Felician amesema Sherman ameshuka kiwango baada ya muda mfuoi wa kuwa Yanga SC |
BEKI wa zamani wa Toto African na Pamba za Mwanza, Francis ‘Fura’ Felician amesema kiwango cha mshambuliaji Mliberia wa Yanga SC, Kpah Sherman kinaanza kushuka, tofauti na alivyokuja nchini kuashiria kwamba hana matunzo mazuri.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Mwanza jana, mdogo huyo wa mshambuliaji wa zamani wa Pamba na Yanga, Fumo Felician alisema kwamba kuna hatari soka ya Sherman ikafia Jangwani, iwapo hawatashituka.
“Kpah Sherman ninavyomuona anajua mpira, ila nahisi hana matunzo mazuri baada ya kutua Yanga, kwa sababu kiwango chake kinashuka siku hadi siku, tofauti na alivyokuja alikuwa mzuri sana na mwenye nguvu, lakini sasa anaanza kuwa mwepesi na uwezo unapungua,”alisema Felician.
Kocha huyo wa akademi mjini Mwanza, amesema uongozi wa Yanga SC unapaswa kufuatilia mwenendo wa mchezaji huyo baada ya kuhamishia maisha yake Dar es Salaam na kuzungumza naye kwa kina juu ya anachokosa kwa sasa, ili waweke mambo sawa aweze kuisaidia timu.
Kpah Sherman kushoto amepangiwa nyumba Mtaa wa Kongo, Kariakoo, Dar es Salaam |
“Mimi sijui, nasikia wamempangia nyumba Kariakoo, kule karibu na klabu (Jangwani). Kule si sehemu ya kuishi mchezaji kama yule. Lazima tu ataua kiwango chake, starehe nyingi kule,”.
“Kwa uwezo alioingia nao Sherman Yanga SC lazima alikuwa anafanya mazoezi ya gym na nini, sasa sidhani kama hapo walipomuweka anapata nafasi ya mazoezi ya gym. Basi tena, ndiyo wanamuua,”amesema.
Aidha, akizungumzia matokeo ya jana ya Yanga SC kutoa sare ya 0-0 na Ndanda FC, Felician amesema kwamba washambuliaji wanaiangusha timu, kwa sababu hawana njaa ya mabao.
“Jinsi wanavyoanza mpira polepole kama wameshapata bao, wanakuja kuanza kucheza kwa bidii mwishoni mwa mchezo, wanakosea. Biashara asubuhi, jioni mahesabu,”amesema.
Felician amesema tatizo wachezaji wa Tanzania hawajitambui na akamtolea mfano mshambuliaji Mganda wa Simba SC, Emmanuel Okwi kwamba anajitambua na anajua wajibu wake.
“Okwi anajitambua na anajua Simba wanamtegemea na Yanga hawamtakii mema, hivyo anafanya kazi unamuona yuko kwenye pilika uwanjani, lakini washambuliaji wa Yanga wanatembea tu uwanjani. Kidogo namuona Tambwe (Amisi) anafanya pilika,”amesema.
0 comments:
Post a Comment