Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ta Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij amefanya mabadiliko madogo katika kikosi chake kilichofungwa na Swaziland mchezo wa kwanza Kombe la COSAFA juzi mjini hapa.
Kuelekea mchezo wa leo jioni dhidi ya Madagascar, Nooij amewaondoa wachezaji wawili, beki Shomary Kapombe na winga Simon Msuva ambao wote walianza mchezo na Swaziland ikilala 1-0.
Erasto Nyoni aliyecheza kama kiungo wa ulinzi siku hiyo, leo atacheza beki ya kulia, Oscar Joshua ataendelea kucheza beki ya kushoto wakati katikati wanarudia Salim Mbonde na Aggrey Morris.
Shomary Kapombe (kushoto) anaanzia benchi leo. Kulia ni Mwinyi Kazimoto anaanza katikati ya Uwanja |
Salum Abubakar 'Sure Boy' kulia anaanza leo. Kushoto Abdi Banda ataendelea kusugua benchi |
Langoni ameanza Deo Munishi ‘Dida’ wakati viungo ni Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Said Hamisi Ndemla, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco, Mrisho Ngassa na Juma Luizio. Sure Boy na Luizio wote walitokea benchi Jumatatu.
Taifa Stars inahitaji kushinda mchezo huo wa pili wa Kundi B utakaoanza Saa 11:00 jioni Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace ili kufufua matumaini ya kwenda Robo Fainali.
Lakini Stars pamoja na kupigania ushindi, itabidi iiombee dua mbaya, Swaziland nayo ipoteze mechi mbele ya Lesotho ili timu timu zote katika kundi ziwe sawa kwa pointi na mechi za mwisho Ijumaa ziamue kinara wa Kundi B.
Tanzania ilifungwa 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza, wakati Madagascar ilishinda 2-1 dhidi ya Lesotho jana.
Michuano hiyo ya 15 itashirikisha timu 14, zikiwemo mbili, Tanzania na Ghana wageni waalikwa. Timu nyingine ni Mauritius, Shelisheli,
Swaziland, Madagascar, Zimbabwe, Namibia,
Lesotho , Botswana, Malawi, Msumbiji, Zambia na wenyeji Afrika Kusini.
Juma Luizio (kulia) anaanza leo, wakati Hassan Dilunga ataendelea kusubiri benchi |
Beki tegemeo la kocha Nooij, Oscar Joshua ataendelea kuanza upande wa kushoto |
Kundi A lina timu za Namibia, Mauritius, Shelisheli na Zimbabwe, wakati Kundi B lina timu za Lesotho, Madagascar, Swaziland na Tanzania.
Mshindi wa kila kundi ataungana na wenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Ghana, Botswana na Malawi kucheza Robo Fainali.
Kutakuwa na Nusu Fainali za aina mbili, kwanza za timu zilizofungwa katika Robo Fainali (Plate Semi Finas) na zilizoshinda (Semis Finals).
Vibonde wataendelea kupepetana hadi fainali yao ambayo itapigwa Mei 29, wakati fainali ya wakali itakuwa Mei 30. Kila la heri Taifa Stars.
0 comments:
Post a Comment