// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); STARS IENDE UTURUKI KUFANYA NINI NA NIGERIA TUNACHEZA NAO NYUMBANI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE STARS IENDE UTURUKI KUFANYA NINI NA NIGERIA TUNACHEZA NAO NYUMBANI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, July 15, 2015

    STARS IENDE UTURUKI KUFANYA NINI NA NIGERIA TUNACHEZA NAO NYUMBANI?

    SEPTEMBA 5, mwaka huu timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza na Nigeria katika mchezo wa kundi G kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mjini Dar es Salaam.
    Huo utakuwa mchezo wa pili kwa kampeni za kuwania tiketi ya AFCON ya Gabon mwaka 2017, baada ya Juni 14 kufungwa mabao 3-0 na Misri mjini Alexandria. 
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo katika mkakati wa maandalizi ya safari ya kambi nchini Uturuki kujiandaa na mtihani dhidi ya Nigeria.
    Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi anahaha kuhakikisha zinapatikana fedha za kuipeleka timu Uturuki kwa kambi japo ya wiki mbili.
    Na Stars inatarajiwa kwenda Uturuki baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki Dar es Salaam.
    Kambi ya Uturuki ni mapendekezo ya Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ ambaye amerithi mikoba ya Mholanzi Mart Nooij aliyefukuzwa kazi mwishoni mwa mwezi uliopita kutokana na matokeo mabaya, ikiwemo kufungwa mechi tano mfululizo.
    Na Mshauri wa Ufundi wa Stars, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ naye amekaririwa na vyombo vya Habari akisistiza juu ya kambi ya Uturuki, kwamba itasaidia mno kwa maandalizi.
    Na kwa TFF hilo linawezekana kutokana na jitihada za Malinzi- ambaye anaonekana kabisa anafanya kazi kwa ajili ya ustawi wa soka ya Tanzania. Inaonekana kabisa Malinzi ana dhamira ya kuipeleka katika anga nzuri soka ya nchi yetu. 
    Kwani hata kabla ya mchezo dhidi ya Misri, Stars ambayo iliweka kambi ya wiki moja Addis Ababa- na tutarajie mfumo wa kambi za nje (kama haya yataendelea kuwa mawazo ya makocha), utaendelea hata kwa mchezo wa tatu dhdi ya Chad Machi 25 mwakani.
    Kwa sababu Malinzi ana kiu kubwa ya kuirejesha Tanzania kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika, ambazo mara ya kwanza na ya mwisho ilicheza mwaka 1980- na ndiyo maana amekuwa akihakikisha maandalizi yanakuwa mazuri.
    Sitaki kupingana na mawazo ya makocha, chini ya Mshauri wao wa Ufundi, lakini nataka niwasilishe tu mawazo yangu kwa TFF na benchi zima la Ufundi la Stars.
    Tutacheza na Nigeria nyumbani mapema Septemba kwenye hali ya joto, kwa nini twende kuweka kambi Uturuki kwenye baridi na mazingira tofauti kwa ujumla?
    Kambi ya nje inafaa kama timu inajiandaa kwa mchezo wa nje- lakini kwa mechi za hapa, nadhani ni bora kutafuta sehemu yoyote katika nchi yetu iliyo tulivu ambayo wachezaji watapata fursa nzuri ya maandalizi.
    Mwaka 2006, Taifa Stars ilipokuwa chini ya kocha Mbrazil, iliwahi kuweka kambi katika hosteli za mgodi wa Barrick Gold Mining, Bulyanhulu mkoani Shinyanga na ikaanza vizuri kampeni za AFCON ya 2008 kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Burkina Faso.
    Haukuwa ushindi tu, bali kwa tuliokuwepo tulishuhudia vijana wakicheza soka maridadi mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
    Na bado maeneo kama Barrick yenye utulivu na faragha nzuri yapo mengi hapa nyumbani Tanzania, ambako Taifa Stars inaweza kuweka kambi ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Nigeria.
    Narudia kusema sipingani na mawazo ya makocha au benchi la Ufundi la Stars kwa ujumla, bali najaribu kuwasilisha mawazo yangu kwao kwa manufaa ya timu yetu.
    Hizo fedha ambazo wanataka kutumia kwa kambi ya Uturuki zitatusaidia mno wakati wa mechi za ugenini dhidi ya Nigeria na Chad.
    Ni bora tutafute kambi tulivu nje ya Dar es Salaam na Pwani kwa ujumla- mathalani Bara huko, timu ikafanye maandalizi ya mchezo dhidi ya Nigeria. Hayo ni maoni yangu tu, bado wakubwa wanaweza kuamua kilicho bora kwa mitazamo yao. Ramadhan Njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS IENDE UTURUKI KUFANYA NINI NA NIGERIA TUNACHEZA NAO NYUMBANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top