengine miongoni mwetu wanawaogopa na kuwaabudu kabisa Wazungu.
    Sina uhakika sana kama Mzungu anaweza akamuheismu mtu mweusi kwa dhati kabisa, lakini nayoyashuhudia katika dunia ya leo naweza kusema inawezekana.
    Naona tunaoana nao. Tunachanganya damu zetu kwa kuzaa pamoja. Tunashirikiana nao kwa namna nyingi tu. Tunaishi nao. Wanakuja kwetu, tunakwenda kwao.
    Hawapati manyanyaso yoyote wakiwa kwetu zaidi ya ukarimu uliotukuka – lakini Waafrika wananyanyasika katika ardhi za Wazungu. Huo ndiyo ukweli.
    Bila shaka msomaji wangu unaweza ukaniuliza kwa nini leo nimeakuja hivi na utashangaa zaidi mada itakavyoendelea.
    Tanzania haijaanza leo kutumia makocha wa kigeni, ni tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (sasa marehemu) rais wa nchi hii – klabu na timu za taifa zimekuwa zikitumia makocha wa kigeni.
    Wametokea baadhi ya makocha wa kigeni hapa walikuwa wana heshima na ushirikiano wa hali ya juu kwa viongozi wao, wachezaji na hata mashabiki.
    tena katika wakati ambao elimu au kujua kuongea Kiingereza havikuwa vigezo vya kupitishwa kugombea uongozi wa klabu au shirikisho.
    Amir Ally ‘Bamchawi’ (sasa marehemu) alikuwa Mwenyekiti wa Simba SC ambayo wakati wake ilifundishwa na Dragan Popadic na haikuwahi kutokea tofauti baina yao.
    Mangara Tarbu (sasa marehemu) amewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga SC ambayo wakati wake ilifundishwa na Mromania, Profesa Victor Stanslescu, lakini haikuwahi kutokea tofauti baina yao.
    Wazee wote hao, Mangara na Bamchawi (Mungu awapumzishe kwa amani) walichukuliwa kama ambao hawakuwa na elimu kubwa ya darasani, lakini walishirikiana vyema na makocha Wazungu.
    Leo hii, klabu zetu zinaongozwa na wasomi wa kiwango cha juu tu, lakini kumekuwa kuna malalamiko ya chini chini dhidi ya makocha Wazungu.
    Kweli Simba na Yanga zinafukuzana sana makocha wa Wazungu, lakini ukifuatilia kwa undani utagundua na wao wamekuwa wana matatizo.
    Ni kama wanawadharau viongozi na wengine hawawezi kushirikiana na makocha wazawa.
    Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola alifanya kazi vizuri na Patrick Phiri, Zdravko Logarusic na Goran Kopunovic, lakini akashindwa kukaa benchi moja na Muingereza Dylan Kerr.
    Kikubwa ambacho binafsi kimekuwa kinanikera ni desturi ya makocha hawa wazawa kudharau wachezaji wa nyumbani na kutoa shinikizo la idadi ya wachezaji wa kigeni kuongezwa.
    Nitaendelea kulia na hila ambazo Kerr alimfanyia Maguri hadi akamuacha Simba SC, wakati wote leo tunakiri ni mshambuliaji mzuri.
    Leo, Azam FC, Simba na Yanga zikiingia uwanjani, asilimia 60 wanacheza wachezaji wa kigeni na hizo ndizo timu ambazo zinategemewa kuzalisha wachezaji wa timu yetu ya taifa.
    Safu zote za ushambuliaji za timu hizo zinategemea wageni – maana yake Taifa Stars itafute washambuliaji kutoka timu nyingine, ambao hawapati nafasi ya kucheza mashindano makubwa kama ilivyo kwa Azam, Simba na Yanga.
    Maguri amepata nafasi kikosi cha kwanza cha Stars kwa sababu msimu uliopita alikuwa Simba SC ambako alicheza mechi nyingi kubwa zilizomjengea uzoefu.
    Lakini amepoteza nafasi ya kuendelea kuwa katika klabu ambayo ingemjenga zaidi na kukuza uwezo wake, kiasi cha kuweza kuisaidia zaidi Taifa Stars.
    Na mbaya zaidi, Azam, Simba na Yanga zimeendelea kusajili wachezaji wakiwemo washambuliaji wanaong’ara katika timu nyingine, lakini haziwatumii matokeo yake wanaua viwango vyao kabla ya kuwatema.
    Viongozi wa sasa wanaoitwa wasomi wameshindwa kupambana na itikadi za makocha Wazungu wasiotaka wachezaji wa Tanzania na matokeo yake wamekuwa mstari wa mbele kuleta wachezaji wa kigeni.
    Uganda ndiyo nchi inayoongoza kwa mafanikio katika soka ya kimataifa katika ukanda huu, na ukienda katika ligi yao sidhani kama kuna mchezaji wa kigeni.
    Sasa wachezaji wa Uganda wanacheza Kenya, Tanzania na nchi nyingine – hadi Ulaya, kwa sababu nchini mwao kuna msingi mzuri tayari wa kuwapambanua kimataifa.
    Lazima wachezaji wetu wapate nafasi ya kufundishwa na hao wataalamu wa Kizungu ili waongeze ujuzi wao. Lazima wapewe nafasi na hao Wazungu ili wakuze uwezo.
    Lakini kitendo cha kuendelea kuwaacha makocha Wazungu waendelee kuwadharau wachezaji wazawa kitazidi kuitia shimoni soka yetu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAMCHAWI, MANGARA WANGEKUWA ‘LEGELEGE’ KWA WAZUNGU… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top