Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KIPA ‘bwana mdogo’ Peter Manyika Jr. jana amedaka mechi ya 20 msimu huu katika klabu yake, Simba SC jambo ambalo ni kinyume kabisa cha matarajio.
Simba SC imeshinda 2-1 dhidi ya wenyeji wa kuhamia, Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Manyika alisajiliwa kama kipa wa tatu Simba SC, tena akiorodheshwa kwenye kikosi cha vijana, ‘Simba B’, lakini akalazimika kuanza kazi mapema baada ya makipa wote wa juu yake kuwa majeruhi.
![]() |
Peter Manyika Jr. jana amedaka mechi ya 20 Simba SC, akifungwa bao la 14 |
Septemba mwaka jana Simba SC ilikwenda Afrika Kusini na makipa wawili, Hussein Sharrif ‘Casillas’ na Manyika kutokana na Ivo Mapunda kuumia kidole.
Lakini kwa bahati mbaya zaidi, Casillas naye akaumia ugoko akiidakia timu hiyo mchezo wa kirafiki dhidi ya Orlando Pirates, hivyo Manyika kuingia dakika ya 43 kumalizia mchezo.
Casillas hajaweza kurejea langoni tangu hapo na Manyika amekuwa akipokezana na Ivo kudaka, jana akifikisha mechi 20, akiwa amefungwa mabao 14 tu katika mechi zote hizo.
Tayari Manyika ni kipa wa kuaminiwa Simba SC licha ya umri wake mdogo- jambo ambalo linamtengenezea mazingira mazuri ya kuwa kipa bora baadaye.
Manyika ambaye amerithi kazi hiyo kutoka kwa baba yake mzazi, Manyika Peter Sr., anaelekea kufuata vyema nyayo za mzazi wake huyo, kwani tayari amepandishwa kikosi cha timu ya pili ya taifa, maarufu kama Taifa Stars Maboresho ambako alisimama langoni kwa dakika zote 90 katika sare ya 1-1 na Rwanda Januari 22, mwaka huu.
Manyika Sr aliwika katika klabu za Mtibwa Sugar, Yanga SC na timu ya taifa, Taifa Stars kabla ya kustaafu na kuwa kocha wa makipa, huku pia akifanya muziki.
Wakati Manyika Jr. amedaka mechi 20 katika msimu wake wa kwanza Simba SC na kufungwa mabao 14, Ivo ambaye anamaliza Mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu Juni mwaka juu, tangu atue Msimbazi Desemba mwaka juzi, amedaka mechi 36 na kufungwa mabao 24.
Casillas naye ambaye amesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar, yeye hadi anaumia Oktoba mwaka jana alikuwa amedaka mechi nane na kufungwa mabao manne.
0 comments:
Post a Comment