ARGENTINA ya Lionel Messi itamenyana na Colombia ya Radamel Falcao katika Robo Fainali ya Copa America Ijumaa wiki hii nchini Chile.
Wenyeji Chile watamenyana na Uruguay katika Robo Fainali ya kwanza Jumatano wakati Alhamisi,
Bolivia watamenyana na Peru.
Robo Fainali ya mwisho itachezwa Jumamosi kati ya Brazil na Paraguay. Brazil imetinga Robo Fainali kwa wa mabao 2-1 dhidi ya Venezuela usiku wa kuamkia leo.
Radamel Falcao ameshindwa kufurukuta mechi zote za makundi, je ataweza kuibeba Colombia mbele ya Argentina? Hapa ni wakati anatolewa na kocha wake, Jose Pekerman dakika ya 65 jana katika mchezo dhidi ya Peru
Ikicheza bila ya nyota tegemeo lake, Neymar aliyefungiwa mechi nne kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha katika mchezo dhidi ya Colombia, Brazil ilipata mabao yake kupitia kwa Thiago Silva dakika ya tisa na Roberto Firmino dakika ya 51.
Fedor ndiye mfungaji wa bao pekee la Venezuela, aliyemtungua kipa Jefferson zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika.
Colombia imelazimishwa sare ya 0-0 na Peru, huku mshambuliaji Radamel Falcao akitolewa uwanjani dakika ya 65 baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya ukuta wa Peru.
Sare hiyo inazifanya timu zote hizo zimalize mechi za Kundi C na pointi nne kila moja na Peru inakwenda Robo Fainali moja kwa moja kama mshindi wa pili nyuma ya Brazil.
Sare hiyo pia inaitupa nje ya michuano hiyo Ecuador iliyokuwa Kundi A, ambayo imemaliza na wastani mbaya zaidi kati ya washindi wa tatu wa makundi yote.
0 comments:
Post a Comment