// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); BAADA YA UWEKEZAJI HUU, VIGOGO WATAENDELEA KUNUNUA MECHI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE BAADA YA UWEKEZAJI HUU, VIGOGO WATAENDELEA KUNUNUA MECHI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, September 13, 2015

    BAADA YA UWEKEZAJI HUU, VIGOGO WATAENDELEA KUNUNUA MECHI?

    UKINIAMBIA lete ushahidi utanishinda. Kwa sababu sina ushahidi wa mchezaji kuhongwa, au timu kupanga matokeo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Lakini ninajua mchezo huo mchafu upo katika soka ya Tanzania- na tuhuma mbalimbali zimewahi kuanikwa, hadi kufikishwa kwenye vyombo vya dola, japokuwa hatua hazijawahi kuchukuliwa.
    Peke yake, Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amewahi kutuhumiwa mara mbili na wachezaji eti aliwapelekea hongo.
    Kesi iliishaje, Kaburu alisingiziwa au kulikuwa kuna ukweli? Sijui kwa sababu pia sijui kesi hizo zilimalizwaje.
    Achana na hayo, imekuwa kawaida kusikia klabu imesimamisha, au kufukuza kabisa wachezaji kwa tuhuma za kupokea hongo kuhujumu timu zao.

    Vigogo wote, Azam FC, Simba na Yanga SC wamewahi kusimamisha na kufukuza wachezaji waliowatuhumu kuwahujumu- na wamekuwa wakituhumiana miongoni mwao.
    Moja kati ya mambo ya awali, Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuahidi kupambana nayo baada ya kuingia madarakani mwaka juzi ni upangaji wa matokeo.
    Sijui vita yake inaendeleaje, lakini msimu uliopita baadhi ya timu zilikuwa zinabeza ushindi wa timu nyingine, zikiuita wa ‘M-Pesa’- yaani wa kununua.
    Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeanza tena jana, mabao 10 tu yakitinga nyavuni katika mechi saba za ufunguzi.
    Hakuna timu iliyoshinda kwa wastani wa zaidi ya bao 1-0 dhidi ya wapinzani wake- timu zote zote zimeshinda 1-0 na 2-1 baada ya mechi zote saba jana.
    Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba SC imewafunga bao 1-0 Africans Sports wakati Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Ndanda FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo Shooting ya Tanga.
    Uwanja wa Majimaji, Songea wenyeji Majimaji FC wameshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam FC imeshinda 2-1 dhidi ya Prisons wakati Toto Africans imeshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC.
    Timu zilizoanza kwa ‘mikosi’ zaidi Ligi ya msimu huu ni Stand United iliyofungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Mbeya City iliyofungwa 1-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itaendelea leo wakati mabingwa watetezi, Yanga SC watakapomenyana na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa tathmini ya haraka ya michezo kutokana na matokeo ya jana- inaonekana kama jana soka ilichezwa kihalali. 
    Na itapendeza kama hali hiyo itaendelea hadi Mei mwakani wakati pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam litakapokuwa linafungwa.
    Lakini uzoefu unaonyesha miaka yote, Ligi Kuu huanza namna hiyo katika hali ya ushindani halisi na baadaye ‘mazingaombwe’ huanza kujitokeza taratibu.
    Mchezo wa kupanga matokeo kwa kiasi kikubwa umekuwa ukidhoofisha soka yetu, kwa sababu tunajikuta hatupati bingwa halisi na pia tunahadaika na wachezaji ambao kumbe wanafanya vizuri ‘kimazabe’ uwanjani.
    Ndiyo maana wachezaji wetu wanafunga mabao mengi katika Ligi Kuu, lakini wakienda kwenye michuano ya kimataifa hawawezi kufanya hivyo na hao ndiyo wanageuka kuwa tegemeo la timu ya taifa.
    Kuna ajabu gani hapo timu ya taifa ya Tanzania kuwa kichwa cha mwendawazimu, ikiwa katika Ligi Kuu ya nchi mchezaji hafungi hadi mabeki wamlegezee baada ya kuhongwa.
    Ligi Kuu ya msimu huu tumeshuhudia, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likirekebisha kanuni ya idadi ya wachezaji wa kigeni, kutoka watano hadi saba.
    Na mchezaji mmoja pamoja na gharama nyingine za kumlipia kibali cha kufanya kazi nchini, mshahara na kadhalika, pia analipiwa ada ya Sh. Milioni 4 na ushei TFF. 
    Wote Azam FC, Simba na Yanga SC wamekamilisa idadi ya saba na taarifa za vyanzo zinasema wamegharamiwa fedha nyingi.
    Zote, Azam FC, Simba na Yanga SC zimekuwa na maandalizi ya muda mrefu kuelekea msimu huu wa Ligi Kuu na zina makocha wa kigeni wanaolipwa dola za Kimarekani.
    Naamini uwekezaji mzuri ndani ya Azam, Simba na Yanga ni sehemu ya siri ya mafanikio yao katika soka ya Tanzania, lakini siwezi kukataa hii dhana kwamba hata upangaji wa matokeo unawabeba.
    Japokuwa sijui Malinzi amejipanga vipi kupambana na hali hiyo, lakini nadhani wakati umefika sasa klabu hizo zenyewe zijisute kama kweli huwa zinafanya hivyo.
    Zinashinda na kuchukua ubingwa kwa rekodi nzuri hapa nyumbani, zikienda kwenye michuano ya Afrika hazifiki mbali. Faida yake nini?
    Lakini pia, baada ya uwekezaji mkubwa, kusajili wachezaji saba wa kigeni kwa mamilioni ya shilingi na kuajiri makocha wa kigeni wanaolipwa kwa dola za Kimarekani, kweli bado kuna haja ya kuendelea kununua mechi?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAADA YA UWEKEZAJI HUU, VIGOGO WATAENDELEA KUNUNUA MECHI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top