HATIMAYE mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Allan Wetende Wanga amesaini Mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Azam FC, akitokea El Merreikh ya Sudan.
Usajili wa Wanga, aliyesaini leo makao makuu wa klabu barabara ya Nyerere, Dar es Salaam unakamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni Azam FC kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Wengine ni Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ kutoka APR ya Rwanda na Serge Wawa Pascal, Kipre Michael Balou, Kipre Tchetche wote wa Ivory Coast, Brian Majwega wa Uganda na Didier Kavumbangu wa Burundi, ambao wote walikuwepo tangu msimu uliopita.
Awali, kulikuwa kuna mvutano baina ya pande hizo mbili, mchezaji akitaka kusaini miezi sita na klabu ikitaka angalau asaini mwaka mmoja- mwishowe makubaliano yamefikiwa.
Wanga aliyezaliwa Novemba 26, mwaka 1985 mjini Kisumu, Kenya pamoja na kusaini Azam FC, lakini ndoto zake bado ni kucheza Ulaya.
Allan Wanga (kushoto) akibalishana Mikataba na Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad kulia |
Allan Wanga kushoto akisaini Mkataba na Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad leo mjini Dar es Salaam |
Hata hivyio, Wanga aliyemaliza Mkataba wake wa mwaka mmoja Merreikh Juni mwaka huu, hatacheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la kagame kwa sababu hakuingizwa kwenye orodha ya wachezaji 20 wa Azam FC kwa ajili ya michuano hiyo.
Katika soka, Wanga amefuata nyayo za baba yake, Frank Wetende, aliyewahi kuchezea AFC Leopards na Posta ya Kisumu pamoja na timu ya taifa ya Kenya miaka ya 1970 na 1980.
Mume huyo wa mtangazaji wa Televisheni ya Kenya, Brenda Mulinya aliibukia katika klabu ya Lolwe mwaka 2005, kabla ya kujiunga na Tusker mwaka Tusker, baadaye Petro Atletico mwaka 2008, FK Baku mwaka 2010, Hoang Anh Gia Lai mwaka 2011.
Mwaka 2012 baada ya kumaliza Mkataba wake Hoang Anh Gia Lai alirejea Kenya kutimiza ndoto za kuchezea timu ya baba yake AFC Leopards, kabla ya kusaini El-Merreikh mwaka 2014.
Leo ameandika historia mpya katika maisha yake baada ya kusaini timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, Azam FC.
0 comments:
Post a Comment