Wachezaji wa Uganda wakicheza staili ya Korongo kushangilia bao lao la tatu lililofungwa na Farouk Miya wa pili kulia |
MABAO mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu yanaweza kuwa yamehitimisha historia ya kocha Mholanzi, Mart Nooij katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars baada ya kufungwa 3-0 na Uganda usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Mchezo huo wa kwanza Raundi ya Kwanza kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Rwanda mwaka 2016, Sekisambu alimtungua kipa Deo Munishi ‘Dida’ bao moja kila kipindi, wakati bao la tatu lilifungwa na Farouk Miya dakika ya 89.
Tanzania sasa inatakiwa kwenda kushinda mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo ili kusonga mbele Raundi ya Kwanza.
Matokeo hayo yanawakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono la Sh. Milioni 1 kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi jana.
Erisa Sekisambu, mfungaji wa mabao mawili ya Uganda katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Tanzania |
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Taifa Stars walicheza vizuri kwa dakika 15 tu za mwanzo, baada ya hapo, Waganda wakaanza kujibu mashambulizi.
Hali ikawa mbaya baada ya Sekisambu kuifungia Uganda bao la kwanza dakika ya 38, akimalizia mpira uliookolewa na kipa Dida kufuatia shuti la Robert Ssentongo.
Simon Msuva alipewa pasi nzuri na Frank Domayo dakika ya 42, lakini akapiga nje.
Kipindi cha pili, Taifa Stars walirudi kichovu zaidi na kuwapa fursa Waganda kutawala mchezo hatimaye kupata mabao mawili zaidi.
Sekisambu alianza kufunga dakika ya na 63 baada ya kumtoka Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kumtungua kwa shuti Dida.
Farouk Miya akafunga bao ka tatu kwa penalti dakika ya 89, baada ya Shomary Kapombe kumkwatua kwenye boksi Frank Kalanda.
Kikosi cha Tanzania; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Abdi Banda, Frank Domayo/Rashid Mandawa dk83, Amri Kiemba/Said Ndemla dk57, Kevin Friday/John Bocco dk58 na Simon Msuva.
Uganda; Alitho James, Brian Ochwo, Dennis Okoth, Muzamiru Mutyaba, Derric Tekkwo, Hassan Wasswa, Bakari Shafiq, Robert Ssentongo/Frank Kalanda dk68, Farouk Miya, John Somazi/Yasser Mugerwa dk55 na Erisa Sekisambu/Kizito Kezron dk81.
0 comments:
Post a Comment