Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
KOCHA wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic leo alikuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya Yanga SC ya Dar es Salaam.
Yanga SC ilishinda 1-0, bao pekee la Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ na Simba SC ndiyo wapinzani wafuatao wa Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani.
Kocha wa Simba SC, Goran Kopunovic akiwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga leo kuwaangalia Coastal Union wakimenyana na Yanga SC
Na kwa sababu hiyo, Kopunovic alihitaji kuwajua wapinzani wake kabla ya kukutana nao Jumamosi na alifika uwanjani mapema tu leo hata kabla timu hazijaingia kupasha misuli moto.
Lakini Goran hakutaka kuonekana na wengi kama yupo Mkwakwani, kwani ‘alijibanza’ nyuma ya wazee wawili, akawa anachungulia kwa ‘kuibia ibia’ huku akiandika taarifa alizohitaji.
Koponuvic anaonekana kupania kuchukua pointi tatu Uwanja wa Mkwakwani Jumamosi na kikosi chake kilitarajiwa kuwasili leo Tanga, ili kesho kianze kujifua mjini hapa.
Akitoka kushinda mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mserbia huyo anahitaji pointi tatu zaidi mwishoni mwa wiki Mkwakwani.
Katika mechi nne za Ligi Kuu, ambazo Goran ameiongoza Simba SC, ameshinda mbili dhidi ya Ndanda FC 2-0 mjini Mtwara na 2-1 dhidi ya JKT Ruvu, wakati amefungwa 2-1 Mbeya City na kutoa sare ya 1-1 na Azam FC.
0 comments:
Post a Comment