// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MSIMBAZI WANAFURAHIA MAMILIONI YA SIMBA DAY, YANGA WANAJUA WENYEWE! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MSIMBAZI WANAFURAHIA MAMILIONI YA SIMBA DAY, YANGA WANAJUA WENYEWE! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, August 12, 2015

    MSIMBAZI WANAFURAHIA MAMILIONI YA SIMBA DAY, YANGA WANAJUA WENYEWE!

    KWA takriban miaka mitano sasa, klabu ya Simba SC imekuwa ikifanya tamasha kubwa la kila mwaka, ambalo hukutanisha malefu ya mashabiki wake Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hilo huwa tamasha maalum kutambulisha kikosi kuelekea msimu mpya na hufanyika wiki ya kwanza ya Agosti kila mwaka.
    Sasa Simba Day limekuwa tamasha maarufu na klabu hiyo imekuwa ikinufaika kwa mamilioni inayokusanya kutokana tu na mapato ya milangoni.
    Sasa Simba SC wanaweza kutengeneza bajeti yao ya msimu, sehemu ya fedha wakitegemea kutoka kwenye Simba Day. Ni ubunifu fulani mzuri ambao klabu imefanya na sasa wanavuna mamilioni ya kutosha kila mwaka.
    Bahati nzuri, hata wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwenye Mkataba wameweka ruzuku ya kufanya tamasha hilo na ninakumbuka wakati fulani ilikuwa ni Sh. Milioni 20, ila kwa sasa sijui na kuna uwezekano dau limepanda.
    Katika Simba Day ya mwaka huu, Simba SC iliendesha kampeni mbili nzuri, kwanza kuuza kadi zake za uanachama na pili ni jezi halali na halisi za klabu.
    Simba SC imetoa jezi ambazo itatumia msimu huu kwa ajili ya mashabiki na Jumamosi iliyopita mashabiki walifanana na wachezaji wa timu yao uwanjani kwa jezi.
    Mwanzoni tu mwa msimu, Simba SC imeuza maelfu ya nakala halisi za jezi zake kwa mashabiki wake- imeingiza fedha za mapato ya mechi na mauzo ya kadi kutokana na Simba Day.
    Simba SC hawajasema wamepata kiasi gani cha fedha kutokana na Simba Day ya mwaka huu, lakini hapana shaka wamevuna mamilioni ya kutosha.
    Wakati huu ukiwa ni mwaka wa tano sasa tangu kuanza kwa Simba Day, watani wao wa jadi, Yanga SC bado wamelala na hawajaonyesha ubunifu wa kujiongezea kipato nje ya udhamini uliojileta wa TBL na kumtegemea Mwenyekiti wao, Yussuf Manji.
    Manji anajitahidi sana kuisaidia Yanga SC kwa fedha za uendeshaji wa timu wa kila siku, ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji ghali, kuajiri makocha Wazungu, kambi za gharama ndani na nje ya nchi hadi Ulaya na hata huduma bora kwa wachezaji na makocha.
    Manji pia analipa mishahara ya watumishi na waajiriwa wote wa klabu kwa ujumla ikiwemo Sekrearieti.
    Lakini pamoja na yote, niseme Yanga SC wamekosa bahati ya kupata viongozi wabunifu, watendaji wazuri na wenye nia ya kuisaidia klabu hiyo.
    Na hii ni kuanzia hao viongozi wa kuchaguliwa hadi wa kuajiriwa. 
    Lakini bahati mbaya watendaji wa kuajiriwa ukiondoa Katibu, Dk. Jonas Tiboroha, wengine kazi zao hazionekani.
    Mfano Meneja Masoko, Omar Kaaya ambaye ana takriban mwaka mzima sasa tangu ameajiriwa na klabu- lakini anachokifanya ni kipi? Anajua mwenyewe.
    Yanga SC haijapata dili jipya la udhamini chini yake. Yanga SC haijaweza kutumia nembo yake kibiashara chini yake. Jezi zote za Yanga SC zinazouzwa mitaani ni feki.
    Na watu wanalazimika kununua jezi feki, kwa sababu hakuna jezi halisi za klabu zilizotangazwa rasmi.
    Simba SC wameweza safari hii, wametengeneza jezi tofauti na zile feki zilizosheheni mitaani kwa miaka sasa na kuzitambulisha rasmi na kuziingiza sokoni.
    Sasa Simba SC wakianza operesheni ya kusaka jezi feki za klabu yao, wataeleweka, kwa sababu kuna jezi halisi za Wekundu hao wa Msimbazi sokoni. Yanga je? Omar Kaaya atatupa jibu.
    Katika Mkataba wa Yanga na TBL kuna fungu lao la kufanya tamasha la kila mwaka kama Simba, lakini hawajawahi kufanya.
    Bila shaka ufadhili wa Mwenyekiti wao, Manji umewalevya Yanga SC na kusahau kuhusu mikakati ya kuifanya klabu ijitegemee, maana hata viongozi wengine, Makamu wa Rais, Clement Sanga na Wajumbe kina Isaac Chanji hatuoni shughuli zao katika klabu.
    Watu wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC ndiyo wa kusimamia shughuli za kiutendaji wa watu waliowaajiri katika klabu, lakini wanaweza kuwalipa mishahara akina Kaaya na wasihoji utendaji wao.
    Imefikia sasa Yanga SC hata tovuti imekufa na pale makao makuu ya klabu kuna Waajiriwa zaidi ya watano akiwemo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Jerry Muro.
    Hili linamuhusu Muro, klabu kubwa kama Yanga SC kukosa tovuti katika dunia ya leo na Kitengo cha Mawasiliano ya Umma ni fedheha. Haya ndiyo mambo ambayo sasa akina Sanga na Chanji wanatakiwa wayasimamie na kuhoji utendaji wa watu wao, kwa sababu tunafahamu Mwenyekiti Manji yeye anatoa fedha tu, hana muda wa kufuatilia utendaji wa kila siku wa waajiriwa wa klabu.
    Ndiyo maana mara kadhaa anapoamua kufuatilia hali ya mambo ndani ya klabu huishia kufukuza watu, kwa sababu anakuja kugundua madudu yaliyolundikana kwa muda mrefu.
    Watu wanapojazana ofisini bila shughuli za kufanya, mwisho wake hugeuka kuwa wapiga majungu tu- kwa sababu vichwa vyao vinakuwa havina mambo mengine ya kufikiria.
    Wenzao Simba SC kwa Simba Day moja tu ya mwishoni mwa wiki wameingiza mamilioni kibao siri yao, lakini wao Yanga, eti wana Meneja Masoko na shughuli anayoifanya haijulikani na akina Sanga, Chanji wanaona poa tu!
    Hii maana yake hata wao nao hawana uchungu na klabu. Hawawezi kuisaidia klabu kupiga hatua yoyote na mwisho wa siku Manji akiondoka Yanga, klabu itarudi kuwa ‘ombaomba’. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSIMBAZI WANAFURAHIA MAMILIONI YA SIMBA DAY, YANGA WANAJUA WENYEWE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top