// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); ESTHER CHABURUMA; ANAYETUNGIKA DALUGA NA MOTO WAKE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE ESTHER CHABURUMA; ANAYETUNGIKA DALUGA NA MOTO WAKE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, November 09, 2015

    ESTHER CHABURUMA; ANAYETUNGIKA DALUGA NA MOTO WAKE

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    UKIZUNGUMZIA mafanikio ya soka la wanawake nchini, hakika  huwezi kuliweka mbali jina la mshambuliaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania (Twiga Stars), Esther Chabruma maarufu kwa jina la Lunyamila.
    Mapema wiki hii Chabruma alitangaza kutundika daluga la kimataifa na kwa heshima ya mchango wake, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kutumia mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Twiga Stars na Malawi kumuaga nyota huyo.
    Spotika lilifanya mahojiaho maalum na mshambuliaji huyo kufahamu ni sababu ipi imepelekea kufanya uamuzi huo wa kuitumikia nchi yake hali ya kuwa kiwango chake bado hakijashuka.
    Esther Chaburuma 'Lunyamila' akizunguka Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na bendera yake kuwagaa mashabiki juzi 

    SABABU ZA KUSTAAFU
    Chabruma aliitaja sababu kubwa iliyomfanya aamue kutundika daluga la kimataifa chini ni kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kulitumikia taifa lao.
    Mshambuliaji huyo alisema kwamba ameitumikia ameitumikia Twiga Stars kwa muda wa miaka 15 mfululizo na sasa wakati umefika wa kukaa pembeni ili wachezaji wengine wenye uwezo kuichezea timu hiyo.
    "Nimeichezea muda mrefu, miaka 15 inatosha, wapo chipukizi wengi wanauwezo nao muda wao wa kucheza umefika, isiwe kila siku Esther tu," alisisitiza mshambuliaji huyo.
    Alisema kwamba anataka kuona wachezaji wengine wanajifunza kupitia kwake na kuamini hakuna kisichowezekana katika maisha ya ndani na nje ya soka.
    Esther Lunyamila akimiliki mpira katikati ya wachezaji wa Wamalawi

    CHANGAMOTO ALIZOPITIA
    Chabruma alisema kwamba maneno ya majirani zao ndiyo yalikuwa yakimuumiza kichwa lakini wazazi wake waliyapuuzia na kuendelea kumpa sapoti katika kuendeleza kipaji chake.
    "Mama na baba hawakuwa na shida, waliuniunga mkono na kunisaidia, ila majirani ndiyo walikuwa wanaleta maneno maneno maneno, kila siku walikuwa wanawaambia wazazi wangu kuwa wakiniacha nicheze mpira nitakuwa mhuni, mvuta bangi au nitaacha shule," alisema nyota huyo ambaye ni mtoto wa saba kuzaliwa kati ya watoto tisa wa familia ya Mzee Chabruma.
    Hawakuwasiliza na kila siku kaka yake (Morgan) alikuwa anamchukua na kwenda naye mazoezini kwa ajili ya kumfundisha zaidi.
    Esther Lunyamila akiwaaga mashabiki juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi

    ANACHOJIVUNIA 
    Nyota huyo alisema kwamba soka limemsaidia kujipatia kipato cha kuendeleza maisha yake na vilevile kusafiri nchi mbalimbali duniani na kuitaja klabu ya Kotodora aliyoichezea kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2003 mpaka 2006.
    "Mimi ndiyo mchezaji wa kwanza wa kike kwenda nje kucheza mpira, nimekaa Sweden miaka mitatu, nimesafiri nchi mbalimbali kwa ajili ya kuitumikia Tanzania na wakati mwingine katika mazingira magumu ," alisema.
    Hata hivyo hakutaka kuweka wazi soka limempatia mali gani ambayo akiitazama anajivunia.
    Amewataka wachezaji chipukizi kuwa na nidhamu ndani na nje ya nchi na hiyo itawasaidia kulinda vipaji vyao na kufanya mazoezi binafsi na si kutegemea yale ya makocha pekee.
    Esther Lunyamila amestaafu soka kwa heshima kubwa

    MECHI NGUMU/KALI
    Aliitaja mechi ya marudiani kati ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Ethiopia dhidi ya Twiga Stars iliyofanyika Addis Ababa kuwa ndiyo mechi ngumu na iliyokuwa na ushindani mkubwa kati ya mechi zote alizowahi kucheza.
    "Hata hivyo Mungu mkubwa, tulishinda 3-1 na Tanzania tutafuzu kwenda Afrika Kusini (Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake -AWC) ilikuwa 2010," aliongeza.
    Akiwa na timu yake ya Sayari Queens, aliutaja mchezo wao dhidi ya Mburahati Queens uliokuwa wa kuwania kikombe maalum na wao kushinda mabao 2-0 (alifunga yeye na Fatuma Mustapha 'Kitunini') ndiyo hataisahau kwa sababu kila upande siku hiyo walicheza mpira wa kiwango cha juu.
    Esther Chaburuma akipewa zawadi kutoka Azam TV baada ya kustaafu

    SERIKALI YA MAGUFULI
    Mchezaji huyo ambaye hana mpango wa kuihama Sayari Queens ambayo ameichezea kwa zaidi ya miaka 18 amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kuwekeza katika timu za wanawake kama zilivyo wanaume ili kuleta usawa.
    "Serikali itupe sapoti kubwa, ikiwezeka kwa wanawake tutafanya vizuri zaidi, tukiwezeshwa, tunaweza," aliongeza.

    (Somoe Ng'itu ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe na Katibu wa Chama cha Soka Wanawake, TWFA)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ESTHER CHABURUMA; ANAYETUNGIKA DALUGA NA MOTO WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top