MSHAMBULIAJI Diego Costa amefungiwa mechi tatu na Chama cha Soka England, baada ya kumkwangua kwa kucha usoni beki wa Arsenal, Laurent Koscielny Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Stamford Bridge.
Hata hivyo, katika mchezo huo ambao Chelsea ilishinda 2-0 kwa mabao ya Kurt Zouma dakika ya 53 na Eden Hazard dakika ya 90+1, Costa hakuadhibiwa kwa sababu refa hakuona.
Lakini baada ya ushahidi wa picha za video, Costa amefungiwa mechi tatu na sasa Chelsea itamkosa katika mechi dhidi ya Walsall Kombe la Ligi kesho usiku.
Nyota huyo wa Hispania mwenye umri wa miaka 26, atakosa pia mechi za Ligi Kuu dhidi ya Newcastle na Southampton, kabla ya kurejea kwenye mchezo na Aston Villa Oktoba 17.
Taarifa iliyoltolewa na Chelsea katika tovuti imesema hawaridhishwi na maamuzi hayo.
"Kabisa tumesikitishwa na uamuzi wa Kamisheni ya Kanuni ya FA kumfungia Diego Costa. Tutasubiri taarifa ya maandishi iliyotaja sababu za kumfungia ili tuchukue hatua zaidi,".
Taarifa ya FA imesema: "Kosa ambalo FA imemtia hatiani Diego Costa kwa vurugu, halikuonekana na marefa wakati anafanya, lakini ushahidi wa picha za video umemnasa vizuri na Tume huru ya Kanuni imemuadhibu,".
0 comments:
Post a Comment