Vincent Bossou anatarajiwa kusajiliwa Yanga SC leo |
SAA 6:00 usiku wa leo dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara litafungwa na klabu zipo mbioni kutumia muda mchache uliobaki kukamilisha usajili.
Yanga SC imeleta wachezaji wawili, Mzimbabwe Thabani Kamusoko kutoka FC Platinum ya kwao na Vincent Bossou wa Togo aliyekuwa anacheza Korea Kusini.
Wawili hao wote wanatarajiwa kusaini leo ili kuwahi dirisha la usajili la Ligi Kuu kabla halijafungwa.
Lakini pia, habari zinasema kuna mchezaji mwingine mpya anaweza akasajiliwa Yanga SC leo, ingawa hajafahamika ni yupi. Yanga SC wanataka kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni leo na kwa ujumla wakamilishe usajili.
Haruna Niyonzima kulia na Amissi Tambwe kushoto wote ni wachezaji tishio katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara |
Salum Telela na Malimi Busungu ni wachezaji wengine tishio kwenye kikosi cha Yanga SC |
Hawafikirii kwamba wanahitaji kuchukua tahadhari katika kusajili, kuhakikisha kwamba wachezaji inayotaka kuwasajili kwa sasa wapo katika kiwango kizuri na wapo fiti kiasi cha kutosha.
Korea Kusini ni moja ya nchi ambazo wachezaji wanalipwa vizuri na kwa ujumla wachezaji wakubwa huondoka Ulaya kwenda nchi za Asia kama China, Korea, Japan, Qatar, Saudi Arabia kufuata maslahi mazuri.
Mchezaji anapotoka nchi kama hiyo kuja nchi masikini za Afrika, lazima kuna namna na Yanga SC wanatakiwa kabla ya kutoa fedha kumsajili Bossou wawe wamejiridhisha hakuna tatizo.
Lakini kama utakuwa usajili wa presha na shinikizo la kuwahi dirisha la usajili, haitakuwa ajabu Yanga SC wakasajili mchezaji ambaye Desemba watamvunjia Mkataba kwa kumlipa na kumruhusu aondoke.
Sina wasiwasi sana na huyu kiungo kutoka Platinum, kwa sababu ni juzi tumemuona akiichezea klabu yake dhidi ya Yanga SC katika Kombe la Shirikisho.
Lakini pamoja na hayo, Yanga SC haina tatizo kubwa sana kikosini mwake, hadi ilazimike kukamilisha idadi ya wachezaji wa kigeni hivi sasa.
Kikosi hiki cha Yanga SC ndicho kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mchezaji muhimu anayekosekana ni Mrisho Ngassa aliyehamia Free State Stars ya Afrika Kusini.
Kpah Sherman aliyehamia pia Afrika Kusini, klabu ya Mpumalanga Blac Aces hakuwa tegemeo Yanga SC na nafasi ya Ngassa wamesajiliwa wachezaji wawili, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya ambao mmoja kati yao baada ya muda ataonekana ameiziba.
Wawili hao wanahitaji muda tu kuzoea kucheza na wachezaji wenzao wapya pale Yanga SC.
Lakini pale mbele Yanga SC imesajili wachezaji wawili wapya wazuri- yaani washambuliaji, Donald Ngoma na Malimi Busungu, ambao ni wachezaji wa aina tofauti kiuchezaji.
Malimi ni mshambuliaji wa pili, ambaye anaweza sana kufunga, mjanja mjanja na aliye makini mno. Ngoma ni mshambuliaji mwenye kasi na nguvu, ambaye atakuwa anawapa wakati mgumu mabeki.
Bado Yanga SC inaye Amisi Tambwe, mfungaji bora namba mbili msimu uliopita ambaye anaweza kuwa anapokezana na Ngoma kucheza na Busungu.
Kwa aina ya majukumu ya Busungu uwanjani ni mchezaji ambaye anapaswa kuwa mchezoni muda mrefu- kwa sababu huyo ndiye anayestahili kuandaliwa kuwa mfungaji wa mabao wa timu.
Katika kiungo, Yanga SC wamesahau waliingia kwenye michuano ya Kombe la Kagame bila Said Juma Makapu ambaye ni majeruhi na ndiyo alikuwa kiungo mkabaji.
Nafasi ya kiungo mkabaji Mbuyu Twite pia hucheza kwa kulazimishwa.
Leonel alisajiliwa Azam FC kwa 'dau' la rekodi, lakini akafukuzwa baada ya miezi miwili |
Yanga SC ina viungo wachezeshaji wawili, Salum Telela na Haruna Niyonzima baada ya kumtoa kwa mkopo Hassan Dilunga na kumtema Nizar Khalfan.
Yanga SC ina mabeki wa kati wanne, Kevin Yondan, Nadir Haroub 'Cannavaro', Pato Ngonyani na Rajab Zahir ambao wote kwa ligi ya nyumbani ni wazuri. Na hata kwenye mchuano ya Afrika tangu mwaka juzi, ukuta huu wa Yanga umekuwa hauruhusu mabao mengi, maana yake klabu haina shinikizo la usajili wa pupa wa beki wa kati.
Kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kikosi hiki cha Yanga SC ni tishio kabisa- ila linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa Afrika ndipo unapoona umuhimu wa kuboresha kikosi kidogo.
Lakini si kuboresha kikosi kwa pupa kiasi cha kusajili magarasa- bali kufanya usajili makini.
Joseph Tetteh Zutah alisajiliwa Juni, lakini sasa anatupiwa virago na ni mchezaji ambaye alipendekezwa na kocha Mkuu wa timu, Hans van der Pluijm ambaye alisema anamjua alimfundisha Ghana.
Wasifu wa Kpah Sherman wakati anajiunga na Yanga SC Desemba mwaka jana ulikuwa ‘unatisha’ na mwonekano wake baada ya kutua hapa nchini ndiyo uliwalainisha kabisa kocha wa Yanga SC wakati huo, Mbrazil Marcio Maximo akapewa Mkataba mnono.
Lakini mwisho wa siku Sherman hakuwa na mchango uliotarajiwa ndani ya Yanga SC ingawa inaelezwa kwamba maisha yake ya nje ya Uwanja yalichangia hali hiyo.
Yanga SC wanahitaji kujua hata tabia ya mchezaji kabla ya kumsajili- je halitakuwa tatizo kwenye chumba cha kubadilishia nguo? Hatakuwa mchezaji majivuno mwenye kujisikia, atakayeigawa timu?
Hatakuwa mchezaji anayendekeza anasa kiasi cha kupoteza mwelekeo kisoka hadi anakuwa mzigo katika timu?
Si kunangalia mtu ana misuli, wasifu mzuri- unampa fomu na Mkataba mnono. Huyo wakala ambaye amewaletea Yanga SC Bossou ndiye aliyewaletea Sherman na ndiye ambaye aliwaletea Azam FC mchezaji anaitwa Leonel Saint-Preux.
Leonel alifukuzwa Azam FC ndani ya miezi miwili kutokana na utovu wa nidhamu na kiburi.
Aliwachukua wachezaji wengine wa Azam FC, Kipre Tchetche, Kipre Balou na Didier Kavumbangu akaenda nao kulala nje ya kambi timu ikiwa Kigali, Rwanda kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Waliporudi asubuhi na kuulizwa, yeye aliwajibu kifedhuli viongozi wa Azam FC na timu iliporejea Dar es Salaam akatupiwa virago. Azam FC sasa hawataki kumsikia Giby Kalule wakikumbuka balaa la Leonel.
Hivyo Yanga SC nao hawana sababu ya kuwa na papara ya kusajili wachezaji wa kigeni, kwani usajili muhimu kwao ni wa Desemba, ambao watasajili kikosi cha Ligi ya Mabingwa Afrika.
0 comments:
Post a Comment