// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HATUELEWANI, KOCHA HAWATAKI WAANDISHI, WACHEZAJI WANAPIGANA NA MASHABIKI, MALINZI ANAWEKA MILIONI 21, NA SISI JE? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HATUELEWANI, KOCHA HAWATAKI WAANDISHI, WACHEZAJI WANAPIGANA NA MASHABIKI, MALINZI ANAWEKA MILIONI 21, NA SISI JE? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, June 20, 2015

    HATUELEWANI, KOCHA HAWATAKI WAANDISHI, WACHEZAJI WANAPIGANA NA MASHABIKI, MALINZI ANAWEKA MILIONI 21, NA SISI JE?

    Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
    HATIMA ya kocha Mholanzi, Mart Nooij kuendelea kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars itajulikana usiku wa leo baada ya mchezo dhidi ya Uganda Uwanja wa Amaan mjini hapa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2016 nchini Rwanda.
    Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Uganda ‘The Cranes’ usiku wa leo Uwanja wa Amaan visiwani hapa katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo ya CHAN, inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Kampala.
    Nooij ameiongoza Taifa Stars katika mechi nane bila ya ushindi, kati ya hizo ikifungwa nne mfululizo, tatu Kombe la COSAFA Afrika Kusini na nyingine wiki iliyopita dhidi ya Misri kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017. 
    Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 17 tangu arithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu, sare sita na kufungwa nane- akifunga mabao 17 na kufungwa 25.
    Hali ni mbaya Taifa Stars, imefikia basi la wachezaji linatupiwa mawe likikatiza mitaani na wananchi wanamalizia jazba zao kutukana viongozi na wachezaji kwenye mitandao ya kijamii.
    Taifa Stars watajaribu kusaka ushindi wa kwanza leo baada ya mechi nane 

    Awali walikuwa hawataki kabisa kusikia kuhusu kocha Nooij, wakiamini yeye ndiye tatizo- lakini baada ya mchezo na Misri wamewageuzia kibao na wachezaji- wanawapiga mawe na kuvunja vioo vya basi lao.
    Jana, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alilazimika kuwaahidi Sh. Milioni 1 kila mchezaji iwapo watashinda mchezo wa leo, ili kuwatia hamasa- na akasema kabisa hali ni mbaya.
    Malinzi aliwafuata wachezaji mazoezini jioni ya jana Uwanja wa Amaan na akawaambia, iwapo watashinda, mbali na posho za kawaida za kambi, atawapa Milioni 1 kila mmoja.
    “Watu wanataka ushindi, matusi yote kwa TFF, huyo Malinzi anatukanwa kila sehemu. Nyinyi wenyewe mnatukanwa, mnapigwa mawe. Kwa kweli hali ni mbaya. TFF tumejitahidi kuwafanyia kila kinachostahili na tutaendelea kuwafanyia, ni jukumu letu na hakuna siku tumewanyima, tungekuwa na posho zaidi, tungewapa,”alisema Malinzi na kuongeza;
    “Lakini sisi tunafanya mambo yetu nje ya Uwanja, mkikanyaga uwanjani ni nyinyi, Bocco...kapaisha, Ndemla kapigwa chenga...kesho (leo) ni vita kubwa haijawahi kuonekana, Waganda mnawajua, Cannavaro mjitahidi kukimbizana nao, msicheze kama mpo ugenini, pambaneni kwa kujiamini, mpo nyumbani.”alisema.
    Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimtia moyo Malinzi kwa kusema kwamba watajitahidi kulipigania taifa na kwamba wako tayari kwa mpambano.
    Jumla ya wachezaji 21 wapo kambini Zanzibar hoteli ya Nungwi Inn na maana yake bila kuhusisha watu saba wa benchi la ufundi, Malinzi atalazimika kutoa Sh. Milioni 21 iwapo Stars itashinda leo.
    Wachezaji waliopo kambini ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Mwadini Ali, mabeki; Mwinyi Haji Mngwali, Hassan Isihaka, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Viungo ni; Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Abdi Banda, Frank Domayo, Amri Kiemba, Said Ndemla, Hassan Dilunga na Kelvin Friday wakati washambuliaji ni; Atupele Green, Rashid Mandawa, Simon Msuva na John Bocco.
    Ahadi ya Malinzi wazi inaashiria anataka kurejesha amani katika timu- kwani Stars ikishinda leo hali itatulia na kelele zitasimama, hivyo timu kujipanga vizuri zaidi kwa mitihani inayofuata.
    Mungu ibariki timu yetu ya taifa, Taifa Stars iweze kuibuka na ushindi mzuri leo ili amani irejee katioka soka ya Tanzania. Amin.

    Septemba tutakuwa wenyeji wa Nigeria kufuzu AFCON, lakini mapema mwezi ujao tunakwenda kurudiana na Uganda mjini Kampala. Tunawania tiketi za CHAN na AFCON kwa wakati huu.
    Hakutakuwa na Mrisho Ngassa kikosini, ambaye CAF imemzuia baada ya kusaini Mkataba na Free State Stars ya Afrika Kusini, maana yake katika safu ya ushambuliaji, Taifa Stars itawategemea John Bocco, Simon Msuva, Ibrahim Hajib na labda Atupele Green na Rashid Mandawa.
    Katika siku za karibuni Taifa Stars imekuwa na makosa mengi kwenye safu ya ulinzi na kipa Deo Munishi ‘Dida’ amekuwa akiokoa michomo ya hatari mno, lakini baadaye anafungwa mabao rahisi.
    Oscar Joshua ni mchezaji ambaye amekuwa akipoteza hali ya kujiamini kila kukicha kutokana na kusakamwa na mashabiki kwa sababu huonekana kama mabao ambayo timu inafungwa yanapitia kwake.
    Lakini wakati mwingine Oscar anaonewa tu- kwani makosa ya kiungo anayecheza juu yake au kiungo wa ulinzi hata mabeki wa kati bado lawama zimekuwa za Joshua.
    Kwa ujumla morali kwa wachezaji wa Taifa Stars imepungua kwa kiasi kikubwa tangu timu itolewe na Msumbiji kwa ‘mizengwe’ ya marefa wa Uganda mwaka jana.
    Na utaona tangu hapo, Stars imeshinda mechi moja tu dhidi ya Benin 4-1 ikitoka kufungwa tena 2-0 na Burundi kabla ya kucheza mechi nane bila kushinda hata moja, ikifungwa nne mfululizo.
    Tumeporomoka na tumevurugana. Hatuelewani. Kocha Nooij anamkunjia sura kila mwandishi wa Habari. Wachezaji nao wanapigana na mashabiki.
    Wachezaji wengine wanawapiga mikwara hadi Waandishi eti watawapiga kwa sababu wanaandika timu haifanyi vizuri. Inachekesha, lakini ndiyo hali halisi. Hali ni mbaya.
    Ni hali ambayo hutokea na imekwishazitokea nchi nyingine kubwa tu- Ufaransa, Hispania, Brazil hata Ujerumani na Italia wamekwishaogelea kwenye wimbi la matokeo mabovu ya kustaajabisha bila sababu. 
    Kocha mzuri, wachezaji wazuri, huduma nzuri- lakini timu inafungwa na timu ambazo huwezi kuamini. 
    Ufaransa wakiwa mabingwa wa Kombe la Dunia na wenye timu bora yenye wachezaji bora kama aliyekuwa Mwanasoka Bora wa Dunia, Zinadine Zidane ilifungwa na Senegal katika Kombe la Dunia 2002 na kuvuliwa ubingwa mapema tu.
    Juzi tu hapa, Hispania ilivurunda katika Kombe la Dunia na kuvuliwa taji hilo kwa kutolewa mapema- ndani yake ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji walioipa Real Madrid ubingwa wa Ulaya. Sehemu kubwa ya wachezaji walioshindwa kuisaidia Hispania katika Kombe la Dunia mwaka jana, mwaka huu tena wameipa Barcelona taji la Ulaya.
    Ipe heshima yake soka na Watanzania wote leo tuunganishe nguvu zetu kuisapoti timu yetu ya taifa, ili izinduke kutoka katika lepe la usingizi mzito wa matokeo mabaya ya mechi nane mfululizo bila ushindi.
    Siyo timu ya Malinzi. Si timu ya Nooij. Ni timu ya taifa ya Tanzania inayoundwa na wachezaji wa Tanzania. Malinzi ameahidi Sh. Milioni 21 timu ikishinda, itakuwa vyema nasi wananchi tukiondoa chuki na kurejesha sapoti yetu kwa timu kwa asilimia 100. Mungu ibariki Tanzania, ibariki Taifa Stars. Amin.   
    Malinzi (kushoto) ameahidi Sh. Milioni 21 timu ikishinda leo. Kocha Nooij kulia hana raha Taifa Stars baada ya kufungwa mechi nne mfululizo 

    REKODI YA MART NOOIJ TAIFA STARS
    P W D L GS GC
    17 3 6 8 17 25

    Tanzania 0-0 Malawi (Kirafiki Mbeya)
    Tanzania 1-0 Zimbabwe (kufuzu AFCON Dar es Salaam)
    Tanzania 1-0 Malawi (kirafiki Taifa)
    Tanzania 2-2 Zimbabwe (Kufuzu AFCON Harare)
    Tanzania 2-4 Botswana (kirafiki Harare)
    Tanzania 2-2 Msumbiji (Kufuzu AFCON Dar es Salaam)
    Tanzania 1-2 Msumbiji (Kufuzu AFCON Maputo)
    Tanzania 0-2 Burundi (Kirafiki, Bujumbura)
    Tanzania 4-1 Benin (Kirafiki, Dar es Salaam)
    Tanzania 1-1 Swaziland (Kirafiki, Mbabane)
    Tanzania 1-2 Burundi (Kirafiki, Taifa. Stars Maboresho)
    Tanzania 1-1 Rwanda (kirafiki Mwanza, Maboresho)
    Tanzania 1-1 Malawi (Kirafiki Mwanza, Stars kubwa)
    Tanzania 0-1 Swaziland (COSAFA Rustenburg)
    Tanzania 0-2 Madagascar (COSAFA Rustenburg)
    Tanzania 0-1 Lesotho (COSAFA Rustenburg)
    Tanzania 0-3 Misri (Kufuzu AFCON Alexandria)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATUELEWANI, KOCHA HAWATAKI WAANDISHI, WACHEZAJI WANAPIGANA NA MASHABIKI, MALINZI ANAWEKA MILIONI 21, NA SISI JE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top