// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); TUTAKUWA WA AJABU TUKICHEZA NA ALGERIA KWA MAANDALIZI YA SIKU NNE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE TUTAKUWA WA AJABU TUKICHEZA NA ALGERIA KWA MAANDALIZI YA SIKU NNE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, October 14, 2015

    TUTAKUWA WA AJABU TUKICHEZA NA ALGERIA KWA MAANDALIZI YA SIKU NNE

    TANZANIA imetinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya kufungwa 1-0 na Malawi Jumapili mjini Blantyre.
    Tanzania, Taifa Stars imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya Jumatano kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, bao pekee la Mwale lilifungwa na John Banda dakika ya 42.
    Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo Novemba.

    Baada ya matokeo hayo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ametoa maoni na mipango yake kuelekea mchezo ujao na Algeria.
    ‘Master’ Mkwasa amesema kwamba anahitaji wachezaji wapya wanne bora kuongeza katika timu yake kabla ya mchezo na Algeria.
    Hao ni beki wa kati, kiungo wa ulinzi, kiungo mchezeshaji na mshambuliaji, ambao amesema atawatafuta katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanzia sasa.
    Ikumbukwe mchezo wa kwanza Taifa Stars na Algeria utachezwa Dar es Salaam Novemba 14 na marudiano Novemba 17 Algiers. 
    Mkwasa amesema muda wa maandalizi uliopangwa kuelekea mchezo na Algeria ni mfupi, hivyo amepanga kukutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuangalia uwezekano wa kuongeza muda.
    Amesema kwamba TFF imepanga Taifa Stars iweke kambi ya siku nne kujiandaa na mechi na Algeria kuanzia Novemba 9, ambazo Mkwasa amesema ni chache.
    Mkwasa amesema ataishauri TFF kuahirisha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania za timu ambazo zinatoa wachezaji wengi timu ya taifa, ambazo kwa kawaida huwa ni Azam FC, Simba na Yanga SC.  
    “Nitashauri mechi zao (Azam FC, Simba na Yanga) ambazo zimepangwa kuchezwa Novemba 7 ziahirishwe, ili zichezwe kabla ya Kombe la Challenge, ili tupate muda mrefu kidogo wa maandalizi kabla ya mechi na Algeria,” amesema Mkwasa.
    Mechi za Ligi Kuu Novemba 17 ni Mgambo Vs Yanga SC mjini Tanga, Kagera Sugar Vs Ndanda FC mjini Tabora, Stand United Vs Mwadui FC mjini Shinyanga, Mbeya City Vs Mtibwa Sugar mjini Mbeya, Azam FC Vs Simba SC mjini Dar es Salaam na Majimaji FC Vs Toto Africans mjini Songea.
    Novemba 8, raundi hiyo itahitimishwa kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Prisons mjini Dar es Salaam, Coastal Union Vs African Sports mjini Tanga, kabla ya mapumziko ya maandalizi ya mchezo na Algeria Novemba 9 Dar es Salaam hadi Novemba 17.
    Baada ya hapo kutakuwa na mapumziko ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Challenge kuanzia Novemba 15 hadi Desemba 15.
    Ushauri wa Mkwasa ni mzuri, huwezi kuingia uwanjani kucheza na timu bora Afrika, Algeria ukiwa na maandalizi ya siku nne. Huo ni mzaha.
    Tunafahamu wapenzi wa soka nchini hawapendi ratiba ya Ligi Kuu ipanguliwe mara kwa mara, lakini hii ni dharula ambayo inatulazimisha kufanya hivyo.
    Hakuna namna nyingine zaidi ya kupangua Ratiba ya Ligi Kuu, ili kweli mechi za vigogo hao watatu wenye mchango mkubwa wa wachezaji Taifa Stars zisogezwe mbele.
    Na Mkwasa ametoa wazo zuri tu kwamba mechi hizo za viporo zichezwe kabla ya kambi ya kujiandaa na Kombe la Challenge.
    Tumeona mchezo wa marudiano na Malawi ulivyokuwa mgumu Jumapili mjini Blantyre kwa sababu timu haikuwa na maandalizi mazuri.
    Algeria wenyewe wameanza muda mrefu kujiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi yetu na Kocha Msaidizi wa timu hiyo Nabil Neghiz aliongozana na Meneja Walid Sadi kushuhudia mechi zote mbili za Tanzania na Malawi nyumbani na ugenini.
    Tutakuwa watu wa ajabu mno, kama kweli tutaingia kumenyana na Algeria baada ya maandalizi ya siku nne.  Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUTAKUWA WA AJABU TUKICHEZA NA ALGERIA KWA MAANDALIZI YA SIKU NNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top