// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KAMA HAKUNA KIBONDE DUNIA YA LEO, KWA NINI TANZANIA ISIITOE ALGERIA? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KAMA HAKUNA KIBONDE DUNIA YA LEO, KWA NINI TANZANIA ISIITOE ALGERIA? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, November 01, 2015

    KAMA HAKUNA KIBONDE DUNIA YA LEO, KWA NINI TANZANIA ISIITOE ALGERIA?

    TANZANIA ipo tayari kwa Kombe la Dunia? Hilo ndilo swali ambalo nimekuwa nikijiuliza wakati huu kuelekea mchezo wa mwisho wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi dhidi ya Algeria.
    Taifa Stars itacheza na Algeria mjini Dar es Salaam Novemba 14, mwaka huu katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ya mwisho ya mchujo, kabla ya kurudiana siku tatu baadaye mjini Algiers.
    Na mshindi wa jumla atakwenda kwenye droo ya makundi matano, ambayo kila timu itakayoongoza itakwenda Urusi mwaka 2018.

    Mafanikio makubwa katika soka ya Tanzania ni kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa Raundi ya Kwanza tu.
    Kwa ujumla, soka ya Tanzania haijawahi kupanda kiasi cha kuwa kwenye orodha ya timu za kumulikwa katika soka ya kimataifa na sababu nyingi zimekuwa zikitolewa juu ya mkwamo huo.
    Kubwa ni kuendesha mchezo huo bila malengo wala mipango ya kitaalamu, itakayotupa matumaini ya siku moja kuwa taifa tishio kisoka.
    Wataalamu wengi wa kigeni wanaokuja Tanzania wamekuwa wakikiri kwamba nchi yetu ina vipaji, lakini ajabu havina soko duniani.
    Havina soko kwa sababu soka yetu kwa ujumla haina mvuto ndiyo maana hata wachezaji wetu, kabla ya mapungufu yao binafsi tu, lakini watu hawajishughulishi nao.
    Roho zinatuuma kuona nchi jirani zetu zikiwa na wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya, wakati sisi Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe ya DRC ndiyo wachezaji wakubwa.
    Zaidi ya hapo tuna nini? Labda Mrisho Khalfan Ngassa anayecheza Free State Stars ya Afrika Kusini, ambayo ni timu ya kawaida tena isiyoshindania mataji, zaidi ya kushiriki tu ili iendelee kuwepo Ligi Kuu (PSL).
    Rais wa sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amekuja na mpango Mkakati wa kuikwamua soka yetu angalau, ambao utekelezaji wake unaendelea.
    Vijana wa chini ya umri wa miaka 12 wamewekwa katika shule ya Alliance Academy mjini Mwanza kuendelezwa kisoka na elimu, ili waje kuwa wachezaji bora baadaye.
    Wakati huo huo kuna timu ya vijana chini ya umri wa miaka 15 inaandaliwa ili miaka miwili ijayo tuwe na U17 bora ya ushindani na tayari TFF imeomba uenyeji wa Mashindano ya Afrika ya U17 mwaka 2019.
    Mpango Mkakati wa Malinzi ni kutaka Tanzania icheze Olimpiki ya mwaka 2020 Japan na baada ya hapo iende Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar na utekelezaji wake umeanza.
    Kuwa na Mpango Mkakati ni hatua moja, na kufanikiwa ni hatua nyingine. Afrika ina nafasi tano za Kombe la Dunia na mchakato wake ni kama huu, mrefu unaoanzia mbali, hivyo na bahati pia inahusika hapa. 
    Wakati Mpango Mkakati wa TFF unatuelekeza tutacheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2022 Qatar, lakini tupo kwenye mbio za Kombe la Dunia la Urusi 2018.
    Mara ilipotoka ratiba ya mechi za mchujo ikionyesha Tanzania itaanza na Malawi, wengi waliokatia tamaa soka yetu hawakuamini kama tutawatoa.
    Tumefanikiwa kuwatoa kwa kuwafunga 2-1, tukishinda 2-0 Dar es Salaam na wao wakatufunga 1-0 Blantyre- na sasa mbele yetu kuna Algeria.
    Timu namba moja kwa ubora wa soka barani na timu iliyofanya vizuri zaidi kati ya timu za Afrika zilizocheza Kombe la Dunia mwaka jana Brazil.
    Kuna watu hawataki hata kusikia mtu anasema tunaweza kuwatoa Algeria. Na hawataki kusikia chochote kuhusu mkakati wa maandalizi ya mchezo, wakiamini tumekwishatolewa.
    Lakini wanasahau kwamba soka haiko hivyo na ndiyo maana tumekuwa tukitilia shaka uelewa wao juu ya mchezo huo, pamoja na dhamana kubwa waliyojibebesha.
    Wachambuzi waliobobea kwenye soka ya kimataifa na makocha wa viwango vya juu, wamekuwa wakisema katika dunia ya leo hakuna tena timu kibonde katika mchezo huu. 
    Kauli hiyo aliirudia kiungo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Sunday Oliseh ambaye sasa ni kocha wa Super Eagles baada ya sare ya 0-0 na Tanzania, tena timu yake ikikoswa mabao matatu ya wazi.
    Lakini hapa Tanzania tuna wachambuzi wa ‘Redio Mbao’ wao kila siku wanawakatisha tamaa Watanzania, eti hatuwezi kutoka kwa Algeria.
    Siyo kwa sababu tuna Mpango Mkakati wa kutuelekeza Kombe la Dunia la Qatar 2022, basi tuachane na harakati nyingine- hapana.
    Hata Watanzania wenyewe hawana imani kwamba tunaweza kucheza Kombe la Dunia la Urusi, lakini wanatamani matokeo mazuri dhidi ya Algeria, jambo ambalo linawezekana iwapo tutaachana na dhana potofu na hasi na wote kuamua kuiunga mkono timu yetu. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA HAKUNA KIBONDE DUNIA YA LEO, KWA NINI TANZANIA ISIITOE ALGERIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top