• HABARI MPYA

        Tuesday, March 31, 2015

        HAROUN CHANONGO KUTUA TOTO AFRICANS

        Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
        WINGA wa Simba SC, Haroun Chanongo anayecheza kwa mkopo Stand United ya Shinyanga, yuko mbioni kutua Toto Africans iliyorejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
        Tayari Simba SC imekwishasema haimhitaji tena Chanongo na ilimtoa kwa mkopo Stand United katika dirisha dogo Desemba akamalizie Mkataba wake.
        Kocha Mkuu wa Toto, John Tegete ameiambia BIN ZUBEIRY jana mjini hapa kwamba, wamekwishafanya mazungumzo na Chanongo na kufikia makubaliano msimu ujao atatua Kishamapanda.
        “Tumezungumza na Chanongo, kimsingi tumefikia makubaliano msimu ujao atakuwa mchezaji wetu. Ni mchezaji mzuri ambaye tunaamini atatusaidia sana,”amesema baba huyo wa mshambuliaji wa Yanga SC, Jerry Tegete.
        Haroun Chanongo yuko njiani kutua Toto Africans ya Mwanza

        Lakini wakati Tegete anasema Chanongo yuko mbioni kutua kwao, tayari kuna habari kwamba mchezaji huyo yupo pia kwenye rada za Yanga SC.
        Simba SC ilimsimamisha Chanongo Novemba mwaka jana kwa madai eti amekuwa akicheza chini ya kiwango katika klabu hiyo kabla ya kumtoa kwa mkopo klabu ya Shinyanga.
        Na ilifikia hatua hiyo kwa Chanongo pamoja na mchezaji mwingine, kiungo Amri Kiemba ambaye yeye alichukuliwa kwa mkopo Azam FC, kwa mpango ule ule, akamalizie mkataba wake hadi mwisho wa msimu na hahitajiki tena Msimbazi. 
        • Blogger Comments
        • Facebook Comments

        0 comments:

        Item Reviewed: HAROUN CHANONGO KUTUA TOTO AFRICANS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry