// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KIU YA WATANZANIA NI USHINDI TAIFA STARS, MKWASA BADO KAZI ANAYO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KIU YA WATANZANIA NI USHINDI TAIFA STARS, MKWASA BADO KAZI ANAYO! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, September 06, 2015

    KIU YA WATANZANIA NI USHINDI TAIFA STARS, MKWASA BADO KAZI ANAYO!

    MAELFU ya mashabiki wa soka wa Tanzania, jana waliondoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam nafasi zao zikiwa zimefarifika licha ya timu yao ya taifa kulazimishwa sare ya 0-0 na wageni Nigeria.
    Mchezo huo wa Kundi G kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2017 ulikuwa mkali na wa kusisimua na pamoja na timu zote kushambuliana kwa awamu, lakini ni wenyeji waliotengeneza nafasi zaidi.
    Wastani wa nafasi tano na tatu za wazi zaidi wachezaji wa Tanzania walipoteza jana na sifa zimuendee kipa Carl Ikeme Onora anayedakia Wolves ya England aliyeokoa hatari mbili langoni mwake, zote za Mrisho Ngassa.
    Watanzania walifurahishwa na kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla baada ya mchezo wa jana- ambao ulikuwa ni wa pili tu mashindano kwa kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa tangu akabidhiwe timu mwezi uliopita.
    Mkwasa alipewa timu ikiwa katika hali mbaya, ikitoka kufungwa mechi tano mfululizo chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij akaanza na sare ya 1-1 ugenini na Uganda mjini Kampala kufuzu CHAN.
    Sifa zinakwenda kwa Mkwasa, lakini inafahamika hafanyi kazi peke yake, kwani ana Mshauri, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Wasaidizi, Hemed Morocco na Manyika Peter anayewanoa makipa.
    Lakini siku zote, lawama na sifa huanzia kwa anayeitwa Kocha Mkuu- hivyo kwa sasa acha sifa zimuendee kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na Yanga SC.
    Ukweli ni kwamba timu yetu ya taifa imebadilika si kwa sura za wachezaji kwamba pale langoni hayupo tena Deo Munishi ‘Dida’ kuna Ally Mustafa ‘Barthez’ au beki ya kushoto kuna Mwinyi Hajji Mngwali badala ya Oscar Joshua- la hasha, bali hata kwa uchezaji pia.
    Baada ya mechi Mkwasa aliwaambia Waandishi wa Habari kwamba sasa anaona mwanga fulani kuelekea kwenye mafanikio- niungane naye, baada ya kipidi kifupi kazi aliyoifanya inaleta matumaini.
    Mchezo wa jana lilikosekana bao tu ambalo vijana walilitafuta kwa juhudi kubwa, niseme haikuwa bahati yao.
    Lakini pia, tusisahau Tanzania ilikutana na Nigeria bora yenye kizazi kipya wachezaji wanaopambana kurejesha heshima ya nchi yao katika soka ya kimataifa.
    Ni hii timu iliyofika hatua ya mtoano ya 16 Bora Kombe la Dunia mwaka jana Brazil na kutolewa na Ufaransa kwa kufungwa 2-0 Juni 30 Uwanja wa Taifa wa Mane Garrincha mjini Brasilia, mabao ya Paul Pogba dakika ya 79 na la kujifunga la beki Joseph Yobo dakika ya 90 na ushei.
    Kwa wenye kuikumbuka mechi hiyo, Super Eagles walicheza sana mpira na bahati mbaya wakashindwa kumalizia vizuri- kwani wakati wanasaka bao la kusawazisha, Yobo akawanyong’onyesha wenzake kwa kujifunga.
    Waliokosekana jana kutoka kile kikosi cha Kombe la Dunia ni wale ‘mafaza’ ambao waligharimu timu akiwemo Yobo, na kocha mpya Sunday Oliseh ameshikia pale pale alipoachia Stephen Keshi, kutengeneza kikosi cha damu mpya.
    Na ukirudi kwenye kikosi cha Tanzania, jana tumeona wachezaji vijana wadogo kama Mudathir Yahya, Said Ndemla, Mwinyi Mngwali, Farid Mussa wakipewa dhamana ambao wote umri wao ni chini ya miaka 23.
    Kundi la pili ni la vijana chini ya umri wa miaka 25 akina Shomary Kapombe, Himid Mao, Mbwana Samatta, Simon Msuva na waliozidi miaka 25, lakini hawafiki miaka 30 akina Mrisho Ngassa, John Bocco, Kevin Yondan, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Nadir Haroub ‘Cannavaro’. 
    Wakati bado tunafikiria kuzalisha nyota wa baadaye, Mkwasa ametuonyesha kwamba hadi kufika Desemba tunaweza kuwa na timu nzuri ya ushindani kutokana na kikosi cha sasa.
    Waswahili wanasema maji yakimwagika hayazoleki na yaliyopita si ndwele, lakini ukweli unabaki pale pale tutaendelea kuujutia muda tuliopoteza chini ya kocha Nooij.  
    Mara baada ya mchezo wa jana, wakati wengine wakifurahia soka nzuri ya matumaini, mimi nilikuwa ninajiuliza, kama timu ingekuwa bado ipo chini ya Nooij, matokeo yangekuwaje?
    Ukweli ni kwamba kutoka kufungwa 3-0 na Uganda nyumbani katika mechi ya kufuzu CHAN hadi jana kutoa sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani ni hatua kubwa. Hongera kwa Mkwasa na timu yake ya benchi la ufundi pamoja na wachezaji, lakini tu wasibweteke, kiu ya Watanzania si kucheza vizuri tu, bali kushinda. Kazi bado wanayo. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIU YA WATANZANIA NI USHINDI TAIFA STARS, MKWASA BADO KAZI ANAYO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top