// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MARA HII TUMEANZA UBAGUZI TAIFA STARS? MALINZI KAZI KWAKE! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MARA HII TUMEANZA UBAGUZI TAIFA STARS? MALINZI KAZI KWAKE! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, September 09, 2015

    MARA HII TUMEANZA UBAGUZI TAIFA STARS? MALINZI KAZI KWAKE!

    TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars mwishoni mwa wiki imetoa sare ya 0-0 na Nigeria katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.
    Stars ilifikisha mechi mbili bila ushindi- baada ya kufungwa mabao 3-0 na Misri katika mchezo wa kwanza- lakini Watanzania walifurahishwa na kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla baada ya mchezo wa huo.
    Ilikuwa mechi ya pili ya mashindano Stars inacheza chini ya kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa tangu akabidhiwe timu Julai.
    Mkwasa alipewa timu ikiwa katika hali mbaya, ikitoka kufungwa mechi tano mfululizo chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij akaanza na sare ya 1-1 ugenini na Uganda mjini Kampala kufuzu CHAN.

    Sifa zinakwenda kwa Mkwasa, lakini inafahamika hafanyi kazi peke yake, kwani ana Mshauri, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Wasaidizi, Hemed Morocco na Manyika Peter anayewanoa makipa.
    Baada ya mchezo huo, kila Mtanzania ameyapokea kwa namna yake matokeo hayo- wengi wakiamini mambo yatakuwa mazuri zaidi chini ya Mkwasa.
    Wenzetu wa Yanga SC, wao walifurahishwa tu na kuona wachezaji wao wengi wakianza katika mechi hiyo, huku mahasimu wao, Simba SC wakiwa hawana hata mmoja.
    Katika mchezo huo, Mkwasa aliwaanzisha Ally Mustafa ‘Barthez’, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wote wa Yanga SC, Shomary Kapombe, Himid Mao, Farid Mussa, Mudathir Yahya wote wa Azam FC, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya DRC na Mrisho Ngassa wa Free State Stars ya Afrika Kusini. 
    Kipindi cha pili aliwatoa Mudathir, Ngassa na Farid na kuwaingiza Said Ndemla wa Simba SC, John Bocco wa Azam FC na Simon Msuva wa Yanga SC.
    Baada ya mchezo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC akatamba kwenye vyombo vya habari, kwamba timu yao ni ya kimataifa na ndiyo maana safu yake ya ulinzi ilitumika dhidi ya Nigeria na kulinda vizuri.
    Muro alizungumza ukweli- kwani karibu safu yote ya ulinzi ya Stars ilitengenezwa na wachezaji wa Yanga SC, lakini tu umekuwa ukweli ambao unaweza kuleta athari kubwa ukiachwa hivyo hivyo.
    Timu ya taifa huundwa na wachezaji ambao wako katika kiwango kizuri kwa wakati husika, na wakati mwingine kocha huchukua wachezaji ambao wanaendana na falsafa yake.
    Ndiyo, kuna wakati mchezaji ambaye watu wanaona ni bora, lakini akaachwa timu ya taifa kwa sababu kocha anaona haenei katika mipango yake.
    Hivyo tambo za Muro zimepokewa kwa hisia hasi na wapinzani wao wa jadi, Simba SC. 
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amemtaka Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwachukulia hatua viongozi wa Yanga SC wanaotoa kauli za uchochezi kuhusu timu ya taifa.
    Poppe alisema kwamba baada ya mechi ya Taifa Stars na Nigeria Jumamosi, baadhi ya vingozi wa Yanga wameanza kuzungumza kauli za ubaguzi na uchochezi kuhusu Taifa Stars.
    “Nimemsikia kiongozi mmoja wa Yanga (Muro) anatamba eti Taifa Stars ni ya wachezaji wa Yanga ndiyo timu ya kimataifa. Kauli kama hizi ni za hatari na zitaleta mgawanyiko tena katika timu.
    Yanga ni wapinzani wetu, leo kusema Taifa Stars ni Yanga maana yake haituhusu Simba, je mashabiki wa Simba wakiisusa timu itakuwaje?”alihoji Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kuongeza.
    “Malinzi anatakiwa kuwachukulia hatua viongozi wa Yanga waliotamka maneno hayo hatari ya kibaguzi na yenye kuhatarisha umoja na mshikamano uliopo ndani ya timu kwa sasa,”.
    Poppe amesema Watanzania sasa wameunganisha nguvu zao kuisapoti timu yao kwa nguvu zote bila kujali itikadi, lakini wanatokea watu wenye kutaka kuubomoa umoja huo- hivyo Malinzi anapaswa kuchukua hatua.
    “Sisi tunaheshimu maamuzi ya TFF kumchukua kocha wa Yanga (Charles Boniface Mkwasa) kufundisha timu japokuwa tunajua Malinzi ni mwanachama wa Yanga na kiongozi wa zamani wa Yanga,”.
    “Tumeheshimu maamuzi ya kocha Mkwasa kupanga wachezaji wake wa Yanga wengi bila kumuanzisha hata mchezaji mmoja wa Simba, lakini hiyo haitoshi, bado wanaanza kuongea pumba kwenye vyombo vya habari,”amesema.
    Poppe amesema wakati wa mwanzo wa kambi ya maandalizi ya mchezo huo, wachezaji wa Yanga SC hawakujiunga na kambi na TFF haikuchukua hatua yoyote- bado Simba wamenyamaza.
    Mfanyabiashara huyo maarufu nchini amewataka mashabiki wa Simba SC kuendelea kuisapoti timu ya taifa bila kujali inafundishwa na nani na wachezaji gani wanacheza, kwa kuwa inavaa jezi za bendera ya nchi.
    “Wakati tunasubiri kuona TFF itachukua hatua gani, ninawaomba Watanzania na mashabiki wa Simba kuyapuuza maneno ya kifedhuli ya watu wenye kutaka kuvuruga umoja na mshikamano katika timu ya taifa,”amesema. 
    Alichokisema Hans Poppe ni sahihi kabisa, maneno ya Muro yanaweza kuleta mtafaruku ambao hatuuhitaji kwa sasa katika timu yetu.
    Siamini kama Muro alifikiria athari zinazoweza kusababishwa na maneno yake kabla ya kusema- kwa sababu ni kiongozi mweledi, msomi na wa mjini angefikiri kwanza, asingethubutu kufanya hivyo.
    Hakuwa na sababu ya kusema aliyoyasema- wakati huu wana Yanga SC wanataka kujua mengi kuhusu timu yao ambayo labda Muro angezungumza, lakini akaenda kutoa kauli ambazo sasa zinataka kutuletea vurugu.
    Katika suala la timu ya taifa, tunapaswa kuwa na mitazamo ya kitaifa na kuondoa fikra za ubinafsi, kwani matokeo yake tutaanza kumyumbisha kocha afikie kuunda timu kwa kufikiria kuweka uwiano sawa wa SImba na Yanga badala ya kuzingatia ubora wa wachezaji.
    Mchezaji wa Simba SC, Yanga SC au Azam FC ni wakati amevaa jezi ya klabu yake- anapokuwa na jezi ya timu ya taifa, huyo ni wa Taifa Stars.  Lazima wote tufikirie hivyo ili kuimarisha umoja katika timu yetu ya taifa.
    Muro hajasema uongo, kwani ni kweli wachezaji wa Yanga SC ni wengi timu ya taifa kuliko wa Simba, lakini maneno yake yana tafsiri ya ubinafsi na ubaguzi, kitu ambacho ni sumu mbaya.
    Poppe amemuambia Rais wa TFF, Malinzi amchukulie hatua Muro- ni kweli huyu bwana mkubwa anastahili kupewa onyo na kukumbushwa juu ya uzalendo.
    Tunapenda kuendelea kuona timu yetu ya taifa inapocheza inashabikiwa na Watanzania wote bila kujali itikadi zao- lakini kwa maneno ya Muro hilo linaweza kuwa shakani.
    Ubaguzi huanza na viashiria na kubwa zaidi ni ubinafsi- leo huyu atasema Yanga wengi Taifa Stars, kesho yule atasema Wakristo wengi, na mwingine atakuja kusema Wamakonde wengi. Tutakuwa tunapanda mbegu gani Taifa Stars?
    Nadhani kabla ya TFF kumchukulia hatua Muro, yeye mwenyewe angerudi kwenye vyombo vya Habari kuwaomba Radhi Watanzania kwa usumbufu wowote aliousababisha kutokaana na kauli zake. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MARA HII TUMEANZA UBAGUZI TAIFA STARS? MALINZI KAZI KWAKE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top