// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YA KOCHA WA SIMBA NA MAGURI NDIYO MACHUNGU YENYEWE YA SOKA! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YA KOCHA WA SIMBA NA MAGURI NDIYO MACHUNGU YENYEWE YA SOKA! - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, August 16, 2015

    YA KOCHA WA SIMBA NA MAGURI NDIYO MACHUNGU YENYEWE YA SOKA!

    JUMAPILI moja, kiasi cha miaka mitatu iliyopita nilikuwa nimeketi na wachezaji kadhaa wa zamani nchini viwanja vya Leaders Club, Kinodoni mjini Dar es Salaam.
    Pamoja na burudani na viburudisho, lakini mazungumzo yalikuwa yanaendelea kuhusu soka na wanasoka kwa wakati tofauti nchini.
    Ninakumbuka, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa nchini, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ au ‘Bonga Bonga’ alisema maneno ambayo yalikaribia kunitoa machozi.
    Ilikuwa ni katikati ya mjadala wa maisha ya wanasoka wengi baada ya soka na Bonga akasema; “Kama ningejua, ningejibidiisha kwenye shule tu, leo ningekuwa na kazi yangu ninaishi vizuri,”.
    Nilimuelewa Bonga. Alianza kuwika kisoka akiwa kijana wa umri chini ya miaka 20, maana yake alianza kujifunza soka bado mdogo sana. Maana yake hakuwa na muda wa kusoma shule.
    Akafanikiwa kisoka, akacheza klabu kubwa, Yanga SC na timu ya taifa, taifa Stars- lakini bahati mbaya, wakati ambao anacheza, hakukuwa na fedha. Ulikuwa wakati wa soka ya ridhaa.
    Soka ya Ridhaa malipo yake yalikuwa umaarufu na nje ya Uwanja, malipo ya ziada yalikuwa kupata ofa za pombe na wanawake wa ‘bure bure’ wapenda ‘mastaa’.
    Miaka mitano iliyopita, nilifanya mahojiano na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima na nikamuuliza angependa mwanawe naye acheze soka, akasema; “Hapana”.
    Nilipomuuliza kwa sababu gani, akajibu; “Soka ni mchezo wenye machungu mengi sana, nisingependa mwanangu apitie machungu hayo, nataka asome aje kuwa na elimu yake nzuri, aishi furaha na amani,”.
    Sahau kuhusu hayo ya Bonga, soka umeendelea kuwa mchezo wenye changamoto nyingi na machungu pia, hususan kwa huku kwetu Tanzania.
    Huku kwetu ndiko wachezaji wanatolewa ‘kafara’ kuficha mapungufu ya uongozi. Mchezaji anaambiwa amehujumu timu na akafukuzwa bila kupewa haki zake.
    Kidogo kwa mfumo wa sasa, tumeondoka huko. Sasa wakifukuzwa, wenye kuweza kufuatilia haki zao, wanapata.
    Wanasema siri ya mafanikio ni bidii ya mazoezi nidhamu na kujituma- lakini si kila anayefanya hivyo hufanikiwa.
    Kocha mpya wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr amemtema mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Elias Maguri baada ya kumjaribu katika mechi nne akifunga mabao matatu, kwa madai kwamba mchezaji huyo anakosa sana mabao.
    Maguri alifunga bao moja kila mechi katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Black Sailor, 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys na 2-1 dhidi ya Polisi Zanzibar.
    Kerr alimtumia Maguri katika mechi nne kwenye kambi ya visiwani Zanzibar wiki mbili zilizopita na mchezaji huyo akafunga mabao matatu, lakini haikumsaidia kumshawishi Muingereza huyo.
    Kerr akawaambia viongozi wa Simba SC waachane na mchezaji huyo hamuhitaji katika kikosi chake.
    Sababu? Kerr akawaambia viongozi wa Simba SC kwamba mchezaji huyo anapoteza nafasi nyingi za kufunga mabao.
    Na akasema kwamba ana vijana wengi wa kikosi cha vijana, Simba B ambao anaweza kuwatayarisha kuwa washambuliaji wazuri kuliko Maguri.
    Lakini uongozi ukamuambia, mchezaji huyo bado ana Mkataba wa mwaka mzima, hivyo akiachwa klabu italazimika kumlipa- na Kerr akawajibu; “Hata akibaki, hatacheza, atakuwa anafanya mazoezi tu,”.
    Baada ya yote hayo, uongozi wa Simba SC ukakutana na Maguri na kumshauri atafute timu ya kucheza kwa mkopo kwa miezi sita ili kurudisha kiwango chake, labda anaweza kurejeshwa Msimbazi.
    Katika kipindi cha mwaka mmoja cha Maguri kuichezea Simba SC, amefunga mabao 12 katika mechi 43 za mashindano yote, zikiwemo za kirafiki tena nyingi akitokea benchi.
    Simba SC ilimsajili Maguri kutoka Ruvu Shooting baada ya kushika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na wakati huo huo akiwa tayari ameanza kuitwa timu ya taifa, chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen. 
    Kabla ya kumpata Kerr, Simba SC ilijaribu kumchukua Kim, lakini wakashindwana- je kama Mdenmark huyo angetua Msimbazi, leo Maguri angetemwa?
    Jana Tottenham Hotspur ya England imetangaza kumsajili mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Cameroon, Clinton N'Jie kutoka klabu ya Lyon ya Ufaransa kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 10.
    Dogo huyo aliyezaliwa Agosti 15, 1993 alijiunga na Lyon mwaka 2010 kwa msaada wa kaka wa beki wa zamani wa timu hiyo, Jean-Jacques Nono na Novemba 2012 akaichezea mechi ya kwanza Lyon akitokea benchi timu ikishinda 3-0 dhidi ya Reims.
    Lakini ni msimu uliopita ndipo alipong'ara katika klabu hiyo ya Ligi Kuu Ufaransa, maarufu kama Ligue 1, akifunga mabao nane katika mechi 33 za mashindano yote, kati ya hizo 15 tu akianza.
    Huyu dogo wa Cameroon alikaa Lyon miaka miwili kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza- na alipoanza kucheza, katika mechi 33 alifunga mabao nane tu, ila leo ananunuliwa Spurs kwa Pauni Milioni 10.
    Nimesema, si kwenye juhudi za mazoezi, nidhamu na kujituma hufanikiwa hata kama ana kipaji- kwani sifa zote hizo unazipata kwa Maguri, ila leo anafukuzwa Simba SC.
    Ninamuheshimu Kerr, lakini pia ninamuhesimu Kim. Na pia ninamuheshimu kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Tom Olaba aliyempa nafasi Maguri Ruvu Shooting hadi akawa mfungaji bora namba tatu katika Ligi Kuu, kiasi cha Simba kumpenda na kumsajili.
    Maamuzi ya Kerr, tufunike kombe ‘mwanaharam’ apite. Pole yake Elias Maguri. Hayo ndiyo machungu ya soka. Akubali matokeo, ajipange upya. Akacheze sehemu nyingine na Mungu anaweza kumjaalia akaibuka tena na kutimiza ndoto zake. Jumapili njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YA KOCHA WA SIMBA NA MAGURI NDIYO MACHUNGU YENYEWE YA SOKA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top