BONDIA Manny Pacquiao amesema kwamba ameachana na ndoto za pambano la marudiano na Floyd Mayweather kutokana na mpinzani wake huyo kutangaza kustaafu kufuatia kumshinda kwa pointi Andre Berto mwishoni mwa wiki.
Mayweather alimshinda kwa pointi Pacquiao Mei mwaka huu katika pamabano la utajiri mkubwa wa ndondi na baada ya kumshinda Berto katika pambano lake la 49 mfululizo kushinda, ametangaza kustaafu akiwa hajapoteza pambano.
Hata hivyo, mashabiki walikuwa wanataka kuona akirudiana na Pacquiao kwa sababu katika pambano baina yao, Mfilipino huyo alipigana akiwa ana maumivu ya bega na pia hivi karibuni imeripotiwa Mayweather alitumia dawa zilizopigwa marufuku mchezoni. Pac Man anatarajiwa kuwa fiti kurejea ulingoni mwakani baada ya kupona bega.
Mbabe wa Ufilipino, Manny Pacquiao anaendelea kuuguza bega lake na atakuwa tayari kupanda tena ulingoni mwakani PICHA ZAIDI GONGA HAPA
"Ngumi si kitu nachofikiria kwa sababu naweza kupigana mwakani tu, ili kulipa mapumziko bega langu,"amesema Pacquiao leo ambaye anaendelea na matibabu ya bega lake la kulia aliloumia mazoezini kujiandaa na pambano dhidi ya Mayweather.
Mbabe huyo ambaye pia ni mwanasiasa nchini kwao, amesema kwa sasa ameelekeza nguvu zake katika ujenzi wa nyumba za watu wasio na makazi kusini mwa nyumbani kwao, jimbo la Sarangani.
"Niko sawa. Kuwe na pambano la pili (dhidi ya Mayweather), si tatizo," amesema. "Nimesikia amestaafu, haijalishi,". Kwa pambano lijalo, amesema atapigana na bondia yeyote. "Kwa sababu sichagui wapinzani wangu,".
Pacquiao pia amesema alikuwa anasubiri kuona Mamlaka za ndondi Marekani zitamchukulia hatua gani Mayweather kwa kutumia sindano ya dawa za IV baada ya kupima uzito kabla ya pambano lao mjini Las Vegas.
0 comments:
Post a Comment