Rashid Mandawa anamfukuzia kwa mabao Didier Kavumbangu |
MBIO za kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, zimezidi kunoga ambapo kwa sasa Rashid Mandawa wa Kagera Sugar na Simon Msuva wa Yanga wanamfukuza kwa kasi ya ajabu Didier Kavumbagu anayeongoza mbio hizo.
Kavumbagu hadi sasa ameshafunga mabao nane, wakati Mandawa na Msuva kila mmoja amecheka na nyavu mara saba, hivyo kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kumpiku Mrundi huyo.
Kwa misimu miwili iliyopita, tuzo hiyo imekuwa ikichukuliwa na wachezaji wa kigeni, Kavumbagu akitaka kuendeleza wimbi hilo msimu huu.
Msimu wa 2012/13, tuzo hiyo ilichukuliwa na Muivory Coast Kipre Tchetche aliyeipora kutoka kwa mzawa John Bocco na msimu uliofuata, 2013/14, Amissi Tambwe wakati huo akiwa Simba (sasa Yanga), ndiye aliyeibuka kidedea.
Na kutokana na kasi ya Mandawa pamoja na Msuva, kuna uwezekano mkubwa wa kutwaa tuzo hiyo msimu huu, lakini iwapo Kavumbagu ambaye ameonekana kutokuwa na mzaha katika kucheak na nyavu, atateleza.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Madawa alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha anasaidia timu yake hiyo kufanya vizuri katika ligi pamoja na kuibuka mfungaji bora.
“sitaki kusema mengi lengo langu ni kuhakikisha nasaidia timu yangu inafanya vizuri huku nikiwanyamazisha wale wanaopenda kuzungumza,” alisema.
0 comments:
Post a Comment