Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
AZAM FC kesho watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mchezo ambao utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi wa Jumapili umeipeleka kileleni Yanga SC baada ya kufikisha pointi 25 kutokana na mechi 13, ikiishushia nafasi ya pili Azam yenye pointi 22 za mechi 12.
Azam FC imecheza mechi tano bila kushinda, tangu iliposhinda mara ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar mabao 3-1 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Januari 20, mwaka huu.
Baada ya ushindi huo uliotokana na mabao ya mawili Mrundi Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche wa Ivory Coast, Azam FC ilitoa sare ya 1-1 na Simba SC.
Kutoka hapo, ikachukua mapumziko ya wiki moja katika Ligi Kuu ili kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa michezo ya kirafiki kujiandaa na mchezo wa kwanza Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya El Merreikh mwishoni mwa wiki.
Wakiwa Lubumbashi, Azam FC walifungwa mechi mbili 1-0 mara zote dhidi ya wenyeji TP Mazembe na Don Bosco ya Kinshasa, wakati mchezo mwingine walitoa sare ya 2-2 na ZESCO United ya Zambia, mabao yao yote yakifungwa na kiungo Frank Domayo.
Waliporejea kutoka Lubumbashi, mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu, walitoa sare ya 2-2 na wenyeji Polisi Jumamosi mjini Morogoro na sasa kesho, kocha Mcameroon Joseph Marius Omog atakuwa anawania ushindi wa kwanza baada ya mechi tano.
Mara ya mwisho, timu hizo zilikutana katika Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwezi uliopita na Mtibwa Sugar ikashinda kwa penalti 7-6 katika Robo Fainali baada ya sare ya 1-1.
0 comments:
Post a Comment