// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); TUNAWEZA KUWA NA AKINA SAMATTA NA ULIMWENGU WENGI IWAPO… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE TUNAWEZA KUWA NA AKINA SAMATTA NA ULIMWENGU WENGI IWAPO… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, November 11, 2015

    TUNAWEZA KUWA NA AKINA SAMATTA NA ULIMWENGU WENGI IWAPO…

    MIKONO ya wachezaji wawili wa Tanzania mwishoni mwa wiki ilishika taji kubwa zaidi la soka kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
    Hao si wengine zaidi ya washambuliaji wetu wa kimataifa, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao wameshinda taji hilo na klabu ya Tout Puissant Mazembe ya DRC. 
    Samatta alifunga bao moja na kuseti moja, TP Mazembe ikitimiza dhamira ya kutwaa ubingwa wa Afrika baada ya kuifunga 2-0 USM Alger ya Algeria Jumapili.
    Mchezo huo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa uliofanyika Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, wenyeji walipata mabao yote kipindi cha pili.

    Na Mazembe inatwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa jumla wa 4-1, baada ya awali kushinda 2-1 mjini Algiers Jumapili iliyopita.
    Samatta aliyewekewa ulinzi mkali siku hiyo na wachezaji wa USM, alilazimika kusubiri kufunga bao lake la saba katika michuano ya mwaka huu kwa penalti dakika ya 75, baada ya Rogger Asale kuangushwa.
    Samatta naye akamsetia pasi nzuri Assale kufunga bao la pili katika dakika za majeruhi baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo.
    Matokeo hayo yanamfanya Samatta pia awe mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu huu, baada ya kufikisha mabao saba, sawa na Bakri Al-Madina wa El-Merreikh ya Sudan.
    Hii maana yake huu unakuwa mwaka wa pili mfululizo, Tanzania kutoa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa, baada ya mwaka jana Mrisho Khalfan Ngassa kuongoza pia akiwa na klabu ya Yanga SC, kabla ya kuhamia Free State Stars ya Afrika Kusini msimu huu.
    Ngassa alifunga mabao sita sawa na El Hedi Belameiri wa Setif, Haythem Jouini wa Esperance na Ndombe Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC, sasa Al Ahly, ingawa Yanga SC iliishia hatua ya 32 Bora.
    Sasa Samatta na Ulimwengu wanajivunia rekodi mpya, kuwa Watanzania wa kwanza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Mbwana pia anajivunia kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga katika fainali, tena zote mbili nyumbani na ugeini.
    Awali, Samatta na Ulimwengu walivunja rekodi mbili zilizowekwa na klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam mwaka 1974 na 1993.
    1974 Simba SC iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walipotolewa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa penalti 3-0 baada ya sare ya jumla ya 1-1, kufuatia kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.
    Ni mechi ambayo Simba SC walirejea na malalamiko kwamba kipa wao, Athumani Mambosasa (sasa marehemu) alifanyiwa fujo, wakati wa upigwaji wa penalti ikiwemo kutishiwa bastola.
    Mwaka 1993 Simba SC iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza fainali ya Kikombe cha Afrika kwa ujumla na Kombe la CAF, ambalo sasa limekuwa Kombe la Shirikisho baada ya kuunganishwa na lililokuwa Kombe la Washindi.  
    Simba SC ilianza vizuri kwa kulazimisha sare ya 0-0 mjini Abidjan, Ivory Coast Novemba 12 dhidi ya Stella kabla ya kufungwa 2-0 mjini Dar es Salaam Novemba 26 mwaka huo.
    Samatta na Ulimwengu mwaka 2013 walivunja rekodi ya Simba SC kucheza fainali ya Kombe la CAF walipoichezea Mazembe katika fainali ya Kombe hilo, wakifungwa 2-0 Novemba 23 na CS Sfaxien nchini Tunisia kabla ya kushinda 2-1 Novemba 30 mjini Lubumbashi, Samatta akifunga bao la pili dakika ya 24.
    Na msimu huo, Samatta akawa mfungaji bora baada ya kufungana kwa mabao na raia wa Ivory Coast, Vincent Die Foneye aliyekuwa anachezea ENPPI ya Misri, kila mmoja akifunga mabao sita.
    Mwaka jana, 2014; Samatta na Ulimwengu wakavunja rekodi ya Simba SC kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichezea Mazembe katika hatua hiyo mechi ya kwanza wakifungwa 2-1 Septemba 20 na ES Setif nchini Algeria na marudiano wakashinda 3-2 hivyo Setif kutwaa taji kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 4-4.
    Sasa wawili hao wanaelekea kuweka rekodi nyingine ya kucheza Klabu Bingwa ya Dunia baadaye mwaka huu Japan.
    Wakati huo huo, Samatta anawania kuweka rekodi nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Anayecheza Afrika baada ya kuingia 10 bora.
    Ni matarajio ya wengi, baada ya mafaniko ya Mbwana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa ataingia kwenye orodha ya mwisho ya wachezaji watatu na baadaye kushinda tuzo hiyo.
    Ndiyo, akiwa na Medali ya Dhahabu ya Ligi ya Mabingwa, Kombe kubwa zaidi la michuano ya klabu barani na kiatu cha dhahabu, kwa nini Samatta asishinde?
    Watanzania tunamuombea Mungu tu Samatta atajwe Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika na tunaomba Mungu amfungulie milango ya kwenda kucheza Ulaya.
    Tunamuombea Mungu amfungulie milango ya mafanikio zaidi na zaidi. Lakini kwa nini dua hizo ni kwa Samatta?
    Wazi, jitihada alizoonyesha yeye binafsi kwa tu kuhakikisha anakuwa katika kiwango cha juu na kucheza kwa kujituma kiasi cha kuwa chachu ya mafanikio ya klabu yake na timu yake ya taifa kwa sasa ndiyo sababu.
    Jitihada hizo zimekuwa changamoto nzuri hata Mtanzania mwenzake, anayecheza naye Mazembe, Ulimwengu kwani naye juhudi zake zimeonekana na ingawa kwa wakati huu anatajwa Samatta, lakini hata Thom anafanya vizuri, naye tunamuombea mafanikio zaidi.
    Tuna matatizo katika mfumo wa soka yetu, kikubwa kutopenda kuwekeza katika msingi wa soka ya vijana, lakini bado pia tuna matatizo kwa wachezaji wetu wa kizazi cha sasa kutojitambua.
    Wapo wachezaji ambao wangejitambua leo tayari wangekuwa na mafanikio makubwa ambayo wanayakimbilia Samatta na Ulimwengu.
    Wahenga wanasema, yaliyopita si ndwele – hakuna sababu ya kuanza kumlaumu wala kumshutumu mchezaji yeyote, bali ipo haja kwa chipukizi wanaoinukia kwa sasa nao kuwa na kiu ya kweli ya kufika mbali kisoka zaidi ya kucheza, Azam, Simba na Yanga.
    Kwa muda mrefu imekuwa kawaida wachezaji wetu chipukizi wanapofanyiwa mahojiano na vyombo vya habari, mwisho wa siku husema; “Matarajio yangu ya baadaye ni kucheza soka ya kulipwa Ulaya”.
    Lakini jitihada haswa za kuwapeleka Ulaya hazionekani, zaidi ya mizengwe ya kuwachukia makocha wanaowapa mazoezi magumu ili wawe fiti zaidi kisoka na hatimaye kufikia kiwango cha juu kisoka. 
    Samatta na Ulimwengu baada ya kazi nzuri na Mazembe wanajiunga na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Algeria Jumamosi.
    Najua, watapokewa vizuri na wachezaji wenzao ambao watawakumbatia na kuwaambia; “hongera”.
    Ni katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kuna wachezaji wadogo wenye umri ambao walikuwa nao Samatta na Ulimwengu wakati wanakwenda Mazembe miaka minne iliyopita.
    Naamini, ni wakati sasa wa wachezaji wetu kufunguka na kuamini haya mambo yanawezekana, wakaongeza bidii na kuwa na dhamira ya kweli ya kufika mbali zaidi kisoka.
    Lazima ucheze vizuri hapa uonekane ili uondolewe hapa kama Samatta alivyonunuliwa na Mazembe mwaka 2011.
    Na ukipata nafasi hiyo, lazima ukajibidiishe ili na huko uonekane na kuanza kutakiwa na klabu za Ulaya kama Samatta. Haya mambo yanawezekana, kwa sababu hata Samatta na Ulimwengu ni wachezaji wa Tanzania pia, kwa nini wengine nao wasiweze? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNAWEZA KUWA NA AKINA SAMATTA NA ULIMWENGU WENGI IWAPO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top