// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HANS POPPE AMTAKA MALINZI AWAADABISHE VIONGOZI YANGA WANAOTAKA KUVURUGA AMANI TAIFA STARS - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HANS POPPE AMTAKA MALINZI AWAADABISHE VIONGOZI YANGA WANAOTAKA KUVURUGA AMANI TAIFA STARS - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Tuesday, September 08, 2015

    HANS POPPE AMTAKA MALINZI AWAADABISHE VIONGOZI YANGA WANAOTAKA KUVURUGA AMANI TAIFA STARS

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amemtaka Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwachukulia hatua viongozi wa Yanga SC wanaotoa kauli za uchochezi kuhusu timu ya taifa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Poppe amesema kwamba baada ya mechi ya Taifa Stars na Nigeria Jumamosi, baadhi ya vingozi wa Yanga wameanza kuzungumza kauli za ubaguzi na uchochezi kuhusu Taifa Stars.
    “Nimemsikia kiongozi mmoja wa Yanga anatamba eti Taifa Stars ni ya wachezaji wa Yanga ndiyo timu ya kimataifa. Kauli kama hizi ni za hatari na zitaleta mgawanyiko tena katika timu.
    Yanga ni wapinzani wetu, leo kusema Taifa Stars ni Yanga maana yake haituhusu Simba, je mashabiki wa Simba wakiisusa timu itakuwaje?”alihoji Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kuongeza.
    Hans Poppe (kushoto) ametaka TFF iwachukulie hatua wanaotaka kuvuruga umoja Taifa Stars

    “Malinzi anatakiwa kuwachukulia hatua viongozi wa Yanga waliotamka maneno hayo hatari ya kibaguzi na yenye kuhatarisha umoja na mshikamano uliopo ndani ya timu kwa sasa,”.
    Poppe amesema Watanzania sasa wameunganisha nguvu zao kuisapoti timu yao kwa nguvu zote bila kujali itikadi, lakini wanatokea watu wenye kutaka kuubomoa umoja huo- hivyo Malinzi anapaswa kuchukua hatua.
    “Sisi tunaheshimu maamuzi ya TFF kumchukua kocha wa Yanga (Charles Boniface Mkwasa) kufundisha timu japokuwa tunajua Malinzi ni mwanachama wa Yanga na kiongozi wa zamani wa Yanga,”.
    “Tumeheshimu maamuzi ya kocha Mkwasa kupanga wachezaji wake wa Yanga wengi bila kumuanzisha hata mchezaji mmoja wa Simba, lakini hiyo haitoshi, bado wanaanza kuongea pumba kwenye vyombo vya habari,”amesema.
    Poppe amesema wakati wa mwanzo wa kambi ya maandalizi ya mchezo huo, wachezaji wa Yanga SC hawakujiunga na kambi na TFF haikuchukua hatua yoyote- bado Simba wamenyamaza.
    Kikosi cha Taifa Stars kilichoanza Jumamosi, kutoka kulia waliosimama ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Mwinyi Mngwali, Thomas Ulimwengu, Ally Mustafa 'Barthez', Himid Mao na Mbwana Samatta. Walioinama kutoka kulia ni Kevin Yondan, Shomary Kapombe, Mrisho Ngassa, Farid Mussa na Mudathir Yahya. 

    Mfanyabiashara huyo maarufu nchini amewataka mashabiki wa Simba SC kuendelea kuisapoti timu ya taifa bila kujali inafundishwa na nani na wachezaji gani wanacheza, kwa kuwa inavaa jezi za bendera ya nchi.
    “Wakati tunasubiri kuona TFF itachukua hatua gani, ninawaomba Watanzania na mashabiki wa Simba kuyapuuza maneno ya kifedhuli ya watu wenye kutaka kuvuruga umoja na mshikamano katika timu ya taifa,”amesema. 
    Jumamosi Taifa Stars ilitoa sare ya 0-0 na Nigeria katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, huo ukiwa mchezo wa tatu kwa Mkwasa tangu akabidhiwe mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij Julai mwaka huu.
    Katika mchezo huo, Mkwasa aliwaanzisha Ally Mustafa ‘Barthez’, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wote wa Yanga SC, Shomary Kapombe, Himid Mao, Farid Mussa, Mudathir Yahya wote wa Azam FC, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya DRC na Mrisho Ngassa wa Free State Stars ya Afrika Kusini. 
    Kipindi cha pili aliwatoa Mudathir, Ngassa na Farid na kuwaingiza Said Ndemla wa Simba SC, John Bocco wa Azam FC na Simon Msuva wa Yanga SC.
    Malinzi alimteua Mkwasa kukaimu Ukocha Mkuu Taifa Stars kwa miezi mitatu tangu Julai na akasema kwa kuanzia atakuwa anachukua mshahara alikuwa analipwa Nooij. 
    Nooij aliyekuwa analipwa dola za Kimarekani 12,500 (zaidi ya Sh. Milioni 25) kwa mwezi, alifukuzwa mwishoni mwa Juni baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mechi ya kufuzu CHAN.
    Mkwasa aliwateua kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwa Mshauri wa Ufundi, Hemed Morocco wa Zanzibar kuwa Kocha Msaidizi na kipa wa zamani wa Yanga SC, Manyika Peter kuwa kocha wa makipa.
    Aidha, beki wa zamani wa Yanga SC, Omar Kapilima aliteuliwa kuwa Meneja na mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar Hussein Swedi ‘Gaga’ kuwa mtunza vifaa vya timu- kukamilisha sura mpya kabisa ya benchi la Ufundi la Taifa Stars.
    Na tangu hapo timu imcheza mechi tatu bila ushindi ikitoa sare ya 1-1 na Uganda mjini Kampala kufuzu CHAN, ikifungwa 2-1 na Libya mchezo wa kirafiki mjini Kartepe, Uturuki na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria mwishoni mwa wiki.
    Hayo yalikuwa mabadiliko makubwa kutoka kwenye timu kufungwa mechi tano mfululizo na kwa ujumla kucheza mechi 11 bila ushindi chini ya Nooij. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE AMTAKA MALINZI AWAADABISHE VIONGOZI YANGA WANAOTAKA KUVURUGA AMANI TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top